Manispaa ya Tabora yampongeza mtumishi wake kwa kumpa Sh3 milioni

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa ya Tabora,Tumaini Mgaya,kushoto,akipokea ngao kutoka kwa Meya wa Manispaa ya Tabora,Ramadhan Kapela,kulia,kutambua mchango wake katika utendaji kazi ambao hata Waziri Innocent Bashungwa aliagiza apewe tuzo.katikati ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tabora,Mohamed Katete.picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

  • Waziri Bashungwa amempongeza mtumishi huyo wakati akizungumza na makundi maalum mjini Tabora wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ukumbi wa Chuo cha Utumishi wa Umma.

Tabora. Manispaa ya Tabora imempongeza mtumishi wake wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Tumaini Mgaya kwa kutambuliwa utendaji wake na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa.

Waziri Bashungwa amempongeza Mgaya leo Mei 26 wakati akizungumza na makundi maalum mjini Tabora wakati wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ukumbi wa Chuo Cha Utumishi wa Umma.

Ameutaka uongozi wa Manispaa ya Tabora, kutambua mchango wake na kumpa tuzo ili kumpa Moyo yeye na watumishi wengine wa Manispaa.

Akizungumza katika Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Tabora, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Dk Peter Nyanja amewaeleza madiwani kuwa ni kweli mtumishi huyo anatekekeza wajibu wake vizuri na anastahili kupongezwa.

"Kwa kumpa tuzo kwa kweli anastahili na pia tunatekeleza agizo la Waziri kumpa tuzo mtumishi wetu," amesema.

Naye Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela mbali ya kumpongeza amesema hakuwa anafanya kazi peke yake bali na wenzake ambao ametaka nao watambuliwe kwa kupewa vyeti na fedha angalau hata Sh100,000 Kila mmoja.

Amesema uzoefu unaonesha kama anatambuliwa mmoja, basi huwa anawekewa vikwazo ili aonekane hafai.

"Mkurugenzi naomba na wenzake wa Idara yake nao wapewe vyeti na angalau uwashike mkono kwa Sh100,000 kila mmoja," amesema.

Tumaini Mgaya ambaye ni mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, amepewa ngao na fedha Sh3 milioni na Manispaa kama ishara ya kutambua mchango wake katika Utumishi wake.