Maofisa wane wa IEBC wafukuzwa kazi

Muktasari:

Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya Kenya kufanya uchaguzi mkuu, kesho Jumanne, Agosti 9, 2022, maofisa wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya wamefukuzwa kazi kwa kushiriki kampeni siku ya ufungaji wake na kufanya mikutano ya siri na baadhi ya wagombea.

Nairobi. Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya Kenya kufanya uchaguzi mkuu, kesho Jumanne, Agosti 9, 2022, maofisa wanne wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya wamefukuzwa kazi kwa kushiriki kampeni siku ya ufungaji wake na kufanya mikutano ya siri na baadhi ya wagombea.
Maofisa hao awali walifanikiwa kukimbia polisi walipokuwa kwenye mikutano ya kampeni lakini walikamatwa wakiwa wanafanya mkutano katika nyumba na wagombea.
Kwenye sakata hilo baadhi ya maofisa wa IEBC waliohudhuria kampeni hizo walifanikiwa kukimbia walipoona kundi kubwa la watu likiwafuata.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, nafasi za maofisa hao zitajazwa leo na amewataka watumishi wote wa tume hiyo kuzingatia maadili na kiapo cha kazi yao.
Chebukati amesema kwa mujibu wa maadili yanayoongoza IEBC, watumishi wake wanatakiwa wasiwe na upande wowote wa kisiasa ili watende haki kwenye kazi zao hivyo kitendo cha maofisa hao kushiriki kampeni na kufanya mikutano na wagombea kinatoa taswira mbaya.
Tayari mgombea urais kwa tiketi ya Kenya Kwanza  na Naibu Rais, William Ruto ameionya IEBC isijihusishe na upendeleo wa chama au mgombea yoyote na wahakikishe wanatenda haki kwenye uchaguzi utakaofanyika kesho.
Mwisho.