Matola: Morrison, Dilunga hawakuwa fiti kwa Yanga

Matola: Morrison, Dilunga hawakuwa fiti kwa Yanga

Muktasari:

  • Wakati mashabiki wengi wa Simba wakionekana kutaka kumwona winga wao Bernard Morrison akicheza kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kocha Seleman Matola amesema hakuwa kwenye mipango yake huku akifafanua kuhusu kiwango cha Hassan Dilunga.
  • Matola katika mashindano hayo ambayo waliingia hatua ya fainali na kupoteza kwa Yanga kwa matuta, alimpanga Morrison kwenye wachezaji wa akiba kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Namungo ambao, walishinda bao 2-1 na fainali ya ushindi kwa Yanga penalti 4-3 hakumtumia licha ya kuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.

Unguja. Wakati mashabiki wengi wa Simba wakionekana kutaka kumwona winga wao Bernard Morrison akicheza kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kocha Seleman Matola amesema hakuwa kwenye mipango yake huku akifafanua kuhusu kiwango cha Hassan Dilunga.

Matola katika mashindano hayo ambayo waliingia hatua ya fainali na kupoteza kwa Yanga kwa matuta, alimpanga Morrison kwenye wachezaji wa akiba kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Namungo ambao, walishinda bao 2-1 na fainali ya ushindi kwa Yanga penalti 4-3 hakumtumia licha ya kuwa kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.

Hata hivyo, Matola aliliambia Mwanannchi kuwa sababu kubwa za kutomtumia Morrison ni kutofanya mazoezi ya pamoja na wenzake kwa kipindi kirefu hivyo, isingekuwa rahisi kucheza kwani timu ilikuwa na malengo ya ubingwà na sio kucheza kwa kujaribu.

“Sikuona sababu ya kumtumia Morrison hata kama alikuwa kwenye wachezaji wa akiba, hajafanya mazoezi kama mwezi mzima, unampangaje mchezaji kama huyo na analeta matokeo gani. Morrison ametoka kuumwa hivi karibuni hivyo, ni lazima awe fiti ndipo atumike.

“Sina budi kuwapongeza Yanga kutwaa ubingwa japo tumefungwa kwa penati, wachezaji wangu wamepambana kadri walivyoweza ndiyo maana dakika 90 hatukufungwa. Nimewatumia Dilunga na Miraji Athuman huku wakiwa wanasumbuliwa na misuli na waliniambia mapema, lakini sikuwa na namna,” alisema Matola, ambaye enzi zake amecheza kwa mafanikio akiwa Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars.

Nyota hao wawili walishindwa kumaliza mchezo ambapo, Matola alilazimika kuwatoa nafasi zao zilichukuliwa na Chris Mugalu pamoja na Ibrahim Ajibu ambao hawakubadili matokeo ya mchezo ambao ulimalizika kwa sare ya bila kufungana.

Hata hivyo, Morrison kwa upande wake baada ya mchezo huo alionekana kwenda eneo ambalo wachezaji wa Yanga na benchi lao ufundi walikuwepo na kuzungumza nao.

“Nawapongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa, kuondoka Yanga isiwe uadui wametwaa ubingwa huu na wanastahili pongezi ingawa sisi tunapambana zaidi na mashindano makubwa haya ilikuwa kama kujiburudisha tu,” alisema Morrison ambaye usajili wake kutoka Yanga kwenda Simba umegubikwa na sintofahamu zilizowafikisha ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kutafuta uhalali kuhusu mikataba.