MAONI: Watafiti wa ndani watatue kero za jamii

Tuesday December 22 2020
WATAFITIPIC

Taarifa za Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) kugundua chanjo inayozuia magonjwa matatu ya kuku sio tu zinaongeza morali wa kujiamini na kuwatumainia watafiti wazawa bali kunadhihirisha uchumi wa viwanda unawezekana.

SUA wamegundua chanjo wanayoiita Tatumoja inayodhibiti mdondo, ndui na mafua ya kuku. Magonjwa haya yote, yamekuwa chanzo kikuu cha vifo vya kuku hivyo kuwasababishia hasara wafugaji wengi.

Kwa ugunduzi uliofanywa na chuo kikuu hicho, sasa mfugaji anao uhakika wa kuwakinga kuku wake wote kwa chanjo moja badala ya tatu tofauti zilizokuwapo awali. Uhakika wa afya ya mifugo hii inayotumika zaidi kwa kitoweo cha familia, sherehe hata maakuli ya jumuiya, utasaidia kuleta mapinduzi katika ufugaji wa kuku unaotatizwa kwa kiwango kikubwa na magonjwa hasa ya mlipuko.

Tofauti na chanjo zilizopo, tumeelezwa Tatumoja inaweza kutunzwa kwenye mazingira ya kawaida. Haihitaji kuwekwa kwenye ubaridi. Mfugaji anaweza kubaini iwapo imechakachuliwa kwa kuongezwa kitu kingine.

Ugunduzi huu wa SUA unatoa hamasa kwa vyuo vingine kujielekeza katika kutatua kero zinazowasumbua wananchi. SUA wamethibitisha kuwa wasomi wetu wanao mchango mkubwa wa kusaidia kuondoa changamoto zinazoisumbua jamii.

Kwa mwendo huu, iwapo vyuo vingine navyo vitajielekeza kutatua changamoto za kijamii, si tu umuhimu wa watafiti nchini utaongezeka bali Tanzania itaweza kujisimamia na jamii itashuhudia hadhi yao ikipanda zaidi kuliko wengi wao kukimbilia kwenye siasa badala ya kutumia taaluma zao zilizowekezwa kwa muda mrefu wa maisha yao.

Advertisement

SUA waliojikita kwenye kilimo wamefanya kitu kwa ajili ya wafugaji, vyuo vingine navyo vijielekeze kwenye maeneo waliyobobea kuleta suluhu za uhakika na za kudumu ili kuifanya Tanzania ijitegemee kwa teknolojia na maarifa. Utafiti unaoisaidia jamii kwa kiasi hiki, tunaamini unahitajika zaidi.

Wataalamu wa Kitanzania sasa wanayo fursa ya kutafiti na kuifikisha bidhaa sokoni kwa ajili ya jamii. Tunaamini, viwanda vitakavyoanzishwa kuzalisha bidhaa zitokanazo na utafiti wa aina hii vitakuwa endelevu kwani vitaweza kushindana ndani hata nje ya mipaka kutokana na ukomavu wa wagunduzi wa bidhaa husika.

Huenda wanataaluma hawa walikuwa wamesahaulika ila sasa ni wakati wao kudhihirisha kuwa bado wanahitajika katika jamii kuongoza mapambano dhidi ya changamoto zinazowakabili wananchi.

Baadhi ya kero zilizopo zinahitaji nguvu ya wanataaluma. Hakuna madaraka wala cheo kinachoweza kuzalisha chanjo kama walivyofanya watafiti wa SUA isipokuwa umakini wa taaluma walizonazo. Jamii inahitaji vitu hivi ilivyovikosa kwa muda mrefu.

Serikali iongeze nguvu kuwawezesha watafiti wetu. Taasisi binafsi pamoja na viwanda vilivyopo navyo viwatumie watu hawa ili kuharakisha utatuzi wa changamoto zilizopo kwa gharama nafuu ikilinganishwa na kuagiza teknolojia zinazotengenezwa nje kisha kuja kutumika nchini.

Tunawapongeza SUA kwa kufungua milango ya kufanya utafiti wenye faida kwa jamii na kuvisihi vyuo vingine kufuata uelekeo huo ili kuwa na jamii isiyokwamishwa na mambo mengi kuyatafuta maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kwa muongozo wa wanataaluma, tunaamini jamii itapiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii hata kisiasa. Jamii yenye uelewa utokanao na utafiti wa kina itaweza kukabiliana na changamoto zilizopo kwa uhakika zaidi.

Advertisement