Makali ya maji kama kawaida

Muktasari:

Mmoja wa watumiaji wa huduma hiyo, John Mgaya anayefanya shughuli zake katika eneo la Kimara alisema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji gharama ya huduma hizo imepanda kufikia hadi Sh1,000 kwa kuoga na Sh300 kwa haja ndogo na kubwa.

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku chache tangu kuzinduliwa kwa mradi wa maji wilayani Kigamboni unaozalisha lita milioni 70 ili kupunguza adha katika baadhi ya maeneo, kilio cha uhaba wa maji kimeendelea kutikisa jijini Dar es Salaam.

Hii si mara ya kwanza kwa jiji hili kukumbwa na hali hii. Novemba mwaka jana kulitokea upungufu wa kina cha maji Mto Ruvu ambao ndiyo chanzo cha maji na kusababisha mgawo wa huduma hiyo kama ambavyo imetokea mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.

Novemba 11 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mradi huo ulioelezwa kuwa kati ya lita milioni 70 zinazozalishwa, lita milioni 25 zitahudumia Kigamboni na lita milioni 45 zitavushwa kwenda kuhudumia maeneo mengine ya jiji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), mtandao wa kilomita 65 umejengwa kuwezesha usafirishaji wa maji hayo kufika maeneo ya Kurasini, Keko, Chang’ombe, Kariakoo, Fire, Muhimbili, Tandale na Magomeni.

Kuanza kwa mradi huo kulienda sambamba na utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alilolitoa Novemba 3 mwaka huu akiielekeza Dawasa kuhakikisha visima 197 vilivyo chini ya mamlaka hiyo vinafanya kazi na kupunguza adha ya upungufu wa maji.

Hadi kufikia jana, Dawasa ilionyesha visima 150 kati ya hivyo vilivyokuwa vinafanya kazi kabla ya agizo hilo kutolewa na visima 14 vimefufuliwa kufuatia maelekezo hayo na kufanya mamlaka hiyo kuwa na visima 164 vinavyofanya kazi ambavyo vimeingiza kwenye mfumo lita za maji milioni 30.6.

Akizungumza jana na Mwananchi, Fatma Abdallah, mkazi wa Kimara Suka Golani alisema katika eneo wanaloishi hawajapata maji kwa mwezi mmoja, hivyo wanalazimika kutafuta maji kwa watu wenye visima au kwenda katika eneo la Saranga au Msikitini kupata huduma hiyo ya maji.

“Wakati mwingine kutokana na umbali, tunawatuma madereva bodaboda kufuata maji; kila dumu moja hugharimu kati ya Sh700 hadi Sh1,000 kutegemea makubaliano kati yetu,” alisema Fatma.

Janeth Joseph, mkazi wa Kariakoo alisema takribani wiki tatu hawajapata maji eneo hilo, hali inayowalazimu kununua kutoka kwa wafanyabiashara wanaouza kati ya Sh500 hadi Sh700 kwa dumu.

Mkazi wa Mbezi, Juma Athamuna alisema huduma hiyo wamekuwa wakiisikia zaidi ya mwezi, “hata huu mgawo wanaousema, sisi nafikiri wametusahau. Kwa sababu hatuna maji mwezi sasa.”

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Jamii wa Dawasa, Neli Msuya alisema maji yanayotoka katika mradi wa Kigamboni yanaendelea kusukumwa na yanasafiri taratibu kuelekea katika maeneo mengine ya jiji kama ilivyoelezwa.

“Maji si kama umeme kwamba ukiwasha yanatoka sehemu zote, maji yanasafiri na taarifa ya leo (jana) ni kwamba yameshafika Kariakoo, hivyo yataenda kupunguza adha katika eneo hilo,” alisema Msuya.

“Kuhusu mgawo sawa, kuna mvua kidogo zilizonyesha lakini hatuwezi kusema maji yameongezeka, hivyo tunaendelea kugawana yaliyopo.”

Hata hivyo, wakati mkurugenzi huyo akieleza hayo ikiwa ni saa nane mchana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya wakati wa eneo la Kariakoo ikiwa ni saa kumi jioni ambao walisema huduma hiyo ilikuwa haijafika.

Vyoo vya umma

Mmoja wa watumiaji wa huduma hiyo, John Mgaya anayefanya shughuli zake katika eneo la Kimara alisema kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji gharama ya huduma hizo imepanda kufikia hadi Sh1,000 kwa kuoga na Sh300 kwa haja ndogo na kubwa.

Hata hivyo, wakati baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wakizidi kuugulia uhaba wa maji, hali hiyo imegeuka dhahabu kwa wamiliki wa magari yanayofanya biashara ya kuuza maji maeneo tofauti.

“Maji yamegeuka dhahabu, bei ni makubaliano na mteja na hapo tunazingatia umbali anakohitaji mteja kupelekewa huduma ya maji, tunaanzia Sh20,000 kwa uniti moja ambayo ni lita 1,000,” alisema Joseph Saimon.

Hilo lilielezwa pia na Juma Mohammed, dereva wa gari, akisema kuchangamka kwa bei hiyo kunachangiwa na sehemu nyingi zinazotoa huduma kwa umma kuhitaji maji, huku akitolea mfano anajipatia oda ya kupeleka maji Masaki na Mbezi Beach.

“Wateja wetu wengi tunaowauzia maji ni wale wenye shule, hospitali, gesti, lodge, viongozi na wanaofanya shughuli za ujenzi na unakuta wanaagiza maji kuanzia uniti nne na kuendelea. Awali, uniti moja ilikuwa Sh13,000 hadi Sh15,000, sasa hivi bei ni maelewano,” alisema Mohammed.

Fursa kwa bodaboda

Wakati watu wakitaabika na mgawo wa maji, waendesha bodaboda maeneo ya Mbezi Salasala wamegeuza fursa kwao, na kuona kubeba abiria sio ishu ukilinganisha na maji.

Dereva wa bodaboda Marco Kamage alisema maeneo hayo dumu moja la maji linauzwa Sh1,000 na ana uwezo wa kubeba madumu sita kwa safari moja hivyo kupata Sh6,000.

Kamage alisema hii ni tofauti na kusubiria abiria kijiweni kwa kuwa, unaweza kukaa saa tatu hujampata na ukimpata ni wa safari fupi ambaye anakupa Sh1,000.

Kutokana na hali hiyo, alisema anajikuta anaondoka na Sh15,000 hadi Sh20,000 kwa siku ambayo ni tofauti na biashara ya maji ambayo kwa siku mtu anaweza kupata hadi Sh70,000.

Mwendesha bodaboda mwingine, David Martin alisema hali hiyo imesaidia kujiongezea kipato, licha ya wao kutoa msaada wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi, huku akikiri kuwa kuna wakati wateja wanawazidi.

Ukiacha wanaowauzia kwenye ndoo, Martin alisema wapo wengine wanataka wajaziwe kwenye mapipa yao ya kuhifadhi maji na kwa lita 5,000 hakosi Sh60,000.

“Hii hali inatufanya tuanze kukufuru na kutamani mgawo uendelee tu, japo sio neno zuri kulisema lakini ndio hivyo,” alisema bodaboda huyo.


Maeneo mengine hali ni shwari

Mwananchi ilitembelea eneo la Kurasini na Mivinjeni lililounganishwa na mradi wa maji kutoka Kigamboni, baadhi ya wakazi walieleza kuwa huduma ya maji inapatikana na hayajakatika tangu yalivyoanza kutoka wiki iliyopita.

Suzan Maganga alisema tofauti na ilivyo kwenye maeneo mengine yenye adha kubwa ya maji, Kurasini maji yanapatikana.

Mtendaji wa Mtaa wa Mivinjeni, Shamsa Mohamed alisema katika eneo hilo hakuna changamoto ya maji tangu yalipoanza kutoka hawajapata taarifa za mgawo.

Hata Mwananchi ilipomtafuta Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za Mtaa jijini Dar es Salaam, Juma Mwingamno ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtaa eneo la Feri alisema mradi wa visima vya maji Kigamboni umesaidia kuondoa changamoto ya maji katika eneo hilo.

Eneo lingine lililonufaika na maji ni wilayani Ilala ambako huduma hiyo ilianza kupatikana jana jioni, baada ya kuikosa kwa zaidi ya wiki tatu.

“Tunamshukuru Mungu baada ya mateso ya kukosa maji kwa zaidi ya wiki tatu, leo saa kumi na moja bomba langu limetoa maji,” Zuwena Hassan, mkazi Mtaa wa Sharifu Shamba aliliambia gazeti hili.

Imeandikwa na Mariam Mbwana, Nasra Abdallah, Elizabeth Edward na Tuzo Mapunda