Mamia wamuaga aliyefariki ajali ya ndege

Muktasari:

Aneth Kaaya mmoja watu 19 waliofariki katika ajali ya ndege ya shirika la Precision Air iliyotokea Novemba 6 Bukoba mkoani Kagera, amezikwa wilayani Arumeru mkoani Arusha na mamia ya waombolezaji.

Arusha. Mamia ya watu wilayani Arumeru wamejitokeza katika ibada ya kumuuaga marehemu Aneth Kaaya aliyefariki katika ajali ya ndege ya shirika la Precision Air iliyotokea Novemba 6 Bukoba mkoani Kagera.

Aneth ni miongoni mwa watu 19 waliofariki katika ajali hiyo, huku watu wengine 24 wakiokolewa baada ya ndege hiyo 5H-PWF, ATR-500 kushindwa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Bukoba na kutumbukia ndani ya ziwa Victoria.

Akizungumza katika mazishi hayo yaliyofanyika katika usharika wa Nkoanrua wilayani Arumeru, mama mzazi wa marehemu, Levina Aloyce amesema kuwa, amepokea msiba wa mtoto wake kwa uchungu mkubwa

 "Sina budi kukubali matokeo, kwani Mungu ndo kanipa na ameamua kumchukua na sina cha kuongea, isipokuwa kumshukuru yeye peke yake," amesema.

Amesema kuwa, katika familia yake alifanikiwa kupata watoto wanne watatu wa kike na mmoja wa kiume, hivyo kwa sasa hivi wamebakia watatu.

Akihubiri katika ibada hiyo, Mkuu wa jimbo la Magharibi dayosisi ya Meru, Mchungaji Annael Nassari amesema kuwa, watu wote wapo safarini wanapita, hivyo kila mtu anawajibika kutenda mema.

“Haya yametokea tuyapokee hata kama ni machungu, tujiandae muda wowote tunaondoka. Kesho na baadaye yetu anaijua Mungu, hivyo tujikabithi mikononi mwa Mungu na tutafakari juu ya mauti na kila mmoja awe mtu wa kuomba,” amesema.

Aidha aliwataka ndugu wanaogombana wapatane na ndugu zao mapema, kwani siku ya mwisho kila mmoja atatoa habari zake mwenyewe. 

Wasifu wa marehemu

Akisoma wasifu wa marehemu, Lilian Kaaya, amesema Aneth Lewis Kaaya alizaliwa Januari 1, 1994 na kusoma shule ya msingi Nkoanrua na kuhitimu darasa la saba mwaka 2005.

Elimu ya sekondari aliipata katika shule ya sekondari Kimandolu kati ya mwaka mwaka 2006 na 2010.

Lilian ambaye ni dada wa marehemu amesema Aneth alisoma Taasisi ya Teknolojia ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam na kupata stashahada ya utawala katika biashara kati ya mwaka 2016 na 2018 na baada ya kumaliza shule alikuwa akifanya biashara hadi umauti ulipomkuta hivi karibuni.

“Aneth angejua kuwa anakwenda kufa asingepanda ile ndege, hata sisi wenyewe ndugu tungemwambia asipande ile ndege ya asubuhi, ila ndo hivyo tupendane tu maana hakuna anayejua saa ya kuondoka duniani," amesema Lilian.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Richard Ruyango amesema kuwa, kauli ya mama mzazi wa marehemu kuwa, hatupaswi kulia imempa nguvu sana na kikubwa kinachotakiwa ni kuhakikisha kila mmoja wetu anaenda mema.

Amesema kwa Mkoa wa Arusha wamepoteza vijana wawili katika ajali hiyo na wote wamezikwa leo maeneo tofauti mkoani humo.  

Amesema kuwa, sasa hivi dunia inapoelekea  sipo na viongozi wa dini  wasichoke  kuelimisha jamii  kwani vijana wengi sasa hivi wanapambana  kulewa, kuiba hivyo viongozi wa dini wajitahidi sana kukemea hayo mambo kwenye nyumba za ibada ili mwisho wa siku watu waweze  kuishi kwa amani .