Prime
Majanga safari za mabasi usiku
Muktasari:
- Mwezi mmoja tangu Serikali iruhusu safari za mabasi kwa saa 24, tathimini ya mamlaka za usimamizi imeonyesha kuwepo ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za usalama barabarani, hali inayohatarisha usalama kwa abiria na mali zao.
Dar es Salaam. Mwezi mmoja tangu Serikali iruhusu safari za mabasi kwa saa 24, tathimini ya mamlaka za usimamizi imeonyesha kuwepo ukiukwaji mkubwa wa sheria na kanuni za usalama barabarani, hali inayohatarisha usalama kwa abiria na mali zao.
Kutokana na ukiukwaji huo, ndani ya muda huo mabasi 759 yamekamatwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) kwa kushirikiana na Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuzidisha mwendo na kuchezea mfumo wa VTS unaodhibiti na kutoa taarifa za kasi ya gari.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo na Kamanda wa Trafiki, Ramadhan Ng’anzi ilieleza kati ya mabasi hayo, 723 yalipewa onyo na mengine kusitishiwa leseni.
“Mabasi yaliyositishiwa leseni mpaka mamlaka itakapojiridhisha kwamba wamebadilika ni 36.
“Kati ya mabasi 246, asilimia 80 (mabasi 197) yamebainika yanaendeshwa kwa mwendo kasi kati ya kilomita 86 hadi 89 kwa saa, huku asilimia tisa yakiendeshwa kwa kilomita 90 hadi 103 kwa saa,” ilisema.
Taarifa hiyo imeonyesha tangu safari za saa 24 zilipoanza Oktoba mwaka huu, madereva waliofungiwa kwa kuchezea mfumo ni 10, walioandikiwa faini kwa makosa ya mwendokasi ni 666, waliofikishwa mahakamani 32 na walioonywa 50.
“Baada ya kumaliza kutumikia adhabu, dereva atatakiwa kuomba kufunguliwa na ofisi ya kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani na kabla ya kufunguliwa atalazimika kutahiniwa ili kupimwa uwezo wake kwenye taaluma ya udereva.
“Na iwapo atafaulu atarejeshewa madaraja ya leseni yake kama atatetea sifa ya kuendelea kumiliki madaraja hayo,” ilisisitiza taarifa hiyo ya pamoja.
Taasisi hizo katika kufuatilia mwenendo wa utoaji huduma kwa kutumia nyenzo mbalimbali, zikiwemo, mfumo wa VTS, ratiba za mabasi, ukaguzi wa maeneo mbalimbali, zimebaini mabasi yameunganishwa kwenye VTS, lakini baadhi ama hazitumi taarifa kabisa au zinatuma taarifa kwa kurukaruka kutokana na kuchezewa kwa mfumo huo.
Pia imebainika kuna madereva ambao hawabonyezi kitufe cha kuwatambulisha (i-button), kutokana na ama hawajasajiliwa, wanasafiri dereva mmoja kwa basi, au wanakwenda safari ya usiku na kurudi mchana bila kupumzika vya kutosha.
Taasisi hizo zimebaini kuwepo vituo vya ukaguzi wa safari ndefu na ubadilishanaji wa madereva, hakuna taarifa ya ubadilishanaji, ambazo wangeziona pia kwa i-button.
i-bottom ni kitufe kidijitaji anachopewa dereva kikiwa kimesajiliwa kwa mfumo wa namba yake ya Kitambulisho cha Taifa (Nida) ambacho kinakuwa na uwezo wa kumulika na kunasa matukio yote yanayofanywa kwa safari nzima na kurusha taarifa hizo kwa mfumo wa satellite kwa mamlaka.
Tiketi mtandao
Kuhusu matumizi ya tiketi mtandao, taarifa hiyo ilieleza kubwa tathmini hiyo ilibaini asilimia 98 ya mabasi yote yanatumia mfumo huo, ingawa taarifa za abiria haziingizwi ipasavyo na orodha ya abiria haiachwi kwenye vituo vya kuanzia safari.
Kabla ya mabasi kuruhusiwa kwa safari hizo, Septemba 29 mwaka huu, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo na Ndani, Jumanne Sagini alitoa tahadhari kwa madereva watakaofanya safari hizo kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu wa leseni zao kuepuka ajali.
Taboa, madereva wakosoa
Matokeo ya ufuatiliaji huo yamekosolewa na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kilichozitaka taasisi hizo ziache kuingiza siasa katika kwenye shughuli za kiutendaji.
Mkurugenzi wa Habari wa Taboa, Mustapha Mwalongo alisema maofisa hao wanatoa taarifa kutaka kuchochea na kuonekana wanafanya kazi.
“Sisi tupo kwa ajili ya kutoa huduma, hatuko kwa ajili ya kufanya siasa, huwezi kufungia basi la mtu kwa kipindi fulani kwa kuwa ni hasara, ni vizuri wakampiga mtu faini akiri kosa maisha yaendelee,” alisema.
Alisema kumsitishia mtu mradi wake kunaleta athari kubwa kiuchumi kwa jamii kubwa, kwa kuwa mwekezaji hafanyi kazi hizo mwenyewe, kuna watu wameajiriwa, wakiwemo madereva.
“Hawa wanapaswa kujikita kutoa elimu badala ya kufungia leseni,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamata), Majura Kafumu alisema kabla ya kuchukuliwa uamuzi wa kufungia leseni za madereva, mamlaka zinapaswa kujiuliza vyuo vinavyofundisha watu kuwa madereva vimekidhi vigezo?
“Kama kila siku sheria zipo na dereva anavunja makusudi, unapatwa na wasiwasi na chuo kilichomfundisha kama kinakidhi viwango vya kuzalisha mtu wa kwenda kutoa huduma kwa jamii bila kuleta madhara,” alisema.
Alisema mamlaka zisipochukua hatua, Tanzania itashangaza dunia kwa takwimu kubwa za ajali kwa kuwa hata madereva wa malori, bajaji na bodaboda wamegeuza sehemu ya kutembea abiria kwa miguu kuwa sehemu za kupakia abiria, jambo ambalo ni hatari.
“Ikitokea ajali maeneo hayo utamsingizia Mungu, ni ajali za kutengeneza na tunashuhudia madereva ambao si weledi ilimradi tu wamemaliza chuo mamlaka zinatoa leseni,” alisema.
Kafumu alisema chama hicho kimebaini vyuo vilivyopo havijakidhi vigezo vya kuzalisha watu watakaokuja kutoa huduma kwa kuzingatia matakwa ya sheria na wamekuwa wakiendesha mabasi kwa kushangaza.
Gazeti hili limezungumza na mmoja wa abiria aliyesafiri safari ya usiku kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, Said Mohamed aliyesema wakiwa njiani walinusurika mara tatu, basi alilopanda lilipoingia kwenye mtaro.
“Muda mwingi dereva alionekana analala usingizi na walikuwa wawili, lakini walionekana wamechoka kwa kuwa walikuwa wanafanya kazi bila kupumzika. Ni muhimu wakaongezwa madereva hata kufikia watatu ili kuepusha ajali siku za usoni,” alisema.