Mahakama yamuongezea Seth na mwenzake siku 15 kujadiliana na DPP

Mahakama yamuongezea Seth na mwenzake siku 15 kujadiliana na DPP

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku 15 kuanzia leo Alhamisi Aprili 8, 2021  kwa mwenyekiti mtendaji wa PAP, Harbinder Seth na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya IPTL, Joseph Makandege kukamilisha majadiliano ya kukiri mashtaka yao waliyoyawasilisha kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku 15 kuanzia leo Alhamisi Aprili 8, 2021  kwa mwenyekiti mtendaji wa PAP, Harbinder Seth na aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya  kufua umeme ya IPTL, Joseph Makandege kukamilisha majadiliano ya kukiri mashtaka yao waliyoyawasilisha kwa mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP).

Imetoa uamuzi huo baada ya siku 30 zilizotolewa na mahakama hiyo kuisha bila wawili hao kufanya majadiliano na DPP.

Februari 25, 2021 mahakama hiyo iliamuru majadiliano ya kukiri mashtaka yaliyowasilishwa kwa DPP na washtakiwa hao, yasikilizwe ndani ya siku 30, kuanzia siku hiyo.

Leo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, mawakili wa washtakiwa hao, Dorah Malaba na Joseph Sungwa wameieleza mahakama hiyo kuwa hawajaweza kufanya majadiliano na DPP kwa ajili ya kuimaliza kesi hiyo.

 "Inaonekana upande wa mashtaka hawana nia ya kufanya majadiliano na wateja wetu, tunaomba waharakishe kukamilisha upelelezi ili kesi hii iweze kuendelea na hatua nyingine" amedai wakili Malaba.

Akijibu hoja hizo wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon akisaidiana na Faraja Ngukah,  amedai kuwa upande wa utetezi ndio wanaostahili kulaumiwa kwa sababu hawajafuatilia kujua majadiliano yamefikia hatua gani.

Kuhusu upelelezi, wakili Simon amedai watawasiliana na wapelelezi wa kesi hiyo kujua hatua waliyofikia katika upelelezi.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema sio wajibu wa washtakiwa kufuatilia majibu kwa DPP, bali DPP ndio anapaswa kutoa majibu kuhusiana na majadiliano hayo.

"Ni kweli mahakama ilitoa siku 30 kwa upande Jamhuri na washtakiwa hawa wawili wakae na kufanya mazungumzo ya kuimaliza kesi yao, sasa naambiwa siku zimeisha majadiliano bado," amesema Shaidi.

Ameeleza kuwa kutokana na hali hiyo ametoa siku 15 kuhakikisha kuwa washtakiwa na DPP wanakaa na  kufanya majadiliano kwa ajili ya kuimaliza kesi hiyo.

Kesi hiyo imeahirisha hadi Aprili 22, 2021 na mahakama imetoa hati ya kuwaita mahakamani washtakiwa hao siku kesi hiyo itakapotajwa.

Mbali na washtakiwa hao, mshtakiwa mwingine ni mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemalira.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 likiwemo la kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh309,461,300,158.27.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam ikielezwa walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.