Marwa kufanyiwa upasuaji

Muktasari:

  • Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imesema inatarajia kumfanyia upasuaji mkubwa wa kuwekewa mfupa bandia wa kuzuia utosi kijana Marwa Msyomi (30) baada ya matibabu ya upasuaji wa kubadilisha fuvu la kichwa kufanikiwa.

Dar es Salaam. Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imesema inatarajia kumfanyia upasuaji mkubwa wa kuwekewa mfupa bandia wa kuzuia utosi kijana Marwa Msyomi (30) baada ya matibabu ya upasuaji wa kubadilisha fuvu la kichwa kufanikiwa.

Februari 28 mwaka huu gazeti hili liliandika habari kumhusu kijana huyu namna alivyoishi miaka saba na rufaa mkononi akishindwa kufika Muhimbili kutokana na changamoto za kiuchumi na hali yake ya kiafya ambapo MOI ilielekeza mgonjwa huyo afikishwe hospitalini hapo kwa matibabu.

Marwa alifanyiwa upasuaji wa kwanza Machi 9 mwaka huu, baada ya mgonjwa huyo kukaa muda mrefu bila tiba, hivyo fuvu bandia alilowekewa awali kupata maambukizi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Daktari bingwa wa upasuaji magonjwa ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Hamis Shaban alisema jopo la madaktari wanatarajia kumfanyia tena upasuaji Marwa miezi mitatu tangu afanyiwe upasuaji wa awali: “Tunatarajia ndani ya miezi mitatu atakuwa amepona haya maambukizi halafu atarudi tena hospitali tuje tufungue tena kile kidonda halafu tumwekee mfupa wa bandia kuzuia ule utosi kwa sababu hawezi kuishi na fuvu la kichwa ambalo halijafungwa, ni hatari, akipatiwa tiba hizo itakuwa tumemaliza matibabu,” alisema Dk Shaban.

Akizungumzia upasuaji waliomfanyia awali, Dk Shaban alisema walitoa usaha mwingi uliokuwa ukionekana juu ya kichwa kiasi wengi kudhani ubongo uko wazi, lakini ulikuwa ndani ya ngozi ya ubongo.

“Tuna wagonjwa wengi sana ambao tumewawekea vifaa bandia kuzuia utosi na huwa tunawaambia kabisa lazima wawe na ratiba maalumu kurudi hospitali, tunachoangalia ni ngozi kama imekaa sawasawa ambacho ndiyo kitu wanachokiona nyumbani.

“Kwa tatizo alilopata Marwa anaweza kupata ugonjwa wa kifafa au degedege, wengi hawahitaji kufanyiwa upasuaji, tunawapa dawa za kuzuia kifafa na wanaishi maisha ya kawaida, huyu ndiyo mtu pekee aliamua kukaa miaka saba,” alisema Dk Shaban.

Hata hivyo, Marwa alisema kwa sasa ameruhusiwa kutoka hospitalini na amekuwa akipokea matibabu kwa kuhudhuria kliniki.

Mke wa Marwa, Jane Marwa alisema mumewe anaendelea vizuri na hatoi harufu kama awali, ila miguu imekosa nguvu ya kusimama.

Unaweza kumsaidia Marwa kwa kutumia namba 0747362904 iliyosajiliwa kwa jina Matinde Msyomi au piga simu kwa mhariri wa Mwananchi.