Makinda awataka vijana kujitafutia ajira wenyewe

Muktasari:

Makinda amesema kuwa takwimu walizochukua zinakwenda kutumika kubadili Mfumo wa maisha ya wananchi wa Tanzania ikiwemo kutoa fursa mbali mbali mbali Kama zinavyotolewa kwenye sekta ya kilimo ikiwemo ruzuku za mbolea ili kusaidia wasio na ajira kuzitumia kujipatia ajira na kukuza uchumi.

Arusha. Kamisaa wa Sensa Kitaifa, Anna Makinda amewataka vijana wasomi kujitengenezea uchumi wao binafsi kupitia fursa zilizoko kwenye maeneo wanayoishi kuliko kutegemea ajira kutoka serikalini au sekta binafsi.

Akizungumza leo Oktoba 12 na Kamati ya sensa katika kikao cha kutathimini sensa kwa Mkoa wa Arusha, Makinda ambaye pia ni Spika mstaafu, amesema kuwa takwimu hizo ni muhimu kwa nchi kwenda kutengeneza mfumo mzima katika hatua zake za kusaidia jamii hasa kiuchumi.

“Lipo jambo kubwa nililoliona nalo ni kundi kubwa la vijana ambao hawana ajira wala hawajishughulishi na kazi yoyote ya kujiingizia kipato na ukimuuliza anasema amehitimu elimu fulani anasubiri ajira, jamani hili la kuajiriwa mtachelewa sana,” amesema Makinda

Amesema kuwa tatizo la ajira linalotupiwa serikali linaweza kutatulika na muhusika mwenyewe kwa kutazama changamoto zilizoko hata katika jamii na kuliwekea ubunifu mzuri na kuwa fursa ya ajira au kujipatia kipato kuliko kusubiri kuajiriwa.

“Mfano mzuri serikali kwa sasa inetengeneza fursa nzuri kwenye sekta ya kilimo na uzuri nchi yetu ina maeneo mengi wazi, lakini utakuta kijana msomi anasema anasubiri kuajiriwa badala atumie fursa kutengeneza ajira, nawaambia hao sio wasomi wazuri ambao Taifa linaweza kuwategemea,” amesema.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongela amesema kuwa jumla ya kaya 2,724 zilihesabiwa katika vitongoji 1,506 na kazi ilifanikiwa kwa asilimia 99.99.

“Kwenye kazi hii serikali ilitupatia kiasi cha Sh5.9 bilioni na tumefanikisha kazi hiyo na vifaa vyote tulivyokabidhiwa tumerudisha kasoro vishwambi vitano ambavyo vilipotea, lakini jeshi la polisi vinaendelea na kazi ya kuvipeleleza vipatikane,” amesema.