Malkia Elizabeth II kuzikwa Septemba 19, wananchi kumuaga

Muktasari:

  • Mazishi ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza, yatafanyika Jumatatu ya Septemba 19, 2022 katika eneo la Westminster Abbey huko London.

Balmoral. Mazishi ya Malkia Elizabeth II wa Uingereza, yatafanyika Jumatatu ya Septemba 19, 2022 katika eneo la Westminster Abbey huko London.

Mwili wa Malkia utalala siku nne katika Ukumbi wa Westminster kuanzia Jumatano Septemba 14, ofisa mwandamizi katika Jumba la Kifalme amesema.

Jeneza la Malkia ambalo limehifadhiwa katika Kasri la Balmoral, litachukuliwa hadi Kasri la Holyroodhouse huko Edinburgh Jumapili Septemba 11, safari ya saa sita kwa gari.

Wafanyakazi wa Balmoral watatoa heshima zao za mwisho kwa Malkia kabla ya kusafirishwa kwenda Edinburgh kesho, imebainishwa kuwa atasafirishwa kupitia Aberdeen katika safari hiyo ya saa nne.

Mfalme Charles III ataliongoza taifa katika maombolezo siku ya Jumatatu ambapo atatembea mbele ya msafara wa jeneza la Malkia katika mitaa ya Edinburgh.

Atakuwa mbele ya familia ya kifalme kwenda kwenye Kasri la Holyroodhouse huko Edinburgh na kupanda hadi Kanisa kuu la Mtakatifu Giles, imetangazwa.

Mfalme na mwenza wake watasafiri kwa ndege hadi Edinburgh na Prince William na washiriki wengine wa Familia ya Kifalme ili kuongoza maandamano.

Kisha atalazwa kwa muda wa saa 24 kabla ya kusafirishwa, kwa ndege, hadi London siku ya Jumanne.

Wananchi watamwona Malkia akiwa amelala katika Kasri la Holyrood na baadaye London katika Ukumbi wa Westminster.

Inaelezwa mwili wa Malkia utaondoka Balmoral kesho Jumapili, Septemba 11, 2022 saa 4 asubuhi kwa gari kupitia Aberdeen, Dundee, Perth, huku maelfu ya watu wakitarajiwa kujaribu kuona na kuligusa gari litakalobeba mwili huo.