Majaliwa kuongoza waombolezaji mazishi mbunge wa CCM

Tuesday January 26 2021
majaliwapic
By Joseph Lyimo

Mbulu. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kasim Majaliwa ataongoza mazishi ya aliyekuwa mbunge wa viti maalumu CCM  Mkoa wa Manyara, Martha Umbulla  yatakayofanyika leo Jumanne Januari 26, 2021 katika kata ya Dongobesh wilayani Mbulu.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga ameeleza hayo leo katika kanisa la KKKT Dongobesh Dayosisi ya Mbulu.

Mofuga amesema Majaliwa ataongoza mazishi hayo na kwamba ibada ya mazishi itafanyika kwenye Kanisa la KKKT Dongobesh Dayosisi ya Mbulu na mwili utazikwa kwenye uwanja wa nyumbani kwake hapo Dongobesh.

"Hivi sasa viongozi mbalimbali wameshafika kwenye eneo hili akiwemo  naibu spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na katibu mkuu wa jumuiya ya umoja wa wanawake wa CCM (UWT) Queen Mpoli," amesema Mofuga.

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo amesema amepoteza mjumbe wa kamati hiyo ambaye alitamani kufanya kazi naye kutokana na uzoefu alionao.

"Tunamuombea Mungu ampumzishe mahali pema peponi marehemu mbunge mwenzetu ambaye tumeungana na wananchi wa Manyara na mikoa mingine katika mazishi haya," amesema Sillo.

Advertisement

Mbunge wa Kiteto, Edward Ole Lekaita  amesema Martha alikuwa kiongozi mwenye msimamo kwani mwaka 2016 alikuwa Mkuu wa wilaya ya Kiteto na aliongoza vyema eneo hilo.

Mwananchi wa Kata ya Dongobesh, Isaya Tluway amesema mbunge huyo alikuwa anashiriki kwenye mambo mbalimbali ya maendeleo na kwenye shughuli za kijamii.

Mkazi wa kata ya Dongobesh, Rachel Thomas amesema Martha alikuwa akiwapenda wanawake na aliwapigania kuhakikisha wanapata mikopo aliyoitoa kwenye taasisi ya Wedac LTD.

Martha  amezaliwa mwaka 1955 kijiji cha Dongobesh wilayani Mbulu mkoani Manyara na kufariki dunia Januari 21, 2021 wakati akipatiwa matibabu nchini India.

Amekuwa mbunge wa viti maalum Mkoa wa Manyara kwa miaka 16 mfululizo kuanzia mwaka 2005 hadi mauti ilipomkuta.
Advertisement