Mambo yanayomleta Makamu wa Rais Marekani nchini

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax ametaja sababu tatu za ujio wa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris nchini Tanzania ikiwemo ushirikiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani ulioasisiwa mwaka 1961.

Dk Tax amebainisha hayo leo Machi 27, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu ziara ya kihistoria ya kiongozi huyo wa juu wa Marekani.

Harris anatarajia kuwasili Tanzania Machi 29, 2023 kwa ziara ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine, mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya mataifa haya mawili itasainiwa.

Amesema sababu ya kwanza ya kiongozi huyo kuja nchini ni kufuatia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan alioutoa Aprili 2022 alipokwenda Marekani kwa ajili ya uzinduzi wa filamu ya "Tanzania: The Royal Tour."

Sababu nyingine amesema ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa Marekani, Joe Biden aliyoitoa Desemba 2022 wakati wa mkutano kati ya Afrika na Marekani, kwamba viongozi wa juu wa Marekani watatembelea nchi za Afrika ili kuimarisha ushirikiano.

Waziri Tax amebainisha sababu nyingine kuwa ni ushirikiano imara kati ya Tanzania na Marekani ambao umezidi kuimarika siku hadi siku kupitia miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taifa hilo lenye nguvu kiuchumi duniani.

"Ushirikiano wetu na Marekani ulianza mwaka 1961, mwaka 1968 tulitiliana saini mikataba kadhaa ya ushirikiano na hadi sasa uhusiano huu unazidi kuimarika zaidi," amesema Dk Tax.

Amesema Marekani ni miongoni mwa mataifa yanayofanya vizuri kwenye uwekezaji hapa nchini ambapo hadi sasa miradi 266 ya Marekani imesajiliwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na thamani ya Dola 4.778 bilioni.

Waziri huyo amesema kupitia miradi hiyo, Marekani imetoa ajira 54,584 kwa Watanzania. Pia, amesema kuna ongezeko kubwa la idadi ya watalii kutoka Marekani ambao wameongezeka kutoka 66,394 mwaka 2015 hadi watalii 100,600 mwaka 2022.

"Kupitia ziara hii, Tanzania na Marekani zitaendelea kudumisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ya biashara, utalii, elimu, afya, kilimo, mazingira na Tehama," amesema Waziri Tax.

Harris atawasili nchini Machi 29, 2023 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na atapokelewa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango.

Atakutana na Rais Samia Machi 30, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo wawili hao wakiwa na historia kwenye mataifa yao kuwa viongozi wanawake wa kwanza, watakuwa na mazungumzo na pia jioni atashiriki futari aliyoandaliwa na mwenyeji wake.