VIDEO: Mama, watoto wanne wafariki wakidaiwa  kukanyagwa Uwanja wa Uhuru

Mama, watoto wanne wafariki wakidaiwa  kukanyagwa Uwanja wa Uhuru

Muktasari:

  • uzuni na majonzi vimetawala nyumbani kwa familia ya Daudi Mtuwa iliyopoteza  watu watano wanaodaiwa kufikwa na umauti katika shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli jana Jumapili Machi 21, 2021 katika Uwanja wa Uhuru.

Dar es Salaam. Huzuni na majonzi vimetawala nyumbani kwa familia ya Daudi Mtuwa iliyopoteza  watu watano wanaodaiwa kufikwa na umauti katika shughuli ya kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli jana Jumapili Machi 21, 2021 katika Uwanja wa Uhuru.

Waliofariki dunia ni Susan Mtuwa na watoto wake wawili, Nathan (6) na Natalia (5) pamoja na watoto wengine wawili Cris (11) na Michelle (8) ambao ni watoto wa shemeji zake Susan huku dada wa kazi wa familia hiyo aliyekwenda pamoja nao uwanjani hapo.

Wakati hayo yakielezwa jana Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliieleza Mwananchi Digital kuwa katika shughuli hiyo baadhi ya watu walijeruhiwa lakini hakuna na idadi kamili na hata leo Jumatatu Machi 22, 2021 alipotafutwa kuhusu suala hilo simu yake iliita bila majibu.

Ndugu watano wafariki wakimuaga Magufuli | Wazazi wasimulia tukio zima

Leo mchana ofisi ya habari na uhusiano katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imetoa taarifa ya kupokea majeruhi saba na maiti moja. Kati ya majeruhi hao mmoja aliruhusiwa kurejea nyumbani.

Kuhusu vifo hivyo, kaka mkubwa wa familia hiyo, Gerald Mtuwa ameiambia Mwananchi Digital kuwa Suzan aliondoka na watoto hao saa 11 alfajiri pamoja na dada wa kazi ambaye hadi sasa hajulikani alipo.

“Jioni tulipigiwa simu na mtu ambaye hatukumfahamu akitueleza kuwa mwenye simu (marehemu) ameanguka, alisema walihisi kuna tatizo limejitokeza kwa ndugu zao baada ya ukimya wa muda mrefu tangu walipowasiliana nao saa sita mchana.”


“Tulifunga safari hadi uwanja wa Uhuru na kukuta gari ya Suzan imeegeshwa katika mazingira mazuri na asilimia kubwa ya watu walishatawanyika. Hii ilikuwa dalili tosha ile simu tuliyopigiwa hatukudanganywa. Tuliitumia gari Suzan kufanya harakati za kuwatafuta,” amesema.

Amebainisha kuwa walikwenda hospitali ya Temeke tuliwatafuta kwenye wodi hatukufanikiwa, kushauriwa kwendakatika chumba cha kuhifadhia maiti na kukuta miili ya ndugu zao.

“Hapa tunaishi kama familia Suzan ni shemeji yangu, tunaishi kama jiji hapa, hawa watoto wengi ni wa shemeji zake. Kwa sasa tunajipanga na vikao ili tujue namna ya kuwahifadhi wapendwa wetu,” amesema.