Mahakama yapiga kalenda kesi ya Rais TCCIA aliyesimamishwa

Paulo Koyi

Muktasari:

Mahakama kuu Kanda ya Dodoma imeahirisha kesi ya maombi madogo ya kurudishiwa hadhi ya aliyekuwa Rais wa Chemba ya biashara, viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Paul Koyi.

Dodoma. Mahakama kuu Kanda ya Dodoma imeahirisha kesi ya maombi madogo ya Rais wa Chemba ya biashara, viwanda na kilimo (TCCIA), Paulo Koyi ya kutaka kurudishiwa hadhi yake ya kutambulika kama Rais halali wa Chemba hiyo.

Uamuzi wa kuahirisha shauri hilo umetolewa leo Novemba 28 na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Cylvia Lusashi ambaye ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, 2023 kwa ajili ya kusikiliza amri zinazostahiki.

Novemba 2, 2022 Juzi, Halmashauri Kuu ya Taifa ya TCCIA ilimsimamisha Koyi kwa madai ya kutoridhishwa na utendaji wake baada ya kufanya kikao chake jijini Dodoma.

Leo Wakili anayemwakilisha Kiongozi huyo, Ruto Stephen amewasilisha maombi ya kupinga kusimamishwa kwa mteja wake katika nafasi hiyo.

Maombi hayo madogo namba 56 ya mwaka 2022 yanatoka kwenye kesi ya msingi namba 21/2022 ambayo Rais huyo aliiomba Mahakama itamke kwamba, uamuzi wa kumsimamisha uliofanywa Oktoba 31, 2022 ulikuwa batili.

Aidha katika kesi hiyo, Koyi ameiomba Mahakama itamke kuwa kikao cha Halmashauri kuu (NEC) kilichofanywa na TCCIA cha kumsimamisha kilikuwa hakina mamlaka hayo, hivyo imtambue kuwa bado Rais halali wa Chemba hiyo hivyo aendelee na shughuli zake kama kawaida.

Kwa upande wake Wakili upande wa walalamikiwa (Chemba), Alex Mgongolwa amesema Koyi alitoa ombi Mahakamani hapo la kutaka kurudishiwa hadhi yake ya kuwa Rais wa Chemba hiyo hadi Mahakama itakapotoa uamuzi.

Amesema upande wa Chemba hiyo umeweka mapingamizi kadhaa ambapo shauri hilo lilitakiwa kusikilizwa, hivyo kumlazimu Naibu Msajili aliyekaa kusikiliza kesi hiyo kuiahirisha.

“Hadhi iliyopo sasa hivi mpaka kesi hii ilipo ni kwamba Paul Koyi ana hadhi yake ya kusimamishwa kwenye uongozi wa Chemba ya biashara, viwanda na kilimo,” amesema Mgongolwa.