Mahakama yatengua hukumu Kilimanjaro Express kumlipa Kisena Sh300 milioni
Muktasari:
- Mahakama Kuu imetengua uamuzi wa fidia ya Sh300 milioni kwa Leonard Kisena dhidi ya Kilimanjaro Express, ikiamuru kesi isikilizwe upya. Kisena kukata rufaa kupinga uamuzi huo.
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua hukumu iliyompa ushindi Leonard Kisena, wa kulipwa fidia ya Sh300 milioni na kampuni ya mabasi ya Kilimanjaro Truck Ltd, baada ya kusababisha ajali iliyosababisha kifo cha mtoto wake, Immaculate Kisena (16).
Badala yake, mahakama hiyo imeelekeza mwenendo wa shauri la madai namba 47/2022 lililofunguliwa na Kisena lisikilizwe upya.
Uamuzi huo umetolewa leo, Septemba 13, 2024 na Jaji Wilfred Dyansobera baada ya mahakama hiyo kukubali maombi yaliyowasilishwa na Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd, kupitia wakili wake Dickson Ngowi, ikiomba mwenendo wa shauri hilo usikilizwe upya.
Hata hivyo, Kisena kupitia wakili wake, Dk Aloys Rugazia amewasilisha kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo uliotolewa na Jaji Dyansobera.
Uamuzi uliokuwa unaopingwa na kampuni ya Kilimanjaro ni wa Desemba 21, 2022, uliimpa ushindi Kisena baada ya mahakama hiyo kuamuru imlipe Kisena Sh300 milioni ikiwa ni fidia kutokana na ajali ya basi la Kilimanjaro Express lilisababisha kifo cha mtoto wake.
Uamuzi wa Jaji
Akitoa uamuzi wake leo, Jaji Dyansobera amesema mahakama hiyo imetengua uamuzi wa awali uliotolewa na mahakama hiyo kwa kuwa ulikuwa na dosari kisheria.
Jaji Dyansobera amesema mahakama hiyo imekubaliana na maombi Kilimanjaro Truck Ltd, ambayo ilikuwa inaomba mwenendo wa shauri hilo usikilizwe upya kwa madai kuwa shauri hilo awali lilisikilizwa upande mmoja.
Amesema maombi hayo yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura, yalitakiwa kutolewa uamuzi mapema zaidi, licha ya kwamba upande wa pili (Kisena) nao uliwasilisha pingamizi ukiomba maombi ya Ngowi yasifanyiwe kazi kwa kuwa yaliwasilishwa nje ya muda kisheria.
Baada ya kutoa uamuzi huo, Jaji Dyansobera amesema kwa sasa jalada la shauri hilo analirudisha kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo kwa ajili ya hatua nyingine, ikiwemo kupangiwa jaji wa kuanza kulisikiliza shauri hilo upya.
Katika maombi hayo, Kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd, kupitia Wakili Ngowi, iliwasilisha mamba kadhaa yakiwemo ya kuomba kuongezewa muda na kuwa mahakama hiyo iruhusu shauri hilo lisikilizwe upya kwa kuwa lilisikilizwa upande mmoja.
Hata hivyo, Wakili wa Kisena, Dk Rugazia akisaidiana na Valentina Charles, alisema makosa ya kimwenendo hayawezi kukosolewa katika mahakama iliyofanya uamuzi, na kwamba tayari mteja wake alishawasilisha pingamizi Mahakama ya Rufani, kupinga waleta maombi kuongezewa muda na mahakama.
Alisema Mahakama Kuu ilipaswa kusubiri maamuzi ya mahakama ya juu ndipo iendelee na usikilizwaji wa shauri hilo.
Dk Rugazia aliongeza kuwa waleta maombi walipaswa kukata rufaa kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai (CPC), Kifungu cha 70 (2), lakini si kwa maombi hayo ambayo hata hivyo yaliwasilishwa nje ya muda.
Wakili Rugazia alidai kabla ya usikilizwaji wa kesi hiyo na kumpa haki mteja wake, waleta maombi walipewa fursa ya kwenda kwenye usuluhishi lakini hawakutokea mara tatu, ndipo jalada likarejeshwa kwa Jaji Leila Mgonya ili kesi iendelee.
Alidai kuwa wadaiwa hao pia hawakuwahi kufika mahakamani, hivyo haoni sababu ya shauri hilo kuanza upya kwa kuwa uamuzi uliotolewa ulikuwa halali.
Alidai kuwa mteja wake licha ya kupata madhara na kupoteza mtoto, wadaiwa hawakuthamini ubinadamu, kwani baada ya ajali hiyo hakuna mtu yeyote kutoka katika kampuni hiyo aliyekwenda nyumbani wala kupiga simu kutoa pole.
Chimbuko la kesi
Kiini cha shauri hilo ni ajali hiyo ilitokea Desemba 24, 2021, saa 11:15 alfajiri, eneo la Kerege wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, wakati Kisena alipokuwa akisafiri na familia yake, wakiwamo watoto wawili na mkewe, kwenda kwao Kilimanjaro kwa ajili ya kusherehekea za Krismasi na mwaka mpya, akitumia gari lake binafsi.
Katika ajali hiyo, Kilimanjaro Express aina ya Scania, lililokuwa likiendeshwa na Mjahid Mohamed, kutoka Kilimanjaro, liliacha njia na kuliparamia gari la Kisena aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T.323 CWB.
Kufuatia ajali hiyo, mtoto wake wa kike, aliyekuwa na umri wa miaka 16, alifariki dunia. Kisena, mkewe na mtoto wao mwingine wa kiume walinusurika japo walipata majeraha.
Baada ya ajali hiyo, dereva wa basi hilo, Mohamed, alifunguliwa kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo, akikabiliwa na mashtaka manne ya kuendesha gari lisilokuwa na bima, kusababisha kifo, kusababisha majeraha, na kusababisha madhara ya uharibifu wa mali kwa kuendesha gari kwa uzembe.
Dereva huyo alikiri makosa hayo na Aprili 5, 2022, Hakimu Mwanakombo Mmanya alimtia hatiani na kumhukumu adhabu ya kulipia faini ya jumla ya Sh110, 000 kwa makosa yote au kifungo cha miezi sita jela akishindwa kulipa faini hiyo. Alilipa faini na kuachiwa huru.
Baada ya hukumu hiyo, ndipo Kisena alipofungua kesi ya madai Mahakama Kuu kudai fidia.
Katika kesi hiyo ya madai namba 47 ya mwaka 2022 dhidi ya kampuni hiyo, Rowland Sawaya (Mkurugenzi mtendaji na mmiliki wa kampuni hiyo) na dereva wa basi hilo, Mjahid Mohamed.
Kisena alikuwa anadai fidia ya Sh400 milioni, ikijumuisha madhara ya jumla na ya hasara halisi kama vile gharama za matengenezo ya gari lake lililoharibiwa, gharama za matibabu ya majeruhi na mazishi ya marehemu.
Kesi hiyo ilisikilizwa na Jaji Mgonya ambaye katika hukumu yake Desemba 21, 2022 iliyosomwa na Naibu Msajili Joseph Luambano, alikubaliana na hoja za upande wa madai na kuiamuru Kampuni ya Kilimanjaro Truck Company Limited, inayomiliki mabasi ya Kilimanjaro Express, kumlipa Kisena fidia ya Sh300 milioni na riba ya asilimia saba kwa mwaka kuanzia tarehe ya hukumu mpaka kukamilisha malipo yote.
Jaji Mgonya aliridhika na ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Kisena dhidi ya kampuni hiyo.
Tangu itolewe hukumu hiyo na mahakama, utekelezaji wake haukufanyika, ndipo Kisena kupitia wakili wake aliporudi mahakamani kukazia hukumu hiyo.
Baada ya kukazia hukumu, basi aina ya Scania liliamuriwa kupigwa mnada, na tayari lilikuwa mikononi mwa dalali wa mahakama, ambaye ni Daniel Mbuga wa Legit Auction Mart, na mnada wake ulipangwa kufanyika Septemba 13, 2024.
Kutokana na hali hiyo, mawakili wa kampuni ya Kilimanjaro Truck Ltd, waliwasilisha maombi kwa hati ya dharura, wakiomba mahakama hiyo itupilie mbali uamuzi uliotolewa, na badala yake iamuru mwenendo wa shauri hilo usikilizwe upya.
Nje ya mahakama
Dk Rugazia amesema tayari amewasilisha kusudio la kukata rufaa kwenda Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo na kuwa sasa wanasubiri nakala ya uamuzi na tamko lililotokana na uamuzi huo ili waendelee na hatua nyingine.
Kwa upande wake, Kisena amesema ameupokea uamuzi huo ambao kwake anaona haujatenda haki na ni wa dhuluma.