Matibabu ya malaria sasa kutolewa bure Tanzania

Dar es Salaam. Serikali imeondoa gharama zote zinazohusu ugonjwa wa Malaria kuanzia huduma za upimaji kwa kutumia kipimo cha MRDT, sindano za Malaria kali, dawa za ALU pamoja na SP zinazotolewa kwa wajawazito.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 25, 2023 wakati wa maadhimisho ya siku ya Malaria duniani na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika maadhimisho ya siku ya Malaria duniani.
Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kutokomeza Malaria pamoja na kupambana na usugu wa dawa.
"Rais ameleta unafuu kwa kutoa huduma za upimaji mbalimbali bure kikiwemo kipimo cha MRDT sasa kitatolewa bure Sindano kali bure, dawa za ALU bure pamoja na SP kwa wajawazito nazo zitaendelea kutolewa bure.
"Nisisitize. Kila mwenye dalili za Malaria nitoe wito lazima apimwe kwanza ndipo apewe dawa na kuhakikisha anakamilisha dozi, lengo la Serikali ni kukabiliana na usugu wa dawa, pia endeleeni kutumia vyandarua," amesema Majaliwa.
Matibabu hayo ambayo yameanza rasmi kutolewa bure nchini, yamekuja siku chache baada ya ripoti ya Wizara ya Afya kuonyesha watu wenye kipato duni ndiyo huathirika zaidi na ugonjwa wa Malaria kwa asilimia 14.5 huku tabaka la chini wakiathirika kwa asilimia 10.9.