Majaliwa ataja mbinu kulinda viwanda vya ndani

Friday December 04 2020
majaliwa pic
By Aurea Simtowe

Dar es Salaam. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa maelekezo mbalimbali kwa mamlaka za serikali ikiwa ni hatua ya kulinda viwanda vya ndani na kuhamasisha Watanzania kutumia bidhaa za ndani.

 Majaliwa amewataka wamiliki wa viwanda kuzalisha bidhaa kwa wingi, bora na kutumia malighafi zinazopatikana katika maeneo yao, bidhaa bandia na zisizo na viwango zisiingie katika soko la Tanzania na kupunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje zinazozalishwa ndani.

Ameyasema hayo leo Ijumaa Desemba 4, 2020 wakati akizindua maonyesho ya tano ya bidhaa za viwanda vya Tanzania yanayofanyika katika uwanja wa maonyesho wa Sabasaba yanayotarajiwa kukamilika Desemba 9, 2020.

Majaliwa amesema malengo ya Serikali ni kuwa hadi kufikia mwaka 2025 watanzania wote wenye dhamira ya kuwekeza wawe wamefanya hivyo na wamepata masoko huku akizitaka mamlaka zinazohusika na biashara kuieleza mifuko inayoweza kuwapatia mikopo.

Amesema ili kuimarisha na kukuza bidhaa za ndani ni lazima kuimarisha eneo la mitaji kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo.

“Tunamalizia mchakato wa kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii inayofanya kazi zinazofanana kuwa mmoja na unaojulikana na kazi zake.”

Advertisement

“Niwahakikishie kuwa eneo la mitaji hili tunaendelea kuliimarisha kupitia benki mbalimbali zinatoa mikopo hadi kiwango cha chini, suala la mitaji na mikopo katika biashara  zenu tunalirahisisha maana huwezi kufanya biashara au uwekezaji bila kukopa ingawa kukopa lazima ulipe lakini mitaji ipo katika taasisi na mifuko tunayoiratibu,” amesema Majaliwa.


Advertisement