Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matamanio ya wananchi bajeti ya Serikali 2026/27

Muktasari:

  • Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/27 inatarajiwa kuwa Sh61.93 trilioni. Kati ya fedha hizo, mapato yote yanayotarajiwa kukusanywa, ikijumuisha misaada Sh46.69 trilioni sawa na asilimia 75.4 ya bajeti yote



Dar/mikoani. Hatua za kupunguza gharama za maisha, fursa za ajira, kuimarishwa kilimo na urahisi wa kufanya biashara na uwekezaji ni miongoni mwa mambo wanayoyatarajia wananchi katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Kwa mtazamo wa wananchi, kuwamo kwa mambo hayo katika bajeti na yakatekelezwa ipasavyo, kutarahisisha njia za utafutaji kipato, kufungua fursa za kiuchumi na hatimaye maendeleo yatapatikana.

Wakati wananchi wakipendekeza hayo, wataalamu wa uchumi, wanasema bajeti hiyo ijikite kulinda uchumi dhidi ya athari za mfumuko wa bei na Serikali itumie zaidi vyanzo vyake vya ndani kukusanya mapato badala ya mikopo ya kibiashara.

Mitazamo hiyo ni sehemu ya mapendekezo ya wananchi kuhusu wanayoyataka ndani ya Bajeti ya Serikali, inayotarajiwa kusomwa bungeni jijini Dodoma, Juni 11, mwaka huu na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar.

Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/27 inatarajiwa kuwa Sh61.93 trilioni. Kati ya fedha hizo, mapato yote yanayotarajiwa kukusanywa, ikijumuisha misaada Sh46.69 trilioni sawa na asilimia 75.4 ya bajeti yote.


Nafuu ya maisha

Akizungumza jana Jumatatu Juni 8, 2026 na  Mwananchi kuhusu matarajio yake,  Neema Robert, mfanyabiashara wa chakula katika Stendi Kuu ya Mabasi Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro ni kushuka kwa gharama za maisha, katika kipindi ambacho bei za bidhaa zimepanda.

“Wananchi wanapunguza uwezo wa kununua kwa sababu maisha yamekuwa magumu. Tunatarajia bajeti itakayosaidia kushusha gharama za maisha na kuboresha mazingira ya biashara,” amesema.

Kwa dereva wa bodaboda, Juma Said amesema gharama za mafuta zimeendelea kuathiri kipato cha wananchi, hivyo matarajio yake ni Serikali kuja na mpango wa kupunguza gharama za nishati hiyo.

“Mafuta yakipanda kila kitu kinapanda. Tunahitaji kuona Serikali ikiangalia namna ya kupunguza mzigo wa gharama za nishati na tozo mbalimbali,” amesema.

Rehema Kimaro anaona changamoto ya nishati hasa umeme inakwamisha shughuli za kiuchumi na kuongeza gharama kwa wananchi.

“Tunatamani kuona bajeti inayowekeza zaidi kwenye nishati ya uhakika ili biashara na shughuli nyingine ziende bila usumbufu,” amesema.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ushirika, Avitus Brasio amesema pamoja na ukali wa maisha, changamoto ya ajira bado ni kubwa kwa vijana wengi nchini.

“Vijana wengi wanahangaika kutafuta ajira huku gharama za maisha zikiongezeka. Serikali ikiwekeza zaidi kwenye sekta za uzalishaji itasaidia kuongeza ajira,” amesema.

Stephano Evarist anayeishi Shinyanga, amesema matarajio yake ni kuona ajira kwa vijana zinaongezeka, unatafutwa unafuu wa gharama za maisha na uimarishaji wa sekta ya kilimo na afya.

“Tunatamani kusika katika bajeti hatua za kupunguza na kuweka unafuu wa gharama za maisha ikiwamo bei za bidhaa muhimu, mafuta, umeme na gharama za usafiri na maji ili kuongeza uwezo wa kumudu maisha,” amesema.

Matarajio ya kuzalishwa fursa zaidi za ajira, anayo pia Jesca Masasy akisema kwa sababu wahitimu wameongezeka, bajeti ijikite kuwekeza kwa kuanzisha viwanda na kuzalisha ajira.


Kipaumbele kwenye kilimo

Mkulima kutoka Mwika, Wilbard Mariki amesema sekta ya kilimo inapaswa kupewa kipaumbele zaidi ili kusaidia uzalishaji wa chakula na kupunguza mfumuko wa bei za vyakula.

“Kilimo kikiboreshwa hata bei za vyakula zitashuka. Serikali iangalie pembejeo na masoko ya mazao ili mkulima naye anufaike,” amesema.

Gerald Mbogo anayefanya shughuli za kilimo mkoani Shinyanga, amesema matarajio yake ni kuona bajeti ikiongeza upatikanaji wa ruzuku mbalimbali kwenye sekta hiyo.

“Wakulima tunatarajia bajeti hiyo ioneshe upatikanaji mzuri wa ruzuku za pembejeo, mbegu bora, mbolea, masoko ya uhakika na miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji na kipato,” amesema.


Mazingira ya biashara yarahisishwe

Kwa upande wa sekta binafsi, Mkurugenzi Mtendaji wa Sethi Ura Company Limited, Stanley Urassa anatarajia kuona Serikali ikiweka rafiki ya biashara na uwekezaji hasa kwa sekta binafsi.

Kwa wafanyabiashara wadogo, amesema wanatarajia marekebisho ya kodi yatakayosaidia kukuza ushindani na kuwawezesha kujimudu katika soko.

“Bajeti inaweza kuwa chombo muhimu cha kuchochea uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi wa kidijitali iwapo itaweka mazingira bora kwa sekta binafsi na wabunifu,” amesema.


Mtazamo wa kiuchumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari amesema bajeti ya Serikali inapaswa kuelekeza nguvu katika kulinda uchumi dhidi ya athari za mfumuko wa bei unaoweza kuathiri maisha ya wananchi na shughuli za uzalishaji.

Dk Mmari amesema moja ya hatua muhimu ni kuangalia uwezekano wa kupunguza baadhi ya tozo na kodi katika mafuta ili kupunguza athari za kupanda kwa bei za nishati katika uchumi kwa jumla.

“Athari za mfumuko wa bei, tayari zimeonekana moja kwa moja katika uchumi, hivyo ni muhimu bajeti ikaelekeza mikakati ya kuzuia athari hizo zisiendelee kuathiri wananchi na sekta za uzalishaji,” amesema.

Dk Mmari amesema Serikali pia inapaswa kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ili kupunguza mahitaji ya kukopa, hatua  itakayosaidia kuimarisha uthabiti wa uchumi na kulinda sekta binafsi.

“Unapopunguza matumizi yasiyo ya lazima, unapunguza ulazima wa Serikali kukopa. Hii inasaidia kuzuia ongezeko la viwango vya riba na kuwezesha benki kuendelea kutoa mikopo kwa gharama nafuu kwa sekta binafsi,” amesema.

Amesema kupungua kwa mzigo wa madeni kunatoa nafasi kwa Serikali kuelekeza rasilimali nyingi zaidi kwenye maeneo ya kipaumbele kama uwekezaji katika miundombinu, utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi.

Ameshauri Serikali kuendelea kupanua wigo wa walipakodi badala ya kuongeza mzigo kwa kundi dogo la walipakodi waliopo sasa.

“Kuwa na walipakodi wengi zaidi kutasaidia kuongeza mapato ya Serikali huku kukiboresha mazingira ya biashara kwa kuhakikisha mzigo wa kodi unagawanywa kwa usawa zaidi,” amesema.

Mchambuzi wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka amesema mabadiliko ya kiuchumi na kifedha yaliyoshuhudiwa katika mwaka uliopita yanapaswa kuwa somo kwa Tanzania katika kupanga vyanzo vya mapato na matumizi.

Amesema kwa muda mrefu nchi inategemea mikopo ya kibiashara na mikopo nafuu kutoka nje, lakini sasa kuna umuhimu wa kuweka mikakati madhubuti ya kuimarisha vyanzo vya ndani na kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje.

“Huenda unayemtegemea hategemeki. Ukiwa na uwezo wa ndani wa kuzalisha na kukusanya rasilimali zako unakuwa na uhakika zaidi wa kutekeleza mipango yako ya maendeleo,” amesema.

Dk Mwinuka amesema wakati utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ukianza Julai mosi mwaka huu, Serikali inapaswa kuweka wazi mikakati itakayohakikisha uchumi jumuishi unakuwa na wananchi wengi zaidi wanashiriki na kunufaika na matunda ya ukuaji huo.

“Ikiwa sekta binafsi inatarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya pato la Taifa katika utekelezaji wa Dira 2050 ni muhimu kuweka mazingira bora yatakayoiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Tunahitaji mifumo rahisi ya kodi, usajili na utoaji wa huduma mbalimbali za kiserikali,” amesema.

Amesema changamoto kubwa si lazima iwe kiwango cha kodi, bali urahisi wa kufanya biashara hivyo uwepo wa mifumo ya pamoja ya usajili wa kampuni, biashara, tozo na huduma nyingine za Serikali unaweza kupunguza gharama za muda na kuongeza ushindani wa biashara.

“Wawekezaji na wafanyabiashara wanahitaji urahisi wa kufanya mambo kwani kadri taratibu zinavyorahisishwa, ndivyo mazingira ya biashara yanavyoboreshwa na uchumi unavyokua kwa kasi zaidi,” amesema.

Ameishauri Serikali kuongeza ubunifu katika utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) ili kupata vyanzo mbadala vya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara.

“Miradi ya ubia inaweza kuwa sehemu ya suluhisho katika upatikanaji wa fedha za maendeleo. Kadri tunavyopunguza utegemezi wa mikopo ya gharama kubwa, ndivyo tunavyoongeza uwezo wa uchumi kustahimili misukosuko na kutekeleza malengo ya muda mrefu ya maendeleo,” amesema.


Imeandikwa na Juma Issihaka, Aurea Simtowe (Dar), Yese Tunuka (Moshi) na Hellen Mdinda (Shinyanga).

­­­­