Manny Pacquiao bondia anayetaka urais Ufilipino, kuondoa umaskini

Muktasari:

  • Bondia maarufu duniani, Manny Pacquiao (42) anaweza kuingia katika historia ya wanamichezo kuwa marais wa nchi zao kama alivyofanya mwanasoka George Weah wa Liberia aliposhinda kiti hicho mwaka 2017.


Bondia maarufu duniani, Manny Pacquiao (42) anaweza kuingia katika historia ya wanamichezo kuwa marais wa nchi zao kama alivyofanya mwanasoka George Weah wa Liberia aliposhinda kiti hicho mwaka 2017.

Pacquiao ametangaza kugombea urais wa Ufilipino utakaofanyika mwakani akiwa na lengo la kwenda kupambana na rushwa, umaskini na uwazi katika serikali ya taifa hilo la Asia.

Mwanamasumbwi huyo aliingia kwenye siasa mwaka 2010 na kuchaguliwa kuwa mbunge, baadaye mwaka 2016 alichaguliwa tena kuwa seneta, nafasi ambayo anaitumikia hadi sasa na amekuwa akifanya siasa huku akishiriki kwenye mchezo wa ndondi.

Pacquiao amepata umaarufu zaidi nchini humo kutokana na kujihusisha kwake na mchezo wa ngumi na amepigana na mabondia mbalimbali duniani, likiwemo pambano lake maarufu la Floyd Mayweather lililofanyika Marekani Mei 2, 2015.

Kutokana na umaarufu wake, kila alipowania uongozi nchini mwake alichaguliwa, huku akiweka wazi kuwa ujasiri wa kutaka kuwania urais katika taifa hilo linaloongozwa na Rais Rodrigo Duterte ambaye haruhusiwi kugombea tena katika uchaguzi wa mwakani.

Pacquiao anaamini kwamba sasa ni wakati wa mabadiliko na atashinda uchaguzi huko kwa sababu amependekezwa na kundi dogo katika chama chake cha PDP Laban ambacho ndicho chama cha Rais Duterte.

Mwanasiasa huyo anakabiliwa na kibarua kikubwa cha kuwahakikishia wananchi wa Ufilipino maisha bora, ikiwemo kutengeneza fursa za ajira ili kuzuia vijana wengi kutojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Rais Duterte amekuwa akipambana vikali na dawa za kulevya ambapo amekuwa akikosolewa na watetezi wa haki za binadamu kwa hatua anazozichukua katika vita ya dawa hizo.

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) inamtuhumu Rais huyo kwa uhalifu dhidi ya binadamu na kwamba mahakama hiyo huenda ikaamuru akamatwe baada ya kuondoka madarakani.

Hata hivyo, hatua ya Pacquiao kutangaza nia ya kuwania urais imepokelewa kuwa mwanzo wa mabadiliko katika taifa hilo na anakubalika na wanachama wengi, hasa ambao wanapingana na Rais Duterte.

“Wakati umewadia, tuko tayari kushiriki katika kinyang’anyiro cha urais,” amesema nyota huyo wa ndondi nchini Ufilipino ambaye amekubali kupeperusha bendera ya kundi lililojitenga na chama cha Rais Durtete.

Bondia huyo alifanya uamuzi wake huo wiki chache baada ya pambano lake la mwisho la ndondi dhidi ya raia wa Cuba, Yuben Yordenis Ugas, ambapo alishindwa Agosti 22 huko Las Vegas, Marekani.

Bondia pekee aliyewahi kuwa bingwa wa ulimwengu katika madaraja nane tofauti ya uzani, amekuwa ni sifa kubwa kwa Wafilipino.

Alikotoka

“Pac Man” alipokuwa mtoto, aliishi mitaani kabla ya kuingia kwenye ndondi Januari 1995 kwa fedha za peso 1,000 (sawa na Euro 19 au Sh57,000) na baadaye akajipatia utajiri unaokadiriwa kuwa zaidi ya Dola za Marekani 500 milioni.

Licha ya maarufu, ukarimu na mafanikio yake, lakini alizaliwa katika umaskini.

“Kwa wale wote wanaoniuliza ni ustadi gani na uwezo gani, je, umewahi kupata njaa?” Alisema Jumapili mbele ya wafuasi wake.

“Je, unajua ni nini kukosa chakula, kukopa pesa kutoka kwa majirani zako au kungojea mabaki ya chakula yaliyokusanywa kwenye migahawa? Manny Pacquiao aliye mbele yenu hapa alipitia mazingira hayo na alizaliwa katika familia maskini.”

Pacquiao alikuwa msaidizi mashuhuri wa Rais Durtete na vita yake yenye utata juu ya dawa za kulevya ambazo waendesha mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wanataka kuchunguza kwa madai ya mauaji yasiyokuwa halali ya makumi ya maelfu ya watu.

Ushindani waongezeka

Baada ya Pacquiao kutangaza nia, sasa anashindanishwa na Christopher “Bong” Go katika uchaguzi ujao, hata hivyo, Go anasema hataki kumrithi Rais Duterte.

Chama chake kinaonyesha nia ya kumpendekeza Go, lakini bado wanaendelea kumshawishi ili afikirie tena uamuzi wake. Kukataa kwake uteuzi huo kumeibua hisia kwamba binti wa Rais Duterte, Sara anaweza kugombea nafasi hiyo.

Bado haijajulikana ni nani katika vikundi ndani ya PDP-Laban na kikundi kipi kitatambuliwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Baadhi ya wachambuzi wa duru za siasa nchini humo walinukuliwa na BBC wakieleza kwamba kwa sababu Rais Duterte hana uwezo wa kuwania awamu nyingine, alisema anataka kuwania nafasi ya Makamu wa Rais.

Chanzo hicho kilieleza kwamba kwa namna anavyoonekana angependa nafasi ya urais iende kwa mmoja wa watu wa familia yake au walio karibu naye.