Mashirika binafsi yaanzisha ugawaji chakula shuleni

Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, Maulid Surumbu (katikati) akipokea mfuko wa chumvi wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusaidia chakula shuleni .

Muktasari:

  • Mpango huo wa chakula shuleni unatarajia kuwafuisha wanafunzi 28,000 kutatua tatizo la utoro Wilaya za Handeni na Mkinga.

Mkinga. Wanafunzi 28,000 wa Shule za Msingi katika Wilaya za Handeni na Mkinga mkoani Tanga, wanatarajia kunufaika na mpango wa kusaidia chakula shuleni unaoratibiwa na mashirika yasiyo ya Kiserikali ya World Vision na Save the Children kwa muda wa miezi mitatu.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Kanali Maulid Surumbu leo Agosti 31 wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika Wilaya ya Mkinga mkoani humo jana.

Surumbu amesema mpango huo utasaidia kupunguza utoro, tatizo la kuanguka shuleni na kuuinua kiwango cha taaluma katika wilaya hizo mbili ambazo zimebainika kuwa na uhaba wa chakula.

Kanali Surumbu amesema Wilaya ya Mkinga ina shule 83 za msingi na kati ya hizo shule tatu pekee ndiyo zenye mpango huo wa chakula mashuleni na kwamba shule nyingine 80 hazina mpango huo hivyo mradi huo utakwenda kuleta tija endapo utatekelezwa vizuri.

“Nitoe rai kwa wazazi na walezi mradi huu ni wa miezi mitatu hivyo tujitahidi baada ya kumalizika na sisi tukawajibike kuwapatia chakula watoto wetu ili waweze kukua vizuri na kufanya vizuri katika masomo yao,” amesema Surumbu.

Aidha, amewataka wataalamu wa kilimo kusaidia kuwashauri wananchi ili waweze kulima mazao kulingana na ikolojia ya eneo husika ili kupunguza uhaba wa chakula.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kaskazini Taisisi ya World Vision, Gilbert Kamanga amesema mradi huo umegharimu Sh597 milioni ambapo vyakula vitakavyogawiwa katika Wilaya ya Mkinga ni kilo 70,697 za mahindi, maharage kilo 39,276, chumvi kilo 2,357 na mafuta ya kupikia lita 393 ambavyo vina thamani ya Sh216.43 milioni.

“Kwa upande wa Wilaya ya Handeni chakula kitagawiwa katika shule 24 ambapo jumla ya watoto 14,689 watanufaika na upatikanaji huu wa chakula mashueni ambapo watapata mahindi kilo 129,000, maharage kilo 53,000, chumvi kilo 3,600 na mafuta ya kupikia lita 9, 000,” amesema Kamanga.