Malkia Elizabeth II: Binadamu aliyekuwa na mamlaka makubwa duniani

Malkia Elizabeth II
What you need to know:
- Juzi mchana, upepo ulibadilika baada ya taarifa kutoka ndani ya kasri la Kifalme la Uingereza, Buckingham Palace, kutoa habari kuwa hali ya Malkia Elizabeth II haikuwa njema na aliwekwa kwenye uangalizi maalum.
Juzi mchana, upepo ulibadilika baada ya taarifa kutoka ndani ya kasri la Kifalme la Uingereza, Buckingham Palace, kutoa habari kuwa hali ya Malkia Elizabeth II haikuwa njema na aliwekwa kwenye uangalizi maalum.
Taarifa hiyo ilieleza Malkia Elizabeth II, alikuwa amepumzishwa kwa ajili ya kutazamwa kwa ukaribu na madaktari, kwenye kasri la Balmoral Castle, Aberdeenshire huko Scotland.
Balmoral Castle ni jumba la mtoto wa kwanza wa Malkia Elizabeth II, Mfalme Charles, ambaye anangoja utawazo rasmi ili avae taji la Ufalme wa Uingereza na baadhi ya nchi za Jumuiya ya Madola kuanzia juzi jioni, baada ya kifo cha mama yake.
Mshangao ulikuwa baada ya taarifa hiyo, wanafamilia wa Malkia Elizabeth II, walifunga safari kutoka sehemu mbalimbali duniani kwenda Balmoral Castle.
Watoto wote wanne wa Malkia Elizabeth; Charles, Anne, Andrew na Edward, vilevile mtoto wa kwanza wa Charles, William ambaye ni hivi sasa ndiye mrithi namba moja wa taji la Mfalme.
Wajukuu wengine wa Malkia Elizabeth II, akiwemo Harry na mkewe Meghan, ambao waliamua kusasa maisha ya kifalme na kwenda kuishi Marekani kwa madai ya ubaguzi, waliahirisha ghafla ushiriki wao kwenye Tuzo za Wellchild, zilizopaswa kufanyika London, juzi usiku.
Harry alisafiri kwenda Scotland na kuungana na wanafamilia kwenye kasri la Balmoral Castle. Meghan alibaki London, ingawa ilielezwa ataungana na mumewe msibani siku chache zijazo.
Wito wa haraka kwa kila mwanafamilia ya kifalme, vilevile taarifa ya afya ya Malkia Elizabeth II kuwekwa hadharani, ilianza kujenga picha ya huzuni duniani. Wengi kuanza kusubiri tangazo la kifo.
Mamia ya watu walikusanyika nje ya kasri la Balmoral Castle kuonesha kuguswa na afya ya Malki Elizabeth II. Wapo walioshindwa kujizuia na kumwaga machozi. Hisia ziliwajuza kuwa huenda Malkia tayari amekwenda.
Mshangao ulikuwa mkubwa pia kutokana na ukweli kuwa siku mbili kabla, yaani Septemba 6, mwaka huu alimteua Liz Truss kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza.
Siku hiyo, Malkia alikuwa mwenye tabasamu pana. Kitendo cha afya kuonekana kubadilika ghafla, kulijenga pia hofu kwamba pengine Malkia alidondoka.
Kumbe, ilimpendeza Mungu kazi ya mwisho ya Malkia Elizabeth II, iwe kumteua Liz Truss na kumbariki kwenda kuunda Serikali mpya, kwani jioni ya juzi, tangazo lilitolewa mwanamke huyo aliyekuwa na nguvu kuliko wote duniani, tayari alishaitikia wito wa mauti.
Naam, ni ahadi iliyopo kwenye kila kitabu kitakatifu kuwa mwisho wa binadamu ni kifo. Ni watu imani ya Rastafarians ndio hawaamini katika kufa kupitia nadharia yao ya Livity, kwamba wao huishi milele. Unaondoka duniani unakwenda bustanini Eden kuendelea na maisha.
Amemfuata Philip wake
Mwaka 1939, Elizabeth II alikuwa binti mwenye umri wa miaka 13. Urembo wake haukuwa na kificho. Mwaka huo, Philip alikuwa kijana barubaru, umri wake tayari ulishatimia miaka 18. Ndipo wakakutana. Binti wa miaka 13 akaangukia kwenye penzi la kijana mwenye miaka 18.
Elizabeth na Philip wakawa wanaandikiana barua za urafiki. Kutoka urafiki, ukawadia uchumba kisha ndoa na baadaye familia.
Ilipofika Aprili 9, 2021, Philip akaitikia wito wa Mungu. Ukihesabu kutoka mwaka 1939 mpaka 2021 ni miaka 82 iliyotimia. Elizabeth aliachwa peke yake na rafiki waliyedumu kwa upendo na uaminifu mkubwa kwa miaka 82.
Baada ya kifo cha Philip? Malkia Elizabeth II alisema alijihisi mpweke mno kuliko wakati wowote ule kwenye maisha yake. Mwaka mmoja na takriban miezi mitano baada ya kifo cha Philip, Malkia Elizabeth amemfuata.
Philip na Elizabeth, mapenzi yao hayakuwa na kishawishi chochote kile cha pembeni. Walipendana wakiwa wadogo, mioyo yao ikiwa bado salama kabisa dhidi ya visa vya dunia. Walipofunga ndoa, wakaishi pamoja kwa takriban miongo nane.
Malkia Elizabeth alikuwa mwanamke mwenye nguvu kuliko binadamu yeyote chini ya jua. Alikuwa Malkia wa United Kingdom (UK) au kwa jina lingine Great Britain, dola inayounganisha visiwa vya Uingereza (England), Scotland na Northern Ireland. Moja ya dola imara ambazo zimekuwa zikitafsiriwa kama viranja wa dunia.
Malkia Elizabeth II, mbali na UK, alikuwa Malkia wa Canada, New Zealand, Australia, Jamaica, Barbados, The Bahamas, Grenada, Papua New Guinea, Visiwa vya Solomon, Tuvalu, St Lucia, St Vincent na Grenadines, Belize, Antigua na Barbuda, St Kitts na Nevis.
Malkia Elizabeth II, alishakuwa Malkia wa Tanganyika (Tanzania Bara) kabla haijajitangaza kuwa Jamhuri Desemba 9, 1961, vilevile Pakistan, Afrika Kusini, Ghana, Nigeria, Kenya, Malawi, Gambia, Trinidad na Tobago, Ceylon, Sierra Leone, Uganda, Mauritius, Malta, Guyana na Fiji.
Chimbuko lake sasa
Aliyekuwa Mfalme wa UK, George VI, alimuoa Elizabeth. Katika ndoa yao, wakapata watoto wawili, wote mabinti ambao ni Elizabeth (mkubwa) na mdogo wake, Margaret. Huyo Elizabeth (mtoto mkubwa), ndiye Malkia Elizabeth II.
Hivyo, Malkia Elizabeth, mama yake naye anaitwa Elizabeth. Kuna Elizabeth Malkia na Elizabeth mama wa Malkia (Queen Mother) ambaye alikuwa mwenzi wa Mfalme (Queen Consort).
Mwaka 1939, Mfalme George VI, akiongozana na mkewe, Elizabeth, vilevile mabinti zake, Elizabeth na Margaret, walitembelea chuo cha kifalme cha mafunzo ya jeshi la majini, Royal Naval College, kilichopo Dartmouth, Devon, England.
Louis Mountbatten ni mjomba wake Philip. Aliuawa mwaka 1979. Mwaka 1939, Mountbatten alikuwa ofisa mkuu wa Chuo cha Royal Navy. Kipindi hicho, Philip pia alikuwa akipokea mafunzo ya kijeshi Royal Navy College.
Sasa, Mfalme George VI na mkewe, Elizabeth, wakawa wanazungumza na Mountbatten. Kuacha mazungumzo ya watu wazima yaendelee, Elizabeth (Queen Mother), akamuomba Philip awazungushe kwenye maeneo ya chuo mabinti zake, Elizabeth (Malkia Elizabeth) na Margaret.
Huo ukawa mwanzo wa Elizabeth (Malkia Elizabeth) kufahamiana na kijana mzuri, aliyemvutia, Philip. Mwaka 1946, Philip akagonga hodi kwenye kasri la Mfalme wa Uingereza kuomba mkono wa ndoa kwa binti yake wa kwanza, Elizabeth II.
Mwaka huo, 1946, Elizabeth alikuwa na umri wa miaka 20. Mfalme George VI alikubali posa ya Philip, lakini sharti likawa kusubiri Elizabeth II afikishe umri wa miaka 21 ndipo aolewe. Ndio maana, mwaka 1947, Elizabeth alipokuwa na umri wa miaka 21, akafunga ndoa na Philip. Baada ya miaka sita ya ndoa, Elizabeth II alitawazwa kuwa Malkia wa UK, kufuatia kifo cha baba yake, Mfalme George VI. Aprili 21, mwaka huu, Malkia Elizabeth II alitimiza umri wa miaka 96 ya kuzaliwa. Kimahesabu, Malkia Elizabeth II alikuwa mtawala kwa miaka 69. Juni 2, 1953, Elizabeth II alitawazwa rasmi kuwa Malkia wa UK na dola nyingine nyingi zilizokuwa chini ya taifa hilo. Mamlaka yote hayo sasa yanakwenda kwa mwanaye Charles.
Malkia Elizabeth II ni kama alikuwa ameshajiandaa kumpisha Charles, kwani alikuwa akimtuma majukumu mengi ambayo angepaswa kuyashughulikia yeye kama Malkia.
Mei mwaka huu, Charles alizindua Bunge la UK kwa mara ya kwanza. Pia alimwakilisha mama yake kwenye ibada ya Alhamisi Kuu mwaka huu. Novemba 11, 2021, Charles aliongoza maadhimisho ya Jumapili ya Kumbukumbu kwa niaba ya mama yake, pia Siku ya Utumishi wa Jumuiya ya Madola.
Baada ya kifo cha Mfalme George VI, ilimchukua Elizabeth II miezi minne kasoro siku nne kutawazwa kuwa Malkia. Haijatajwa ni lini Charles atatawazwa.
Kwa kawaida, cheo cha Mfalme wa UK huendana na uchaguzi wa jina. Elizabeth II alitaka kutumia jina lake halisi, inadhaniwa kuwa hata Charles ataitwa hivyohivyo, ingawa atatambulishwa kama Mfalme Charles III.