Malasusa aitaka CCM kusimamia misingi yake

Muktasari:

  • Katibu wa  Chama cha Mapinduzi Itikadi, Uenezi , Paul Makonda amemtembelea Askofu Mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa kwa lengo la kujitambulisha na kupokea nasaha

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani (DMP), Alex Malasusa ametoa wito kwa Chama cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kusimamia misingi yake, ikiwemo kuhakikisha Watanzania wote wanatendewa haki na kuwa sikio lao la wananchi wanyonge.

Askofu Malasusa ambaye katika mkutano mkuu wa 21 wa kanisa hilo, Agosti 25, 2023; alichaguliwa kuwa Mkuu wa KKKT, ametoa kauli hiyo leo Desemba 2, 2023 alipotembelewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi , Paul Makonda.

Makonda amemtembela Askofu huyo kwa lengo la kumsalimia na kumpongeza kwa kuchaguliwa kwake kuliongoza kanisa hilo, kwa mara nyingine kwani aliwahi kuwa Mkuu wa kanisa hilo kuanzia 2007-2015 kabla ya kumpisha Askofu Fredrick Shoo.

Katika nasaha zake, Askofu Malasusa amesema viongozi wa dini na kiroho wataendelea kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwa na busara na hekima anapoendelea kuliongoza taifa, kama ambavyo tayari ameonesha uimara, tangu alipobeba dhamana na Mamlaka ya Kiongozi Mkuu wa Nchi.

“Hivyo nitoe wito kwa Chama cha Mapinduzi, kuendelea kusimamia misingi yake, ikiwemo kuhakikisha Watanzania wote wanatendewa haki, kuwa sikio lao la wananchi wanyonge na kuwasemea changamoto zao mbalimbali kila inapojitokeza, ili zifanyiwe kazi na kubadili hali zao,” amesema Malasusa.

Kwa upande wake, Makonda amemshukuru Mkuu huyo Mteule wa KKKT kwa ushirikiano, utayari wake yeye na viongozi wenzake katika kanisa, kuendelea kuliombea taifa na Watanzania wote kuendelea kudumisha upendo, amani, utulivu na mshikamano bila kujali tofauti za kiitikadi.

“Nitumie nafasi hii pia kukupongeza kwa kuchaguliwa tena kuwa Mkuu wa KKKT, hivyo nakutakia kila la heri katika majukumu yako na ninakuahidi ushirikiano wa Chama Cha Mapinduzi, ambacho nimepewa wajibu wa kuwa msemaji wake,” amesema Makonda.

Ziara hii ya leo aliyoifanya Makonda, ni mwendelezo wa ziara zake za kuwatembelea viongozi mbalimbali wa kiroho, pamoja na wale wa kijamii, kwa ajili ya kuwasalimia, kujitambulisha na kuwaomba ushirikiano wa kikazi.