Mahakama yaibana Uber haki za madereva

Mahakama yaibana Uber haki za madereva

Muktasari:

Madereva nchini Uholanzi wanakuwa miongoni mwa nchi zilizoipeleka Uber mahakamani kudai haki zao za ujira wakati Uingerezawakipewa mikataba ya ajira.

The Hague, Uholanzi. Mahakama nchini Uholanzi imesema madereva wote wanaoendesha teksi zinazotumia programu ya Uber ni waajiriwa wa kampuni hiyo yenye makao makuu nchini Marekani.

Kesi ya hukumu hiyo iliyotolewa jana, ilifunguliwa na Chama cha Wafanyakazi miezi michache baada ya mashtaka mengine kama hayo kufunguliwa katika mahakama nchini Uingereza kudai haki za madereva hivyo kuilazimu kampuni hiyo ya jijini Francisco kuridhia kubadili mkataba wake.

“Uhusiano wa kisheria kati ya Uber na madereva hawa unakidhi vigezo vyote vya mkataba wa ajira. Hii inamaanisha Uber inalo jukumu la kutoa mikataba kwa madereva hawa na madereva wanayo haki ya kulipwa ujira,” imesema hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Jiji la Amsterdam District.

Chama cha Wafanyakazi nchini Uholanzi (FNW) kiliipeleka Uber mahakamani mwishoni mwa Desemba iliyopita kikisema Uber inao mkatab ana madereva wake lakini wakati mwingine inawalipa pungufu ya mshahara wa kima cha chini.

Kwenye hukumu iliyotolewa, majaji walioisikiliza wameiamuru Uber kulipa faini ya dola 59,000 za Marekani (zaidi ya Sh136 milioni) kwa kutotekeleza matakwa ya mkataba wa ajira na madereva hao.

Hata hivyo, Uber inayotoa jukwaa la kidijitali linalowaunganisha madereva huru na wateja wanaohitaji usafiri imesema itakata rufaa kupinga hukumu hiyo.

“Tumeshangazwa na hukumu iliyotolewa na hatujaridhika kwa sababu tunafahamu madereva wengi wanapenda kuwa huru. Wengi hawapendi kujifungia sehemu moja ya kuegesha gari, muda wa kumpata abiria na mahali pa kumchukua,” alisema Maurits Schoenfeld, meneja mkuu wa kampuni ya Uber kanda ya Ulaya Kaskazini alipozungumza na Shirika la Habari la AFP.

Kwenye utetezi wake mahakamani, Uber ilisema ni ngumu kuwaajiri zaidi ya madereva 10,000 ilionao nchini humo kwa mara moja huku 5,200 wakiwa jijini Amsterdam.

Mapema Machi, Uber iliwapa ajira madereva wake wote nchini Uingereza hivyo kuanza kuwalipa haki zao kikiwamo kima cha chini cha mshahara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu ingawa imegoma kufanya hivyo katika mataifa mengine inakotoa huduma ikisema madereva hao ni vibarua wenye shughuli nyingine.

Jijini California, Marekani, mahakama iliwataka madereva hao kutambulika kama makandarasi huru.