Matumizi ya Teknlojia 2020 na kuongezeka kwa mapato ya Serikali

Mwaka 2020 ulikuwa ni mwaka wa mwisho wa muhula wa kwanza wa Serikali ya Rais John Magufuli, ambaye hata hivyo alichagulia tena na wananchi kuliongoza Taifa kwa miaka mingine mitano hadi 2025 huku akiahidi kuendeleza pale alipoishia katika ingwe yake ya kwanza.
2020 ni mwaka ambao wananchi walipata fursa ya kuchagua Serikali ya kuwaongoza hata hivyo ulikumbwa na changamoto lukuki ikiwa ni pamoja na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ambao ulileta athari nyingi za kijamii na kiuchumi hata hivyo makusanyo ya kodi ya Serikali yaliendelea vizuri.
Katika hotuba ya bajeti kuu ya Serikali 2020/2021, iliyowasilishwa na kupitisha Bungeni Juni, 2020 Waziri wa Fedha Dk Philipo Mpango alisema katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, mapato ya ndani yameongezeka kufikia shilingi trilioni 18.5 mwaka 2018/19 kutoka shilingi trilioni 11.0 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 69.1.
Mpango alisema katika mwaka wa fedha 2019/2020 Mapato ya kodi na maduhuli kutoka katika sekta zilizoathirika zaidi na COVID-19 yalipungua hususan mapato ya sekta ya utalii, tozo/ada za Visa, kodi zinazolipwa na hoteli, ada za viingilio kwenye viwanja vya michezo na maeneo ya sanaa na burudani.
Hata hivyo alisema licha ya nafuu za kikodi zilizotolewa baada ya mlipuko wa Covid-19 ili kutengeneza uchumi Mapato ya kodi yanatarajiwa kufikia asilimia 12.9 ya Pato la Taifa mwaka 2020/21 kutoka matarajio ya asilimia 12.1 mwaka 2019/20.
“Wastani wa mapato ya kodi kwa mwezi umeongezeka kutoka Sh825 bilioni mwaka 2014/15 hadi wastani wa Sh1.3 trilioni mwaka 2018/19 na kuongezeka zaidi hadi wastani wa Sh1.5 trilioni katika kipindi cha Julai 2019 hadi Aprili 2020,” alisema Mpango
Alisema ongezeko hilo la mapato lilitokana na kudhibiti upotevu wa mapato kwa kuimarisha usimamizi wa Sheria za kodi na matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ikiwa ni pamoja na EFD na mfumo wa miaka ya hivi karibuni wa sstempu za kielektroniki (ETS).
Mfumo ETS ambao ulianzishwa ili kuongeza uwaza na kudhibiti mianya ya upotevu wa kodi unasimamiwa na Kampuni ya Uswis iitwayo Societe Indusrielle et Commerciale de Produits Alimentaires (SICPA) ulianza kutekelezwa Januari 15, 2019 kwa vinywaji aina ya bia, Mvinyo na pombe kali ambapo kampuni 19 zilifungiwa mfumo huo.
Awamu ya pili ilitangazwa Agosti mosi ilikuwa kwa vinywaji aina ya vinywaji baridi kama soda na vinginevyo visivyo na kilevi na Novemba mwaka huu mfumo huo umeanza kutumika kwa bidhaa za maji, juisi na bidhaa za filamu na muziki. Kuchelewa kwa awamu hiyo kunatajwa kuwa kulilenga kutoa nafasi zaidi ya wadau kuelewa mfumo huo.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa katika kipindi cha Februari hadi Oktoba 2019 baada ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ETS mapato katia ushuru wa bidhaa zilizowekewa mfumo huo yaliongezeka kwa asilimia 33.7 hadi kufikia Sh58.2 bilioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018.
Vilevile ushuru bidhaa za vinywaji bardi uliongezeka kwa asilimia 8.9 hadi Sh10 bilioni kwa mwezi Septemba hadi Oktoba, 2019 ikilinganishwa na kipindi kama hicho 2018.
Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo aliliambia gazeti hili kuwa takwimu zinaonyesha kuna ongezeko la ukusanyaji wa mapato kutokana na awamu ya kwanza ya mfumo huo.
“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa hesabu halisi za uzalishaji na malipo ya ushuru wa forodha bila kuingiliwa na mtu, tuliwiwa kufanya kazi naSICPA  baada ya kuona mafanikio ya mfumo huu katika nchi za Kenya, Morocco, Uganda, Malaysia, Brazil, Turkey na Albana,” alisema.
Alisema sasa TRA inakuwa na uwezo wa kujua kiwango halisi kinachozalishwa na punde Mamlaka hiyo itazindua programu ya simu ambayo itamuwezesha mteja kujua kama bidhaa hiyo ina stempu ya TRA.
Zanzibar
Baada ya mafanikio hayo Agosti 5, 2020 Serikali ya Zanzibar ilitagaza kuanza kutumia mfumo wa risti za kielektroniki katika uuzaji jambo ambalo linatajwa kuwa litaongeza makusanyo ya kodi kwa Zaidi ya asilimia 10.
Tofauti na mashine zinazotumika Tanzania bara ambazo huitwa (EFD) upande wa Zanzibar watakuwa wakitumia VFD (Virtual Fiscal Divice) ambayo ni ya kisasa zaidi ya na inatuma taarifa za mauzo moja kwa moja makao makuu ya Bodi ya mapato ya Zanzibar (ZRB).
Kamishina wa ZRB Joseph Meza aliliambia gazeti hili kuwa VFD inatoa risti ya kielektroniki na inatuma taarifa wakati huo huo kama mtandao uko vizuri na hata kama hakuna mtandao inatunza taarifa hizo na pindi inapopata mtandao jambo la kwanza ni kuzituma.
“Tunatarajia utaratibu huu utaongeza ukusanyaji wa mapato kwa kiasi kikubwa kwa kuanzia tunaweza kuongeza mapato ya Sh5 bilioni kiasi hicho cha fedha kwa Zanzibari ni kingi sana na wastani wetu wa mapato huwa ni zaidi ya Sh40 bilioni,” alisema  Meza.
Alisema kabla kuanzishwa kwa mfumo huo Zanzibar ilikuwa ikitoa risiti za kuandikwa kwa mkono ambazo zinatoa mwanya kwa watu kufanya utanganyifu wa kiasi cha kodi ambacho kinalipwa kwa kwa bodi ya ukusanyaji wa mapato.
“Tunajaribu mfumo huu ambao ni mpya kwetu tutaangalia ufanisi wake na tuna wataalamu wa kufanya maboresho kulingana na udhaifu tutakaokuwa tumeuona. Tunafanya kazi na binadamu ambao kila siku wanatafuta mbinu nyingi za kufanya udanganyifu hivyo lazima kuendelea kujenga,” alisema Meza.
Aidha aliongeza kuwa mbali na VFD ZRB inafikiria kuwa na mfumo wa ETS kwa hapo baadaye lakini itazingatia na mahitaji ya wakati kwani kwa sasa wanataka kuimarisha kwanza mfumo wa VFD lakini wataalamu wanendelea na maboresho na ujenzi wa mifumo mingine.