Mahindi yaliyozuiwa kuingia Kenya yarejeshwa Tanzania
Muktasari:
- Magari yenye shehena ya mahindi kutoka Tanzania yaliyokuwa yamezuiwa katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Namanga kwa zaidi ya mwezi mmoja yameanza kurudi nchini.
Arusha. Magari yenye shehena ya mahindi kutoka Tanzania yaliyokuwa yamezuiwa katika mpaka wa Kenya na Tanzania eneo la Namanga kwa zaidi ya mwezi mmoja yameanza kurudi nchini.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Aprili mosi, 2021 mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe amesema shehena ya mahindi hayo imerejeshwa nchini kutokana na kutopatikana muafaka kutoka nchi ya Kenya juu ya taratibu za kuzuia sumu kuvu.
"Wameanza kuondoa mahindi hapa mpakani kwani bado taratibu rasmi hazijatolewa na Serikali ya Kenya na jambo hili limekuwa na hasara kubwa kwa wakulima na wafanyabiashara," amesema.
Hata hivyo, amesema mahindi mengi yamepata masoko katika nchi nyingine za Malawi, Zambia na Burundi.
Mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji wa bidhaa ya mahindi katika mpaka wa Namanga, Daniel Wainaina aliomba kusitishwa agizo la kuzuiwa mahindi kuingia Kenya kwani limekuwa na hasara kwa wafanyabiashara na wakulima.
"Jambo hili linaathiri ushirikiano wa Afrika Mashariki kwani miaka mingi Kenya wamekuwa wakiingiza mazao kutoka Tanzania bila tatizo," amesema
Mkaguzi wa mazao wa mamlaka ya kilimo na chakula nchini Kenya, Calistus Efuko amesema bado msimamo wa Serikali ni kulinda afya ya walaji na hakuna mabadiliko hadi wajiridhishe mahindi kutoka Tanzania hayana sumu kuvu.