Mashine za kieletroniki zatesa wapigakura Kenya

Muktasari:

  • Baadhi ya wapigakura nchini Kenya, wamepata usumbufu katika vituo vya kupigia kura baada ya Mashine za utambuzi wa kieletroniki (KIEMs) kwa mpigakura kugoma kutambua alama za vidole vyao.

Baadhi ya wapigakura nchini Kenya, wamepata usumbufu katika vituo vya kupigia kura baada ya Mashine za utambuzi wa kieletroniki (KIEMs) kwa mpigakura kugoma kutambua alama za vidole vyao.

Kutokana na tatizo hilo baadhi ya maeneo mtu mmoja alilazimika kutumia dakika tano hadi 10 ndiyo apige kura hali iliyosababisha malalamiko kutoka kwa watu waliokuwa kwenye misururu mirefu ya kupiga kura.

Mgombea Mwenza wa urais kupitia Kenya Kwanza Alliance, Rigathi Gachagua naye alikumbana na adha hiyo ingawa alifanikiwa kupiga kura baada ya kutumia daftari la kawaida lenye majina ya wapiga kura.

Matumizi daftari la kawaida la wapiga kura yaliamriwa na Mahakama siku chache zilizopita baada ya mgombea urais kwa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga kupeleka kesi kutaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) nchini Kenya kuruhusu utaratibu wa kuhakiki majina ya watu kupitia daftari hilo badala ya kutegemea mfumo wa kieletroniki pekee.

Hata hivyo kambi ya Kenya Kwanza, ikiongozwa na chama cha UDA kilipinga hukumu hiyo kikidai inalenga kumfufaisha zaidi Odinga na wagombea wa kambi hiyo.

Hata hivyo leo, mara baada ya kupiga kura Gachagua aliwaambia waandishi wa habari kuwa pamoja na changamoto hizo za kiufundi anaamini uchaguzi utakuwa huru, wenye uwazi na wa haki.

Mgombea mwenza wa urais, Martha Karua naye alikumbana na kadhia kama hiyo ambapo ilimchukua dakika 10 kukamilisha zoezi hilo.