Makamu wa Rais Dk Mpango kuzindua kampeni ya mazingira

Makamu wa Rais Dk Mpango kuzindua kampeni ya mazingira

Muktasari:

  • Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) yaanda kampeni kubwa ya mazingira itakayozinduliwa na Makamu wa Rais Dk, Philip Mpango.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amesema wameandaa kampeni kubwa ya mazingira itakayohusu utunzaji wa mazingira kwa ujumla, itakayozinduliwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango.


Amesema kampeni itakwenda sambamba na mashindando katika ngazi mbalimbali ikihusisha upandaji miti, utunzaji na usafi wa mazingira.


Jafo ameeleza hayo  leo Jumatatu Aprili 12,2012 Jijini Dodoma, wakati wa kikao kazi na menejimenti ya ofisi ya makamu wa Rais na wanahabari kilichofanyika katika Mji wa Serikali Mtumba.Amesema lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kielelezo cha utunzaji wa mazingira.


Amefafanua kampeni hiyo itahusisha mikoa yote 26,  zawadi na tuzo zitatolewa kwa washindi katika ngazi mbalimbali mara baada ya tathmini kufanyika,  zitakazotolewa siku ya mazingira duniani inayofanyika kila Juni 5 kila mwaka.


“Kampeni hii pia itashindanisha majiji, manispaa, halmashauri za miji na majiji, kata na vijiji. Kwenye sekta za elimu na afya, vyuo, shule za sekondari na msingi hospitali, zahanati na vituo vya afya vitashindanishwa.


“Tunafahamu changamoto kubwa za usafiri katika shule yetu na taasisi za elimu ya juu, zawadi kama magari, pikipiki, vifaa vya kufundishia na kompyuta zitatolewa.Pia tutatoa zawadi ya vifaa  tiba katika sekta ya afya ikiwemo vitanda katika hospitali zitakazoibuka vinara zitatolewa,”  amesema Jafo.


Jafo amesema makundi mengine yatakayoshindanishwa ni pamoja wanahabari sekta za viwanda hifadhi ya taifa madampo, viwanja vya ndege,  na stendi za mabasi .


Kwa mujibu wa Jafo, kampeni hiyo itakuwa na washindi 152 kutoka makundi mbalimbali watakaopatikana na kukabidhiwa zawadi na fursa za kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo mbuga za wanyama.