Maswali kibao wezi kuvunja, kuiba ofisi ya Takukuru

Muktasari:

Wakati maswali yakiibuka kuhusu wezi kuvunja na kuiba katika ofisi za Takukuru, Jeshi la Polisi mkoani Tanga linamshikilia ofisa mmoja wa taasisi hiyo kuhusiana na tukio hilo.


Dar es Salaam. Wakati maswali yakiibuka kuhusu wezi kuvunja na kuiba katika ofisi za Takukuru, Jeshi la Polisi mkoani Tanga linamshikilia ofisa mmoja wa taasisi hiyo kuhusiana na tukio hilo.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi, baada ya watu wanaodhaniwa ni wezi kufungua mlango wa mbele kwa kutumia ufunguo bandia kisha kuvunja sefu iliyokuwa na silaha hizo.

Habari kutoka chanzo cha kuaminika wilayani Handeni, kulikokuwa na timu ya uchunguzi ya Jeshi la Polisi zinasema ofisa huyo ameongezwa na kufanya wanaoshikiliwa kuwa wawili.

Ofisa huyo (jina lake linahifadhiwa) anashikiliwa kwa kuwa ndiye aliyekuwa akihusika na utunzaji wa funguo za milango ya jengo hilo.

“Anashikiliwa kwa sababu wezi walifungua mlango wa mbele wa jengo la ofisi, wakafika ndani ndio wakavunja mlango wa kamanda, lakini pia walitumia funguo kufungua kasiki (sefu) ambalo lilitunza silaha hizo tatu,” kilisema chanzo chetu.

Silaha nyingine aina ya shotgun iliyokuwa kwenye sefu hiyo, ambayo ilikuwa na risasi zake haikuchukuliwa.

Pia habari hizo zinasema, risasi zilizoibiwa hazikuwa 21 bali ni 48, baada ya uchunguzi kubaini risasi nyingine zilichukuliwa zikiwa kwenye boksi.

“Taarifa ni kwamba bastola moja aina ya Beretta ilikuwa na risasi tano na ile nyingine aina ya Browning ilichukuliwa na risasi 43 zilizokuwa kwenye boksi,” kilisema chanzo chetu hicho kikirekebisha taarifa zilizopatikana juzi.

Jana gazeti hili likinukuu chanzo chetu, liliripoti kuwa bastola zote mbili zilizoibwa ni aina ya Beretta na risasi zake 21.

Habari zilizopatikana zilieleza pia wezi hao waliondoka na simu aina ya Galaxy pamoja na pingu ambazo hata hivyo zilipatikana porini, jirani na ofisi hiyo. Vyote hivyo vilikuwa kwenye kasiki hiyo.

“Watuhumiwa wawili wanaoshikiliwa hadi sasa wanahojiwa, hasa mlinzi anaonekana anazo taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa wahalifu hao,” kiliendelea kueleza chanzo hicho kikisisitiza kuhifadhiwa jina lake.

Tukio hilo limeibua maswali kadhaa, hasa ikizingatiwa, kulipofanyika tukio hilo ni katika ofisi ya umma yenye kutunza nyaraka nyeti.

Ofisa mmoja aliyestaafu akiwa na wadhifa wa mkuu wa upelelezi wilaya (OC-CID), alisema ofisi nyingi za umma zina upungufu katika masuala ya ulinzi kwa kuwa walinzi ni raia au mgambo.

“Taasisi nyeti kama Takukuru, Mahakama au zile zinazotunza sensitive documents (nyaraka nyeti) na vitu kama silaha ni lazima ulinzi wake uwe madhubuti. Lakini katika hili tukio la ofisi ya Takukuru naona kuna kauzembe mahali,” alisema.

“Ili wahalifu wawe na ujasiri wa kuvamia taasisi kama hizo ni lazima wawe na taarifa za ndani kuhusu kile wanachokitaka. Sasa kama wameiba bastola mbili na risasi zake huenda ni kundi linalotaka kupanda daraja.

Mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni binafsi ya ulinzi ya Secularms (T) Limited, Deo Lekule alisema wizi wa aina hiyo unahitaji makachero wanye weledi, hasa ikizingatiwa ofisi hiyo inatunza nyaraka za kesi mbalimbali.

“Ukiona wezi wa aina hiyo wanaenda kwenye ofisi kama hiyo lazima kuna kitu wanakitaka. Huenda kuna watu wana kesi nzitonzito za uhujumu uchumi zinachunguzwa, sasa huwezi kujua kuna baadhi wana mkono au ni wezi wenye lengo lao,” alisema.

John Sebastian, mkazi wa Makorora jijini Tanga alisema kilichofanywa na Takukuru ni uzembe mkubwa wa kuhifadhi silaha hizo katika jengo lao badala ya kuzisalimisha polisi ambako kuna chumba cha kutunzia silaha.

Inaelezwa mgambo aliyekuwa akilinda jengo hilo hakuwa na silaha yoyote zaidi ya rungu.

Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Henry Mwaibambe hakupatikana jana kuzungumzia maendeleo ya upelelelezi huo na hata alipopigiwa simu hakupokea.

Pia si mkuu wa wilaya ya Handeni, Sirily Mchembe wala Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba aliyepatikana kuzungumzia suala hilo.