MAONI: Ndalichako na kibarua cha mageuzi ya elimu

Muktasari:

Akiwa miongoni mwa mawaziri sita waliodumu katika baraza la mawaziri la Rais John Magufuli kwa miaka mitano ya kwanza, kurudi kwa Profesa Joyce Ndalichako katika wadhifa wake ni ishara kuwa bado anaaminiwa na bosi wake.

Akiwa miongoni mwa mawaziri sita waliodumu katika baraza la mawaziri la Rais John Magufuli kwa miaka mitano ya kwanza, kurudi kwa Profesa Joyce Ndalichako katika wadhifa wake ni ishara kuwa bado anaaminiwa na bosi wake.

Awali Profesa Ndalichako aliteuliwa kuwa mbunge mwaka 2015 kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Elimu, akitokea kwenye uga wa wanataaluma (mhadhiri). Kabla ya hapo alipata umaarufu zaidi alipokuwa Katibu mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Kwa hiyo kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Elimu kulipokelewa kwa matumaini makubwa na Watanzania walio wengi walioamini kuwa sasa upele umepata mkunaji.

Sekta ya elimu nchini inakabiliwa na changamoto nyingi zinazojirudia miaka nenda rudi. Kwa mfano, changamoto ya uhaba wa walimu tangu shule za msingi, sekondari hadi vyuoni, ilitarajiwa kupatiwa majibu katika uongozi wa Profesa Ndalichako.

Kwa mujibu wa takwimu za elimumsingi ( BEST) za mwaka 2016 na 2017, idadi ya walimu kwa shule za msingi imeshuka kutoka walimu 191,772 mwaka 2016 hadi kufikia 179,291 mwaka 2017, ikiwa ni anguko la asilimia 6.5 na kufanya uwiano wa walimu na wanafunzi kuwa 1:50.

Pia katika shule za awali, idadi iliyopungua ni walimu 1,948 hivyo kufanya uwiano wa walimu na walimu na wanafunzi kuongezeka kutoka 1:135 mwaka 2016 hadi kufikia 1:159 mwaka 2017 badala ya 1:25 ambao ni uwiano unaokubalika.

Licha ya uhaba wa walimu, walimu waliopo wana kabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za kutopandishwa madaraja, mishahara na kutokuwa na mazingira mazuri ya kazi.

Hili ndilo eneo ambalo Profesa Ndalichako alipaswa kuanza nalo katika miaka mitano iliyopita. Lakini tumeona katika miaka mitano, Serikali ikijiweka karibu tu na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ilhali matatizo yako palepale.

Changamoto nyingine ni utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambapo kwa kiasi kikubwa Serikali imeitumia kutoa elimumsingi bila malipo.

Katika sera hiyo, Serikali ilitoa waraka namba 8 wa mwaka 2011 unaoelekeza kufutwa kwa ada na michango shuleni. Pia ada ya mtihani kwa kidato cha pili na cha nne nayo imefutwa rasmi.

Lakini changamoto imekuja kwenye ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa kulingana na miundombinu iliyopo yakiwamo madarasa, maabara na madawati.

Pia kutokana na uhaba wa walimu, ongezeko hilo limefanya kazi ya ufundishaji kuwa ngumu.

Kwa shule ambazo hazikuwa na walimu wa kutosha hasa masomo ya sayansi, hali imekuwa mbaya kwa sababu hata waliokuwa wakigharamikiwa na wazazi waliacha kazi kwa sababu Serikali ilifuta michango ya wazazi.

Mbali na utoaji wa elimu bila malipo, utekelezaji wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 bado haujakamilika, huku kukiwa na mkanganyiko kati ya sera na sheria ya elimu.

Kwa ujumla, utekelezaji huo haujaleta matokeo chanya, kwa kuwa suala la ubora wa elimu limebaki kuwa kitendawili. Ushahidi ni matokeo ya mitihani ya kitaifa ambapo shule za Serikali zinazotoa elimu bure zimeonekana kuwa nyuma, huku shule binafsi zikifanya vizuri zaidi.

Changamoto nyingine ni kwenye utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Licha ya suala hilo kuwapo kabla hata ya awamu ya tano, lakini ilani ya Serikali ya awamu ya tano ilisisitiza kuondoa bugudha kwa wanafunzi wanaonufaika.

Lakini sote ni mashahidi jinsi ambavyo utoaji huo umekuwa ukikunmbwa na kero. Changamoto hazikosekani kila mahali, lakini kibaya ni pale wanafunzi wanapohoji ahadi ya kutobughudhia kupata mikopo hiyo wanapotishiwa kwa kusimamishwa masomo.

Waziri Ndalichako kama mzazi anapaswa kuliangalia suala hili. Isitoshe, mikopo yenyewe imeongezwa riba mpaka asilimia 15, jambo linalokuwa mzigo kwa wakopaji hata wanapoajiriwa.

Jambo lingine linalomsubiri Profesa Ndalichako ni ubora wa elimu. Changamoto nilizotaja na nyinginezo zinaathiri utoaji wa elimu kwa wanafunzi.

Miongoni mwa matokeo yake ni kupata wanafunzi mbumbumbu wasiojua kusoma na kuandika, hawana uelewa fasaha wa lugha za kufundishia na hata wakimaliza vyuo vikuu hawaajiriki.

Kwa kuwa Profesa Ndalichako amerudishwa tena katika wizara hiyo, analo jukumu kubwa la kuleta mageuzi yatakayoweka alama katika sekta ya elimu. Inawezekana mambo mengine yako juu ya uwezo wake, lakini kwa kutumia nafasi yake anaweza kujenga hoja serikalini ili kuinua kiwango cha elimu nchini.

Elias Msuya ni mwandishi wa Mwananchi. [email protected]