Maofisa TFDA wapandishwa kizimbani

Maofisa wanne wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) wakipelekwa katika chumba cha hakimu kwa ajili ya kusomewa shtaka moja la kuisababishia hasara mamlaka hiyo ya Sh58,390,000.Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

Maofisa wanne wa Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la uhujumu uchumi.


Dar es Salaam. Maofisa wanne wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) wamepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka moja la kusababisha hasara ya Sh58,390,000 kwa kuidhinisha malipo mara mbili kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo.

Waliosomewa hati ya mashtaka ni Raymond Wigenge, Ezekiel Mubito, Adelard Mtenga, Abdalah Juma na mshtakiwa wa kwanza, Chary Ugullum ambaye hata hivyo hajafikishwa mahakamani.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwezile alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja wanashtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi.

Wakili Swai alidai kuwa kati ya Mei na Desemba mwaka 2016 washtakiwa hao wakiwa katika ofisi ya TFDA kwa uzembe waliisababishia hasara ya kiasi cha Sh58,390,000 kwa kuidhinisha posho maalumu kwa wafanyakazi ambao walishalipwa na kufanya walipwe mara mbili jambo ambalo ni kosa la kisheria.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa walikana shtaka hilo na upande wa Jamhuri walidai kuwa upelelezi umekamilika na waliomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali.

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rwezile alisema dhamana kwa washtakiwa hao ipo wazi hivyo wanatakiwa wadhamini wawili wawe na kitambulisho cha Taifa (Nida) na barua za utambulisho.

Pia kati yao mmoja awasilishe fedha taslimu Sh5.8 milioni au hati yenye thamani ya Sh5.8 milioni.

Hata hivyo washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo wote wamerudishwa mahabusu.

Hakimu Rwezile aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikiliza hoja za awali.