Majaliwa awajibu kiaina wanaobeza mradi wa umeme

Majaliwa awajibu kiaina wanaobeza mradi wa umeme

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni kama amewajibu baadhi ya viongozi wanaoubeza mradi wa kufua na kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa kusema ni wa uhakika, utakamilika kwa wakati na utakuwa wa gharama nafuu.

Rufiji. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni kama amewajibu baadhi ya viongozi wanaoubeza mradi wa kufua na kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa kusema ni wa uhakika, utakamilika kwa wakati na utakuwa wa gharama nafuu.

Juzi mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo aliukosoa mradi huo alipokuwa akichangia hoja bungeni, akisema umewekezwa kwa fedha huku akiitaka Serikali kuachana na mradi huo kwa kuwa utachelewa faida.

Profesa Muhongo, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini alisema: “Ni vyema Serikali ikaachana na miradi ya uzalishaji umeme wa maji, inachelewa kuleta faida na ili kuupatia faida lazima uwe umewekeza fedha nyingi na unahitaji miaka mingi ili kupata faida ndio umeme wa maji uwe bei chini.”

Pia, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iliutaja mradi huo kujengwa kwa kutumia upembuzi yakinifu wa mwaka 1970 pamoja na kuelezea kasoro nyinginezo.

Lakini akizungumza juzi, Waziri Mkuu Majaliwa aliyetembelea eneo la mradi unaotumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji, alisema utarahisisha uhakika wa upatikanaji wa umeme nchini.

Alisema umeme huo utakuwa nafuu ikilinganishwa na vyanzo vingine vya umeme, ikiwamo mafuta na gesi ambavyo gharama zake ni kubwa maradufu.

Majaliwa alisema umeme huo mkubwa utakaozalishwa kwa megawati 2,115 ukichanganywa na unaopatikana sasa wa megawati 1,500, utaiwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha, usiokatika ovyo na kupata ziada itakayouzwa nje ya nchi.

“Kukamilika kwa mradi huu mkubwa kutawafanya wananchi kulipa umeme kwa gharama nafuu ya Sh36 kwa uniti moja na hata kukiwa na gharama za uendeshaji kwa kiasi gani haitaweza kuzidi Sh50 kwa uniti moja,” alisema Majaliwa.

Pia, alisema gharama ya gesi ni Sh147 kwa uniti moja na umeme wa mafuta unaohitaji majenereta kuuendesha ni Sh440 hadi Sh600 na ndio unatumika kwa sasa. Alimtaka mkandarasi mjenzi, Kampuni za JV Arab Contractors na Elsewedy Electric za Misri kukamilisha mradi huo kwa ubora na wakati ili kudhihirisha uhusiano mzuri na urafiki uliopo baina ya Tanzania na Misri.

Mradi huo mkubwa wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere unatarajiwa kukamilika Juni 2022 na kukabidhiwa kwa Serikali. Shughuli zote zilizo ndani ya mkataba tayari zimekamilika kwa asilimia 100.

Pia, Waziri Mkuu alisema mradi huo ni utekelezaji wa maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere yaliyoanzishwa na hayati Rais John Magufuli na unaendelezwa na Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan.

Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato alisema Serikali imeshalipa Sh2.12 trilioni kati ya Sh6.5 trilioni zinazotarajiwa kukamilisha mradi huo wa umeme.

“Tunaishukuru Serikali kwa ufadhili wa mradi huu na fedha zinalipwa kwa wakati kwa mkandarasi kila hatua kwa asilimia 100, hakuna deni kwa mkandarasi na spidi inaridhisha,” alisema.

Waziri Mkuu alitembelea kingo za kuzuia maji, eneo la kuchepusha maji lenye mitambo na maporomoko ya maji, daraja la kudumu litakalokuwa la pili kwa ukubwa baada ya lile la Mkapa la Mto Rufiji.

Pia alitembelea eneo la kupokea umeme utakaozalishwa kupelekwa Chalinze ili kupozwa na kusambazwa kwenda Dodoma na Kinyerezi kisha kusambazwa nchini kupitia gridi ya Taifa.