Maofisa habari wa Serikali kushiriki vikao vya menejimenti

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Muktasari:

  • Serikali inasema inakamilisha mkakati utakaowaruhusu maofisa habari kushiriki vikao vya maamuzi katika taasisi zao.

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Serikali ipo mbioni kufanikisha utaratibu wa kisheria utakaowaruhusu maofisa habari wa Serikali kushiriki vikao vya maamuzi katika taasisi zao.

Kauli hiyo ya Nnauye inakuja wakati ambao, Maofisa habari wanalalamikia mfumo wa Kazi yao kuwa kikwazo cha utendaji wao, wakisisitiza hawana nafasi hata ya kushiriki vikao vya juu vya taasisi zao.

"Mfumo unamfanya ofisa habari kuchukuliwa kama mtu wa kupiga picha viongozi tu na wakati mwingine haruhusiwi kushiriki hata vikao, ataitwa kama viongozi wanataka kupigwa picha,” amesema Katibu Mkuu wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano (PRST), Ndege Makura.

Kauli ya Nnauye ameitoa leo, Machi 27, 2023 katika kikao kazi cha 18 cha maofisa habari, uhusiano na mawasiliano wa Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

"Kama Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa anaingia kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri kwanini hawa Maofisa habari wasishiriki vikao vya maamuzi katika taasisi zao," amesema.

Amesema haoni sababu ya maofisa habari kutoshiriki vikao vya maamuzi vya taasisi zao, akisisitiza mkakati unaoandaliwa utakuja na jawabu hilo.

Amesema pamoja na mkakati huo, mwingine unaoandaliwa ni ule wa taarifa wakati wa majanga na mkakati wa kujitagaza ambayo yote inatarajiwa kuleta mapinduzi katika sekta ya habari.

Hata hivyo, amesema mikakati hiyo itaweka wajibu wa kila mdau katika mnyororo wa thamani wa upatikanaji habari.