Martha Karua katika mtihani wa kihistoria

Martha Karua

Muktasari:

Uteuzi wa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga, umekuwa na msisimko mkubwa kuliko ule wa Rigathi Gachagua, atakayesimama na William Ruto.

Uteuzi wa Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga, umekuwa na msisimko mkubwa kuliko ule wa Rigathi Gachagua, atakayesimama na William Ruto.

Msisimko huo kwa sehemu kubwa unakuzwa na hoja moja; Martha ni mwanamke. Uteuzi wake wa kuwa mgombea mwenza unampandisha daraja Raila kuwa kiongozi anayeheshimu nguvu ya wanawake.

Wanaharakati wa haki za wanawake wamepokea uteuzi wa Martha kuwa mgombea mwenza kama karata kuu ya kuipigania katika Uchaguzi Mkuu Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, 2022.

Ruto, ambaye ni Naibu Rais wa Kenya, bila shaka ananyimwa usingizi na uteuzi wa Martha. Na mipango ya sasa ni kufanya mashambulizi ya haraka ili kudhoofisha athari ambayo inaingia kwa wanawake kwa kasi kubwa.

Tangu Raila, anayegombea urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja One Kenya, amtangaze Martha kuwa mgombea mwenza, mwanasheria huyo mahiri na mtetezi wa haki za binadamu amekuwa akitajwa mno kuliko Gachagua wa Ruto.

Hilo ndilo linajenga hofu kubwa upande wa Ruto, wakipanga mbinu za kutumia wanawake kudhibiti karata ya Martha. Hivyo, yanakwenda kuwa mapambano ya wanawake kwa wanawake.

Mbunge wa Kandara, Alice Wahome ni mwanamke na alikuwa mmoja kati ya majina yaliyokuwa yanatajwa katika kinyang’anyiro cha kumpata mgombea mwenza wa Ruto kupitia Kenya Kwanza. Hata hivyo, dodo likamdondokea Gachagua.

Hivi karibuni, Alice alihudhuria mazishi ya kaka wa kambo wa Gachagua, yaliyofanyika kwenye Kijiji cha Hiriga, Jimbo la Mathira. Akiwa kwenye shughuli hiyo ya mazishi, Alice aliwataka wanawake kupuuza uteuzi wa Martha kuwa mgombea mwenza, kwani ni mwanamke mmoja na hauleti usawa wa kiuongozi.

Mkakati ni kuwatumia Alice na wanawake wengine ndani ya Kenya Kwanza ili kuonyesha kuwa uteuzi wa Martha ni utapeli tu wa kisiasa unaofanywa na Raila pamoja na timu yake ya Kenya Kwanza.

Kazi ya Raila na Azimio ipo kwenye makundi mawili; mosi ni kuendelea kutetea uamuzi wa kumteua Martha na kuujengea uhalali kwa jinsia zote. Pili ni kubadili msisimko ambao umeletwa na Martha kuwa kura halisi.

Kuelekea kupata jina la mgombea mwenza, kila upande ulikuwa unapiga hesabu kuhusu kura za Mlima Kenya. Kwa Ruto kumteua Gachagua, maana yake tayari amejenga ushawishi Mlima Kenya.

Raila, kwa kumteua Martha ambaye naye anatokea Mlima Kenya, maana yake anajaribu kupiga ndege wawili kwa jiwe moja; kupata kura za Mlima Kenya, pili kujenga ushawishi kwa wanawake.

Sasa matarajio ni kuwa kampeni kubwa ndani ya Mlima Kenya, sio tena Raila na Ruto, bali Martha na Gachagua. Je, nani ataweza kuwafanya wananchi wa Mlima Kenya wamwone ndiye anafaa zaidi?

Ipo hoja inajengwa upande wa Kenya Kwanza kuwa Martha alishakuwepo kwenye sanduku la kura mwaka 2013. Na kura alizopata hazikuonyesha kuungwa mkono na wanawake.

Nguvu ya wanawake pia inapimwa kwa kuwatazama wanawake wengine waliothubutu kuwania urais Kenya mwaka 1997, Charity Ngilu na Wangari Maathai.

Hoja nyingine dhidi ya Martha ni uwakilishi duni wa wanawake kwenye Bunge, Seneti, mabunge ya kaunti, vile vile magavana. Hapa ni kuonyesha kuwa wanawake hawashawishi sana kura.

Mwaka 2013, Martha akigombea urais na mgombea mwenza wake akiwa Augustine Lotodo, alipata kura 43,881, sawa na asilimia 0.36 ya waliojitokeza kuchagua Rais. Akashika nafasi ya sita kati ya wagombea wanane waliokuwa wanawania nafasi ya urais wa Kenya. Haya yalikuwa matokeo mabaya kwa mtu ambaye alikuwa mbunge tangu mwaka 1992, akawa waziri kwenye Serikali iliyoongozwa na Rais Mwai Kibaki.

Mwanamke mwingine aliyegombea urais Kenya mwaka 2013 ni Winnie Kaburu, ambaye mgombea mwenza wake alikuwa Profesa James Kiyiap. Winnie alipata kura 40,998, sawa na asilimia 0.34 ya kura zote zilizohesabiwa.

Mwaka 2013, pacha wa zamani wa Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta na William Ruto, walikusanya kura milioni 6.2 na kushinda uchaguzi, wakifuatiwa na ‘mapatna’ waliovurugana hivi sasa, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka, waliopata kura milioni 5.3. Musalia Mudavadi na Jeremiah Kioni, walitoka wa tatu na kura zao 484,000.

Mwanamke mwingine aliyewahi kupata kura chini kabisa ya matarajio Kenya ni Wangari Maathai. Mwaka 1997, alipata kura 4,246, sawa na asilimia 0.07, akisalia wa 13 katika wagombea 15.

Angalau Charity Ngilu, ambaye hivi sasa ni Gavana wa Kitui. Mwaka 1997, Charity akiwa mbunge wa Kitui Kati, aligombea urais na kupata kura 488,600, akiwa na Chama cha Social Democratic (SDP). Katika uchaguzi huo Charity alisalia katika nafasi ya tano katika wagombea 15.

Kura za Charity mwaka 1997, hazikumweka mbali sana waliopata juu yake. Mshindi alikuwa Rais Daniel Arap Moi, aliyepata kura milioni 2.5, wa pili alikuwa Mwai Kibaki, ambaye hakufikisha milioni mbili.

Raila ndiye alitoka wa tatu mwaka 1997. Kura zake zilikuwa 668,000 na kijana Wamalwa alikuwa wa nne, kura zake zikizidi kidogo nusu milioni. Ukipima kura za Raila na Wamalwa kwa kuzitazama za Charity, unapata picha jinsi alivyojenga ushawishi.

Wanawake wengine waliopata kugombea urais Kenya ni Nazlin Omar mwaka 2007 kupitia chama cha Workers Congress, alipata kura 8,624 sawa na asilimia 0.09. akishika namba sita kati ya wagombea tisa. Mwaka 2017, alikuwepo Miriam Mutua, ambaye alisimama kama mgombea mwenza wa Michael Wainaina, aliyekuwa anawania urais kama mgombea binafsi. Wainana na Miriam walipata kura 8,870, sawa na asilimia 0.06 ya kura zote zilizohesabiwa.


Hitimisho

Martha ameleta msisimko kwa kuwa ni mwanamke na ndio maana Kenya Kwanza ya Ruto wanapigana kumnyamazisha. Hata hivyo , historia haiwapendelei wanawake kwenye mbio za urais Kenya.

Hivyo, Martha akitaka kusimama kweli kama mwanamke, ana vita tatu kubwa; mosi, kuhakikisha Raila anapata kura nyingi Mlima Kenya. Pili, nguvu yake iakisi kura za wanawake nchi nzima. Tatu, atatazamwa kama mshindi kama Raila atashinda na yeye kuwa Naibu Rais, hivyo kubadili historia mbaya ya wanawake kushindwa hovyo kwenye urais.