Mahakama yamuondoa Bob Wine kizuizini

Mahakama yamuondoa Bob Wine kizuizini

Muktasari:

  • Mahakama kuu nchini Uganda imeviamuru vyombo vya ulinzi nchini humo kuacha kuzingira nyumba ya aliyekuwa mgombea wa kupitia chama cha upinzani (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu Bob Wine.

Kampala. Mahakama kuu nchini Uganda imeviamuru vyombo vya ulinzi nchini humo kuacha kuzingira nyumba ya aliyekuwa mgombea wa kupitia chama cha upinzani (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu Bob Wine.

Uamuzi huo ulitolewa jana ambapo mahakama ilieleza kuwa imebaini kuwa suala la vikosi vya ulinzi wa nchi hiyo kuendelea kuzingira nyumba ya Kyagulanyi linafanywa kinyume cha sheria.

“Kuendelea kwa vizuizi visivyoeleweka na kuzuiliwa kwake katika nyumba yake, ni kinyume na sheria na haki yake ya kuwa huru imevunjwa,” alisema Jaji wa kanda ya Kampala Michael Elubu.

Elubu aliongeza kuwa: “Kwa kubaini kuwa vizuizi hivyo viko kinyume na sheria hivyo, inaamuliwa kuwa viondolewe”.

Bob Wine ambaye alikuwa mshindi wa pili katika uchaguzi wa Januari 14, 2021 uliomrudisha Rais Yoweri Museveni Ikulu kwa awamu ya sita, aliwekwa kizuizini nyumbani kwake na maofisa wa ulinzi tangu siku ya uchaguzi.

Makumi ya maaskari polisi na wanajeshi wenye silaha wamekuwa wakiizingira nyumba ya mwanamuziki huyo wa zamani kwa zaidi ya siku 10. Yeye, mkewe na wengine waishio humo ndani hawakuruhusiwa kutoka.

Wiki iliyopita Balozi wa Marekani nchini alizuiliwa kumtembelea Bob Wine na baadaye Serikali ilimtuhumu balozi huyo kwa kuvunja maadili ya kidiplomasia.

Msemaji wa Serikali ya Uganda Ofwono Opondo alisema: “Tulitarajia kuwa balozi angemuandikia barua Waziri wa mambo ya nje na kufuata maadili ya kidiplomasia. Hatudhani kuwa taifa rafiki au yeyote anayetaka kusaidia katika nyakati ngumu anaweza kufanya hivyo,”

Kwa mujibu wa Shirika la habari la AFP Serikali ya Uganda imeeleza Bob Wine amezuiliwa kwa sababu za ulinzi wake binafsi na kuzuia maandamano ya kupinga uchaguzi uliompa ushindi Rais Museveni.

Aidha, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda (EC) Rais Museveni ambaye alikuwa mgombea wa chama tawala cha NRM alishinda kwa kura 5,851 037 sawa na asilimia 58.64 huku Bobi Wine wa chama cha NUP akipata kura 3,475 298 sawa na asilimia 34.83.

Awali wakati mchakato wa kuhesabu kura ukiendelea Bobi Wine aliwaeleza waandishi wa habari kuwa hayatambui matokeo yanayoendelea kutangazwa na badala yake alijitangaza kama mshindi wa Urais.

Bob Wine ambaye alijiita Rais mteule alidai kushinda katika uchaguzi wa Rais huku akikataa matokeo ya awali yaliyotolewa na kuonyesha Rais Yoweri Museveni anaongoza katika kinyang’anyiro hicho.

“Nina imani kubwa kwamba tumemshinda dikteta. Ninatoa wito kwa Waganda wote kukataa hujuma hii. Ni wazi kabisa tumeshinda uchaguzi na tumeshinda kwa mbali. Watu wa Uganda watakataa na lazima wakatae unyang’anyi huu wa wazi wa na sauti yao,’ alisema.

Bob Wine alidai kuwa kulikuwa na wizi na mawakala wake pamoja na wawakilishi wameendelea kukamatwa, alisema uchaguzi huo ulitawaliwa na wizi mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Uganda, lakini hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai hayo badala yake alisisitiza kuwa mapambano yameanza