Matukio ya kijinai yaongoza uchunguzi DNA

Mkemia Mkuu wa Serikali Dk Fidelice Mafumiko

Muktasari:

  • Mamlaka ya Maabara ya Mkemia wa Serikali (GCLA) imebainisha kuwa uchunguzi wa sampuli za vinasaba (DNA), unaofanywa na maabara hiyo, mwingi ni ule unaohusu matukio ya kesi za kijinai.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia wa Serikali (GCLA) imebaini kuwa uchunguzi mwingi wa wa sampuli za vinasaba (DNA) katika maabara hiyo, ni ule unaotokana na kesi za kijinai, tofauti na ilivyozoeleka.

Matarajio ya wengi ni kudhani kuwa sampuli zinazoongoza kwa wingi katika maabara hiyo, ni zile zinazohusiana na wazazi kutaka kujua uhalali wao kwa watoto walionao wanaodaiwa ni wao.

Akizungumza Novemba 30,2023 jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa wahariri na waandishi wa habari, ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi wa Huduma ya Sayansi Jinai kutoka GCLA, David Elias amesema sampuli zinazopelekwa ni nyingi kutokana na matukio ya jinai kuwa  mengi.

“Sampuli za makosa ya jinai hazina mipaka, kwa hiyo jinai ndiyo inayoongoza kupokea sampuli nyingi kwenye maabara ya sayansi ya jinai,” amesema.

Baadhi hizo za jinai kwa mujibu wa GCLA, za matukio ya ubakaji, ulawiti, mauaji, ujangili wa wanyamapori na dawa za kulevya.

Akitoa takwimu za sampuli zilizofanyiwa uchunguzi, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko amesema kuna ongezeko la sampuli zinazofanyiwa uchunguzi.

Mfano, Dk Mafumiko amesema: “...kwa mwaka 2021/2022 sampuli 155,817 zilichunguzwa ambazo sawa na asilimia 139.94 ya lengo la kuchunguza sampuli 111, 349.

“Mwaka 2022/2023, sampuli 212,306 sawa na asilimia 133.9 ya lengo la kuchunguza sampuli 158,600 zilifanyiwa uchunguzi wa kimabaara,” ameongeza kusema.

Kwa matukio ya sumu, Dk Mafumiko amesema katika kipindi cha miaka mitano 2018/2023, kituo cha kudhibiti matukio hayo, kimewezeshwa kupata taarifa na kutoa elimu ya kuzuia na kujikinga na matukio hayo.

“Tumepunguza matukio ya sumu mbalimbali kutoka 143,260 mwaka 2019 hadi visa 95,663 kwa mwaka 2022,” amesema na kuongeza;

“...DNA ni zaidi ya kubainisha uhalali wa watoto kwa wazazi, pia hutumika kutambua binadamu na wanyama wakati wa majanga. Lakini pia tunaweza kutumia sampli hizo kutambua jinsia inayotawala, hasa kwa watu wanaodaiwa kuwa jinsi tata.”

Amesema pia kuwa chunguzi za maabara hiyo kupitia DNA, zinaweza pia kubaini kuwapo au kutokuwapo kwa mahusiano ya kindugu na utambuzi wa viungo vya binadamu.

Kwa upande mwingine, Dk Mafumiko amesema upimaji wa sampuli za vinasaba kwa watu wanaohitaji ni Sh100,000 kwa mtu mmoja, lakini upo utaratibu maalumu ambao mtu atapaswa kufuata ili afanyiwe uchunguzi huo.

Dk Mafumiko amesema kwa mtu anayetaka kufahamu kama mtoto ni wake atatuma maombi kupitia kwa wakili wake anayetambulika au ofisa ustawi wa jamii akiambatanisha sababu za kutaka uchunguzi huo.

Njia nyingine kwa matukio ya jinai maombi ya uchunguzi wa vinasaba huwasilishwa na Jeshi la Polisi lakini kwa watu wenye jinsia tata maombi huwasilishwa na daktari.

“Kwenye jinsia tata tuna vifaa maalumu ambavyo tunaweza kugundua kama ni jinsi gani inafanya kazi zaidi ya nyingine na tukatoa majibu, vivyo hivyo kwenye upimaji wa sampuli ya figo uchunguzi wa vinasaba unaombwa na daktari,” amesema.

Akizungumzia muda wa uchunguzi wa sampuli, Dk Mafumiko amesema kwenye sampuli zinazohisiwa kuwa na sumu, wataalamu wa GCLA hutumia siku 11 za kazi kutoa majibu.

Pia kwa wastani wa siku sita na nusu ni muda unaotosha kukamilisha uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za dawa za kulevya, mioto, na milipuko. 

“Wastani wa siku 27 za kazi kukamilisha uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli za vinasaba vya binadamu (kutegemea aina ya sampuli),” amesema.


Kuhusu Kanzidata

Mkemia mwanadimizi Leticia Waitara amesema mamlaka hiyo ipo kwenye hatua ya ujenzi wa kanzidata ya vinasaba kwa Watanzania wote ambayo itarahisisha utoaji wa huduma ya vinasaba kwenye matukio ya ajali, uhalifu au masuala ya kijamii.

Ametaja sababu za kuwa na kanzidata hiyo ni uchunguzi wa sampuli kufanyika haraka,  kwa kufanya ulinganifu na sampuli iliyopatikana na ile iliyopo kwenye kanzidata.


Teknolojia kwenye utendaji

Akizungumzia matumizi ya Tehama, Dk Mafumiko amesema upo mpango wa mfumo wa usimamizi wa taarifa za maabara (LIMS) -kuunganisha mfumo wa haki jinai,

Lengo la kufanya hivyo ni kubadilishana taarifa za matokeo ya uchunguzi wa maabara na mifumo mingine ya haki jinai.

”Mfumo wa kutoa ushahidi kwa ki-electroniki– kupunguza gharama za kusafirisha  wataalamu kwenda kutoa ushahidi mahakamani kwenye mnyororo wa haki jinai,” amesema.

Akizungumzia wadau wanaojishughulisha na biashara ya kemikali, Dk Mafumiko amesema wameongezeka kutoka 2,125 mwaka 2020/2021 hadi 3,371 mwaka 2022/2023.        


Ufahamu kuhusu vinasaba

Vinasaba ni chembechembe ndogo ambazo hubeba taarifa zote za kibailojia ambazo hutumika katika ukuaji na ufanyaji kazi wa kiumbe hai.

Vinasaba ndivyo hubeba taarifa zote za kiumbe hai mfano, rangi yake ya ngozi, kimo, nywele na magonjwa ya kurithi aliyonayo.