Mara kuanza msako wazazi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni

Mkuu wa mkoa wa Mara, Ally Hapi akiongea na baadhi ya wazazi na wanafunzi katika shule ya Sekondari Mmazami wilayani Butiama  alipofanya ziara shuleni hapa kukagua madarasa matatu yaliyojengwa kwa fedha za Uviko-19. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amewaaagiza watendaji wa kata zote kwa kushirikiana na polisi kuwakamata wazazi wote ambao watoto wao watashindwa kusajiliwa shuleni kwaajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Butiama. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi amewaaagiza watendaji wa kata zote kwa kushirikiana na polisi kuwakamata wazazi wote ambao watoto wao watashindwa kusajiliwa shuleni kwaajili ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza.

Hapi ametoa agizo hilo leo Januari 18, 2022 wilayani Butiama wakati wa ziara ya kukagua na kukabidhiwa madarasa yaliyojengwa na fedha za Uviko-19 wilayani humo ambapo amesema kuwa msako wa wazazi wa watoto ambao hawataripoti shuleni uanze Jumatatu ya wiki ijayo.

Amesema kuwa suala la utoro shuleni limekuwa ni tatizo sugu mkoani Mara hali ambayo imekuwa ikichangia matokeo mabaya katika mitihani ya kitaifa hivyo serikali haiwezi kulifumbia macho.

Amesema kuwa wamebaini sababu kadhaa zinazosababisha utoro mashuleni na kutaja baadhi ya sababu hizo kuwa ni wazazi kuwashirkisha watoto wao kwenye shughuli za kilimo, biashara na hata ajira huku wengine wakiwalazimisha mabinti kuolewa na kuacha shule.

"Sasa hivi hakuna mzazi aliyesumbuliwa na mchango wa ujenzi wa darasa lakini pia tayari nimetoa muda wa mwezi mmoja watoto ambao hawana sare waende shule hata wakivaa madera hakuna shida kwahiyo mzazi kushindwa kumpeleka mtoto shule ni makusudi tu na hatuwezi kukubali hali hiyo" amesema Hapi

Akitoa taarifa ya mradi wa Uviko-19 katika sekta ya elimu mkurugenzi wa halmashauri  ya wilaya ya  Butiama,  Patricia Kabaka amesema kuwa kupitia mradi huo wameweza kujenga madarasa 78, bweni moja la wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ofisi 34 za walimu pamoja na viti na madawati 2,880.

Amesema kuwa wilaya hiyo ilipokea Sh1.64 bilioni kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba kukamilika kwa mradi kutawezesha wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari watapata nafasi.