MAONI: Afrika inahitaji nidhamu, umakini katika ukopaji

Thursday December 02 2021
maoni pic
By Ephrahim Bahemu

Uhusiano wa China na mataifa ya Afrika kwa muda mrefu umekuwa wa kupigiwa mfano, lakini kwa siku zijazo huenda ikiwa tofauti kwa kuwa tayari kuna ishara zisizo njema dhidi ya urejeshaji wa mikopo ambayo nchi za Afrika imeichukua.

Baadhi ya mataifa ya Afrika hutegemea mikopo mikubwa kutoka China ili itekeleze miradi ya maendeleo.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi 2019 China ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 153, ambazo ni sawa na Sh352.2 trilioni za Tanzania, huku mkopaji mkubwa ni Angola.

Ukiachilia mbali Angola, katika orodha ya nchi zenye madeni mkubwa kutoka China zipo Ethiopia, Zambia, Kenya, Sudan, Nigeria, Cameron, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, Misri na Ghana.

Ukizungumzia mikopo ya China kwa mataifa ya Afrika kumbukumbu miongoni mwa wengi itakuwa ni taarifa za kudaiwa kutwaliwa kwa uwanja wa ndege wa Zambia kwa kile kinachodaiwa ni kushindwa kurejesha mkopo wao kutoka China mwaka 2018.

Hivi karibuni kulikuwepo kwa taarifa za China kutaka kutwaa reli ya Kenya kwa kisa kinachofanana, jambo lililowalazimu Kenya kukimbilia Shirika la Fedha duniani (IMF) kuchukua mkopo ili kuhudumia deni hilo, taarifa kuhusiana na sakata hilo zilianza kusambaa Septemba mwaka huu.

Advertisement

Miezi miwili baadaye Taifa jingine la ukanda wa Afrika Mashariki linapata mtihani kama huo, ambapo duru ndani ya Uganda zilieleza kuwa uwanja wa Kimataifa wa nchi hiyo (Entebbe) huenda ukatwaliwa kwa kushindwa kulipa deni la China baada ya mazungumzo kati ya viongozi na mkopeshaji kuhusu deni hilo kugonga mwamba.

Wengi wamekuwa wakikimbilia mikopo ya China kwa kuwa haina masharti mengi kama ilivyo ya mataifa mengine na mashirika ya kimataifa, hilo linatokana na sera ya mambo ya nje ya China ambayo haijihusishi na masuala ya ndani ya Taifa jingine. Sera hii hupendwa na mataifa mengi ya Afrika.

Ukiomba mkopo China kinachozingatiwa zaidi ni kusudio la mkopo na namna ya kurejesha na wala hawatoi masharti ya ziada ya kile cha kufanya katika nchi yako, kwa ufupi fedha yao ni ya haraka haraka isiyo na mizengwe mingi.

Hata hivyo, lengo langu si kujadili kuhusu madeni China kwa mataifa ya Afrika, la hasha, kwani nchi hiyo si mkopeshaji pekee Afrika, licha ya kuwa masharti ya mikopo yake yamekuwa yakitajwa kuwa ni magumu, lakini wakopaji huelezwa mapema na kuyakubali sio kwa kulazimishwa.

Lengo ni kuzungumzia nidhamu ya kukopa kwa Serikali za mataifa ya Afrika, lakini kuna kauli wanazoambiwa wananchi wa nchi zinazokopa kuwa wamepewa mkopo wenye masharti nafuu, lakini hawaambiwi athari za mkopo usiporejeshwa kwa wakati.

Ukopaji kwa nchi zinazoendelea haukwepeki, hasa mikopo inapokuwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, hata mataifa makubwa ambayo hukopesha mataifa yanayoendelea nayo hukopa ili kutimiza mipango yao ya maendeleo.

Mtaani tukianza kusimangwa na madeni huwa tunasema anayekopeshwa anayekopesheka, kwa maana kuwa anayepata mkopo ni mwenye uwezo wa kulipa.

Katika minajili hiyo, deni si baya, bali jambo la kuzingatia ni kwa nini unakopa na unakopa kwa masharti yapi, masharti hayo hayaufanyi kuwa mkopo umiza kama vile ambavyo wananchi hulia kupigwa, kwa viongozi wa nchi wenye uzalendo wanapaswa kuiona mikopo husika kama binafsi ili kuupa umuhimu wa kipekee.

Kiongozi kabla ya kuingia mkataba fikiria nchi ndiyo kama familia yako na mali zako unazozimiliki halafu uone kama ingekuwa kwa masharti hayo uliyopewa ungekubali kukopa?

Mara nyingi mikopo ya nchi, hususani ya maendeleo huiva baada ya muda mrefu, marejesho yake yanaweza yasiwe miaka mitano ijayo au ikaanza kulipwa wakati aliyeidhinisha ukopaji hayupo hai, lakini kwa kuwa ni mkopo wa nchi deni hilo hulipwa na waliopo muda huo.

Deni hulipwa kutokana na mapato ya Serikali, hivyo kodi hutumika, asiyelipa deni hilo, kizazi kitalipa na huenda Serikali ikabidi ikaze kwenye ukusanyaji wa kodi ili ilipe deni au kupunguza fungu la maendeleo ili kuhudumia deni.

Nasisitiza uzalendo na umakini katika mikopo kwa kuwa nchi siyo kwa ajili ya waliopo sasa, bali ni urithi wa kizazi na kizazi.

Hatari zaidi ni kwamba wakopeshaji nao pindi urejeshaji unapokwama hupendelea kutwaa yale maeneo ya kimkakati katika maendeleo ya nchi kama bandari, uwanja wa ndege, mtandao wa reli kwa kile ambacho wanaamini hapo ndipo watarejesha fedha.

Tunapaswa kuwa makini na uamuzi unaofanyika sasa ili vizazi vijavyo visije kukosa kurithi nchi iliyokamili.

Kuna wasiwasi wakakuta sehemu ya nchi inamilikiwa na ambao walioikopesha nchi.

Advertisement