Masanja Mkandamizaji anatukumbusha maadili ya diplomasia

Friday December 17 2021
masanjapiic
By Noor Shija

Desemba 9 ilikuwa siku ya uhuru wa Tanganyika. Nchi ilikuwa imetimiza miaka 60 tangu ipate uhuru Desemba 9 mwaka 1961. Lilikuwa tukio kubwa na la kipekee kwa nchi.

Viongozi kadhaa kutoka nchi jirani, akiwamo Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Philipe Nyusi wa Msumbiji na Paul Kagame wa Rwanda walikuja kushiriki maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uhuru.

Kilichofanywa siku hiyo na mchekeshaji Masanja Mkandamizaji hakipaswi kuachwa kipite bila kusemwa ili tujisahihishe. Na suala hili ndio limekuwa mada kwenye mitandao ya kijamii, kila mmoja akisema lake.

Mchekeshaji huyo, baada ya kuona maonyesho ya kazi mbalimbali za kijeshi ikiwamo ushonaji wa nguo za maofisa, uokoaji na zana za kivita, akili yake ikalenga ikajielekeza kwenye zana za kivita pekee na kuacha mambo mengine mazuri ya jeshi yanayofanywa kwa wananchi.

Mchekeshaji huyu alifikia hatua ya kutamka zana hizo za kivita zinakaa tu bila kazi, hivyo Tanzania iombe vita na Rwanda ili zifanyiwe majaribio kuliko ilivyo sasa kwamba zimekaa tu.

Unaweza kuona ni kauli ya kuchekesha, lakini imefikisha ujumbe. Nasema hivyo nikikumbuka mahojiano yangu na Jaji Joseph Warioba hivi karibuni. Jaji Warioba alinieleza alivyofunzwa na Mwalimu Nyerere jinsi ya kupata ujumbe wa wananchi kwenye mikutano ya hadhara.

Advertisement

Alisema Mwalimu Nyerere alimwambia awe makini kusikiliza kila kinachoelezwa na wananchi, ikiwamo hotuba yao, nyimbo, ngonjera na maigizo, huko kote huwa kuna ujumbe kwa mgeni rasmi.

Kauli ya Masanja siku ya Desemba 9 inaweza kuwa ililenga kuchekesha lakini si wote walijua ulikuwa uchekeshaji. Majaribio ya silaha duniani huwa yanaleta malalamiko hata kama jaribio hilo halikulenga nchi yoyote. Tumekuwa tukisikia Taifa fulani likilalamika kuhusu jaribio la kombora lililorushwa na nchi fulani.

Masanja inawezekana hajui madhara ya vita na ndiyo maana alidiriki kuleta utani kwenye eneo hilo. Kwa wanaokumbuka vita ya Kagera hawawezi kutamani wala kuleta utani wa kutaka nchi iingie tena vitani hata kama ni ya kirafiki kama anavyopendekeza.

Wakati wa vita ya Kagera nilikuwa darasa la nne, lakini moto wake tuliuona, shuleni tulichimba mahandaki kwa mwongozo wa wanajeshi na namna ya kuyatumia. Ilikuwa ni hekaheka za vita badala ya kujenga uchumi.

Masanja aelewe vita ina madhara mengi kuanzia vifo, ulemavu wa kudumu, majeruhi, uharibifu wa mali na inarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Pengine umefika wakati kwa waandaaji wa sherehe na matukio ya kitaifa na kimataifa waanzishe utaratibu mpya wa kuwapa mafunzo kujua maudhui yao kabla ya shughuli.

Nasema hivyo nikikumbuka tukio moja la kitaifa la siku nyingi lililofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja kuhusu siku ya kimataifa ya watoto.

Siku hiyo alialikwa mwanamuziki Dk Remmy Ongala na alipotumbuiza kutumbuiza aliimba wimbo wake wa mambo kwa soksi. Ni wimbo wenye maudhui ya kujilinda na maambukizi ya Ukimwi kwa kutumia kondomu.

Hata hivyo, siku hiyo wakati akitumbuiza aliongeza vionjo vyenye maneno yenye matusi ndani yake na kuihusisha Zanzibar na mambo ya hovyo. Wale mawaziri waliokuwa meza kuu walichanganyikiwa huku wakiulizana nani amemleta. Nakumbuka iliandikwa hadi kwenye magazeti.

Nimekumbushia hili kueleza umuhimu wa kuwapa mwongozo wa maadili wanaopewa nafasi ya kutumbuiza au kusherehesha kwenye hafla zinazohusisha viongozi wa kitaifa na kimataifa.

Tanzania ilipokuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Serikali ilipeleka waandishi wa habari jijini New York nchini Marekani ili kuwahabarisha Watanzania.

Lakini, Serikali haikuwabeba tu na kuwapeleka, iliwapa mafunzo ya maadili ya kidiplomasia pale Chuo cha Diplomasia Kurasini ili kujua taratibu na maadili ya namna ya kukaa na viongozi. Lengo kubwa lilikuwa kuliepusha Taifa na aibu inayoweza kufanywa na watu wasiojua maadili.

Kilichofanywa na Masanja itoshe kuwapa funzo waandaaji wa shughuli hizi kwamba wasanii watakaopewa nafasi ya kutumbuiza wapewe angalizo la kimaadili, wafanye mazoezi na maudhui yao yafahamike ili wakienda kinyume wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Nasema haya nikichukua mfano wa Mwalimu Nyerere kwamba hata sanaa na burudani kwenye hafla za kitaifa na kimataifa huwa zinafikisha ujumbe.

Hivyo, kujikwaa siyo kuanguka na yaliyopita si ndwele tugange yajayo kwa kujenga utaratibu utakaoliepusha Taifa na aibu ambazo zinaweza kuepukika kwa kuweka utaratibu mzuri.


Mwandishi anapatikana kwa namba ya simu 0746005607 au baruapepe: [email protected]


Advertisement