Mahakama yamtaka Lissu, yeye aeleza hofu yake kurejea Tanzania

Muktasari:

Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anahitaji kurejea nchini lakini anahofia usalama wake.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anayekabiliwa na kesi ya uchochezi ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anahitaji kurejea nchini lakini anahofia usalama wake.

Wakati Lissu akieleza hayo kupitia kwa mdhamini wake,  Ibrahim Ahmed, Mahakama hiyo imesema inamtaka mahakamani na kutoa msisitizo wa mdhamini wake kuhakikisha jambo hilo linafanyika.

Novemba 21, 2019 Mahakama hiyo iliwataka wadhamini wa mwanasheria mkuu huyo wa Chadema kuhakikisha wanampeleka mahakamani ili kesi ya msingi iendelee.

Lissu ambaye leo Alhamisi Desemba 19, 2019 amechaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa Chadema, amewasilisha maelezo yake hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Thomas Simba kupitia kwa Ahmed.

Septemba 7, 2017, Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye gari nje ya makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.

Baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma kisha usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako alitibiwa hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa Ubelgiji kukamilisha matibabu na sasa amepona.

Katika maelezo yake mahakamani, Ahmed amedai alifanya utaratibu kama alivyoelezwa na Mahakama, alipomfikishia mteja wake agizo hilo alijibiwa kuwa anatamani kurejea nchini lakini ana hofu na usalama wake.

“Nilifanya kama Mahakama ilivyonituma mshtakiwa aje kwenye shauri lake. Leo nilizungumza naye nikamueleza anahitaji kurudi nchini lakini akasema bado anajenga hofu ya usalama wake na bado naendelea kumhimiza ili aje,” amesema Ahmed.

Wakili wa Serikali, Silvia Mitanto amedai upande wa mashtaka umeshindwa kuleta mashahidi kutokana na mshtakiwa wa nne kutokuwepo.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Simba alimsisitiza mdhamini huyo kuhakikisha Lissu anafika mahakamani kwa kuwa taratibu za dhamana zinaeleweka.

"Tunakusisitiza tunamtaka mshtakiwa mahakamani taratibu za dhamana zinaeleweka kabla sheria haijatekelezwa,” amesema  Hakimu Simba

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 20, 2020.

Lissu na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni  mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina; Jabir Idrisa na mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbooh.

Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam.  Jabir, Mkina na Lissu wanadaiwa kuandika habari  na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi.

 

Kauli za Lissu kurejea Tanzania

Novemba 29, 2019 wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha KTN cha nchini Kenya na mtangazaji, Paul Nabiso, mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki alisema atarejea Tanzania baada ya  marafiki zake kumhakikishia usalama wake.

“Hali  ya usalama wangu bado si nzuri, nafikiri hakuna mtu anayetaka kuona narudi nyumbani kesho na keshokutwa ninapigwa risasi tena. Bado kuna vitisho vya aina hii,  watu wenye busara lazima wakae na kuangalia namna nzuri ya kufanya ili niweze kurudi nyumbani kuendelea na shughuli zangu lakini nikiwa salama.”

“Hizi jitihada zinafanywa na marafiki wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha nakuwa salama kurudi Tanzania. Ikifika mahala wakasema usalama wangu utaangaliwa nitarudi nyumbani. Sitaki kuishi uhamishoni na sipo uhamishoni. Nilienda kwenye matibabu nimeshatibiwa nasubiri niambiwe usalama wangu utakuwaje katika mazingira halisi,” alisema Lissu

Oktoba 9, 2019 wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Sauti ya Marekani (VOA), Lissu alisema kuwa hawezi kurejea Tanzania kwa kuwa mazingira ya  usalama wake si mazuri.

Septemba 7, 2019,  Lissu alikaririwa akisema atarejea Tanzania “mchana kweupe” akitokea Ubelgiji alikoenda kutibiwa, kwamba suala hilo halitakuwa siri kama ambavyo anashauriwa na watu wengi.