Mali za mtoto wa rais zauzwa kununua chanjo

Muktasari:

  • Wizara ya Sheria, Marekani (DOJ), imetangaza kuwa fedha ambazo zimepatikana kwa kupiga mnada mali za Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Nguema Obiang Mangue, zitatumika kununua chanjo na kuisaidia nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Wizara ya Sheria, Marekani (DOJ), imetangaza kuwa fedha ambazo zimepatikana kwa kupiga mnada mali za Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Nguema Obiang Mangue, zitatumika kununua chanjo na kuisaidia nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Obiang ni mtoto wa Rais wa Equatorial Guinea Teodoro Obiang Nguema Mbasongo. Wizara ya Sheria Marekani, inaamini kuwa mali hizo za Obiang ambazo zimepigwa mnada, zilipatikana kwa njia ya rushwa.

Kwa mujibu wa DOJ, fedha zilizopatikana kwa kuuza mali za Obiang ni dola 25.6 milioni (Sh59 bilioni). Wakaeleza kuwa dola 19.25 milioni (Sh44.4 bilioni), zitapelekwa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kununua chanjo za Uviko-19. Vilevile, watatumia dola 6.35 milioni (Sh14.4 bilioni), kununua dawa na vifaa tiba, kisha kupeleka Equatorial Guinea.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa DOJ imebainisha kuwa mwaka 2011, Obiang, akiwa Waziri wa Kilimo, alichota zaidi ya dola 300 milioni (Sh692 bilioni).

Kulingana na makubaliano ya mwaka 2014, Obiang, alitakiwa kuuza jumba lake la kifahari lililopo Malibu, California, kwa dola 30 milioni, sawa na Sh69.2 bilioni.

Kibano kila upande

Hali ikiwa hivyo Marekani, kwa United Kingdom (UK), Julai mwaka huu, Serikali ilimwekea vikwazo. Sababu ni kiongozi huyo kujihusisha na ufisadi. Kwa uamuzi huo, Obiang hatakanyaga Uingereza, Scotland na Ireland Kaskazini.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Dominic Raab, alisema Obiang, amekuwa akitumia vibaya fedha za wananchi wa Equatorial Guinea, ikiwemo kununua majumba ya kifahari, ndege binafsi ya kutembelea, vilevile alitumia dola 275,000 (Sh637 milioni) kununua glavu alizovaa Michael Jackson kwenye ziara ya Bad.

Raab alisema kuwa Obiang alinunua jumba lenye thamani ya dola 100 milioni (Sh232 bilioni), Paris, Ufaransa, amenunua ndege binafsi (private jet) kwa dola 38 milioni (Sh88 bilioni), ana boti la kifahari ambalo hutumia kula raha baharini. Ana idadi kubwa ya magari daraja la kwanza duniani, kama Ferrari, Bentley, Aston Martin na kadhalika.

Uamuzi wa kumpiga marufuku Obiang, unaenda sambamba na kutaifisha mali zake. Tamko la UK ni kuwa mali zote za Mangue zilizopo kwenye nchi hiyo, zimechukuliwa na Serikali.

Huyu ndiye Obiang

Baba yake Obiang, Mbasongo, ambaye yupo madarakani tangu mwaka 1979. Miaka 42 imekatika. Aliingia madarakani baada ya kumpindua na kumuua mjomba wake, Francisco Macías Nguema.

Mwaka 1968, Macías Nguema, aliipatia uhuru nchi yake kutoka kwa Hispania. Baada ya uhuru, Macías Nguema akaifanya Serikali ya Equatorial Guinea kuwa mali ya familia yake. Wizarani na Jeshini akajaza wanafamilia. Baadaye wanafamilia wakageukana. Mbasogo akampindua na kumuua mjomba wake, Macías Nguema.

Zikafuata zama nyingine za familia kujitanua madarakani. Nchi maskini yenye utajiri wa mafuta, familia moja inafilisi mkate wote. Wananchi wanaishi katikati ya umaskini mkubwa. Nani anajali?

Sasa, katika mgawo wa vyeo kwa familia, ndipo unampata Obiang (Teodoro Nguema Obiang Mangue). Ni mtoto wa damu wa Rais Teodoro Obiang.

Maisha ya Mangue ni tamthiliya iliyokithiri ufahari. Wananchi wa Guinea wanapigika, yeye anavyoishi unaweza kudhani ni maisha ya kufikirika, mithili ya James Bond katika maandishi ya galacha wa Uingereza, Ian Fleming.

Oktoba 19, 2020, BBC waloripoti kuwa Obiang yupo likizo Maldova, akila raha za daraja la kwanza duniani. Kwa siku alilipa hoteli dola 50,000 (Sh116 milioni) huku Equatorial Guineayenye watu takriban milioni 1.5, wengi wao kwa siku ama walishinda njaa au walilala bila kuweka kitu tumboni.

Mwaka 2017, Mahakama Ufaransa ilimhukumu Obiang kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kumkuta na hatia ya kupora mali za Equatorial Guinea na kuwekeza Ufaransa.

Mahakama ilitaifisha majumba na magari ya kifahari ya Mangue. Mali zote zilizotaifishwa zilikuwa dola 178 milioni. (Sh413 bilioni.


Mwaka 2014, Voice Of America (VOA), waliripoti kuwa Serikali ya Marekani ilitaifisha mali za Obiang zenye thamani ya dola milioni 38 (Sh88.2 bilioni). Mali hizo ni pamoja na jumba la kifahari alilonunua ufukweni, jijini Malibu, California, vilevile baadhi ya vitu vya Michael Jackson, ikiwemo glovu, ambazo alinunua kwenye mnada.

Uamuzi wa kumnyang’anya mali hizo Obiang, ulifuata baada ya kumbaini kwamba mwaka 2011, aliingia Marekani na dola 80 milioni (Sh185.6 bilioni), alizozipata kwa njia zisizo halali, kisha kuzitumia kuwekeza nchini humo.

Mwaka 2018, mali za Obiang, zenye thamani ya dola 16 milioni (Sh37.2 bilioni), zilitaifishwa Brazil. Polisi nchini humo walimbaini Mamgue na watu wake ambao hawakuwa na utambulisho wa kidiplomasia, kuingia Brazil na fedha taslimu dola 1.5 milioni (Sh3.5 bilioni), vilevile saa za kifahari zenye thamani ya dola 15 milioni, sawa na Sh34. 8 bilioni. Kwa sheria ya Brazil, fedha taslimu ambazo mtu anaruhusiwa kuingia nazo ni dola 2,400, yaani Sh5.6 milioni.

Mwaka 2017, Serikali ya Uswisi ilitaifisha magari ya kifahari na boti yenye anasa nyingi . Mali zote hizo ni za Obiang. Thamani ya mali zilizotaifishwa ni dola milioni 100. Fedha hizo ni sawa kabisa na Sh232 bilioni.

Pamoja na mali nyingi kutaifishwa, lakini Obiang bado hatetereki. Anaendelea kutumbua. Mwaka 2018, alipost picha Instagram akiwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akasema ndio watu wenye nguvu kubwa ulimwenguni. Ni yeye na Putin.

Alipo, Obiang, anasubiri baada ya baba yake, Teodoro Mbasongo, yeye aapishwe kuwa Rais wa Equatorial Guinea. Rais Mbasongo yupo kimya. Matendo ya mtoto wake, haoni kama yanamharibia katika uongozi wake. Zaidi, inaonekana yeye anaridhika kwa kila kitu kinachofanywa na mtoto wake kipenzi, ndio maana mpaka amempa cheo kikubwa. Amemkaribisha jirani na uraus.