Mashahidi 12, vielelezo 11 vyakamilisha ushahidi kesi kina Zumaridi

Muktasari:

  •  Upande wa Jamhuri katika kesi ya jinai inayomkabili Diana Bundala maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi’ na wenzake nane umesema umemaliza ushahidi baada ya shahidi wa 12 kumalizi kutoa ushahidi wake.


Mwanza. Upande wa Jamhuri katika kesi ya jinai inayomkabili Diana Bundala maarufu kama ‘Mfalme Zumaridi’ na wenzake nane umesema umemaliza ushahidi baada ya shahidi wa 12 kumalizi kutoa ushahidi wake.

Leo Ijumaa Septemba 23, 2022 shahidi wa 12 wa upande wa mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Joseph amemaliza kutoa ushahidi wake, katika shtaka hilo la shambulio la kudhuru mwili.

Upande wa Jamhuri umekamilisha ushahidi wake kwa kuwasilisha mashahidi 12 na vielelezo 11 vinavyojumuisha maelezo ya onyo ya washtakiwa hao.

Baada ya shahidi wa 12 kumaliza kutoa ushahidi wake leo Ijumaa Septemba 23, 2022, Mwendesha mashtaka wa serikali, Dorcas Akyoo ameieleza mahakama kuwa wamefunga ushahidi.

"Mheshimiwa hakimu, upande wa Jamhuri hatuna shahidi mwingine wa kuita mahakamani. Tunaomba kufunga ushahidi wetu leo," ameeleza Akyoo

Kufuatia ombi hilo, Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekobora ambaye anasikiliza kesi hiyo amesema mahakama itasoma uamuzi Oktoba 4, 2022 kuona kama washtakiwa wana kesi ya kujibu.

"Nafunga ushahidi wa upande wa Jamhuri, mahakama itatoa maamuzi kama washtakiwa wana kesi ya kujibu tarehe tajwa. Washtakiwa walioko mahabusu wataendelea kukaa huko na walioko nje kwa dhamana wataendelea na dhamana yao," amesema Ndyekobora

Mfalme Zumaridi na wenzake nane wanashtakiwa kwa kosa la kufanya shambulio la kudhuru mwili dhidi ya maofisa wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana kosa wanalodaiwa kulitenda Februari 23, 2022 katika mtaa wa Buguku kata ya Buhongwa jijini Mwanza.