Mauaji ya Osama, maziko yake baharini (5)

Wednesday September 15 2021
Osama pc

Katika toleo lililopita tulimsoma aliyekuwa Rais wa Marekani, George W. Bush akisema “tutamng’oa Osama bin Laden kwenye pango lake” baada ya kusikia amekimbilia kwenye mapango na mahandaki ya Tora Bora.

Mwezi uliofuata, Desemba 2001, Rais Bush aliahidi kuwa Osama angepatikana “akiwa hai au amekufa.” Wiki mbili baadaye akaitangazia dunia kuwa “Osama hatatutoroka”, lakini hadi anaondoka madarakani Januari 20, 2009, Bush hakumkamata.

Habari kubwa duniani ilikuwa ni kwamba Osama na makamanda wake walifanikiwa kutoroka na walifika salama katika ardhi ya Pashtun nchini Pakistan. Mwingine aliyefanikiwa kutoroka kutoka Afghanistan alikuwa kiongozi wa Taliban, Mullah Omar, wanamgambo wake na mtu namba mbili wa al-Qaeda, Ayman al-Zawahiri.

Rais aliyechaguliwa Marekani baada ya George W. Bush, Barack Obama aliendelea pale alipoachia Bush kutafuta Osama. Mei 1, 2011, Timu ya SEAL (kikosi cha Jeshi la Marekani cha Majini, Angani na Ardhini) iliyoitwa ‘Team Six’ ilidaiwa kuwa ilivamia makazi ya bin Laden katika mji wa Abbottabad, Pakistan.

Baada ya kutambua kwamba mlengwa alikuwa ndiye Osama bin Laden, kiongozi wa al-Qaed, makamanda wa SEAL walitangaza wamemuua, kisha wakachukua mwili wake na kuuzika baharini ili kuhakikisha hakutakuwa na hija kwenye kaburi lake.

Marekani ilikuwa imetoa ahadi ya dola 25 milioni kwa yeyote atakayewezesha kupatikana kwake.

Advertisement

Siku nne baadaye, Mei 6, kwa mujibu wa gazeti ‘Daily Mail la Uingereza, al-Qaeda walikiri kuwa ni kweli Osama ameuawa na kulingana na gazeti hilo, waliahidi kulipiza kisasi. Gazeti hilo liliwanukuu ‘al- Qaeda’ hao wakiapa hivi: “Furaha yenu itageuka kuwa huzuni.”

Siku hiyo, Mei 2, Rais Obama alitangaza kifo cha Osama. Wakati akitoa tangazo hilo alisema “Leo naweza kuripoti kwa watu wa Amerika na dunia kwa ujumla kuwa Marekani imeendesha operesheni iliyomuua Osama bin Laden, kiongozi wa al-Qaeda, na gaidi aliyehusika na mauaji ya maelfu ya wanaume, wanawake na watoto wasio na hatia.”

Walimwengu walipoanza kutilia shaka mauaji ya Osama, hususan kutokana na kile kilichodaiwa kuwa mara baada ya kuuawa mwili wa Osama bin Laden ulitumbukizwa “haraka sana” baharini, Rais Obama alitamka: “Kamwe hamtamwona Osama akitembea tena duniani humu.”

Ikulu ya Marekani ilidai kuwa Marekani iliamua kumzika Osama baharini kwa mujibu wa taratibu za maziko ya Kiislamu, lakini wengi walipinga jambo hilo, wakisema maiti ya Mwislamu inaweza tu kuzikwa baharini ikiwa anayezikwa alifia baharini na mwili wake umeanza kuoza.

Mufti al-Qubaisi aliongeza kuwa inaruhusiwa kumzika Mwislamu baharini, lakini ruhusa hiyo ni kwa matukio yasiyo ya kawaida. “Lakini hili la Osama si tukio mojawapo la kumfanya azikwe baharini.”

Mohammed Qudah ambaye ni profesa wa sheria za Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Jordan alisema kumzika Osama bin Laden baharini hakukatazwi iwapo hakuna mtu aliyekuwa tayari kuupokea mwili wake ili auzike Kiislamu.

“Bahari na ardhi vyote ni mali ya Mungu mwenye uwezo wa kuwalinda na kuwaamsha wafu siku ya hukumu,” alisema.

Viongozi wa kidini nchini Iraq waliohojiwa na AP walisema kitendo cha Marekani kumzika Osama baharini kilikuwa cha kuwafaidisha tu samaki.

Baada ya Osama, Ayman al-Zawahri alikuwa kiongozi mpya wa al-Qaeda, na kufikia mwaka 2014 aliaminika kuwa alikuwa amejificha nchini Pakistan.

Serikali ya Marekani ilitoa zawadi ya dola milioni 25 kwa yeyote ambaye angetoa habari zitakazowezesha kupatikana kwa al-Zawahiri, na milioni 10 kwa taarifa zitakazowezesha kupatikana kwa Mullah Omar, ambaye naye pia aliaminika kuwa alikuwa amejificha nchini Pakistan.

Vita ya Marekani dhidi ya Afghanistan ilikuwa na matokeo mengine yanayohusiana na vita dhidi ya ugaidi. Nchini Afghanistan wanajeshi wa Marekani waliwateka wanajeshi wanaodhaniwa ni al-Qaeda na wa Taliban, na mawakala wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) katika sehemu nyingine za ulimwengu waliwakusanya watu wanaoshukiwa kuwa magaidi na kuwaweka katika jela za siri sehemu mbalimbali duniani.

Jumanne ya Novemba 13, 2001, Rais Bush alisaini Agizo la Serikali la kutangaza “dharura isiyo ya kawaida,” na hivyo kuruhusu jeshi kumzuia na kumshtaki mtu yeyote ambaye Serikali ilimwona “mpiganaji adui,” na walipewa mamlaka ya kufanya hivyo hata kwenye mahakama za kijeshi.

Kwa njia hiyo, mtuhumiwa hangeweza kupata haki zilezile ambazo angeweza kuzipata kwenye mahakama za kawaida. Wafungwa wangeweza kukabiliwa na adhabu ya kifo na ushahidi wowote wa kusikia na taarifa zozote walizotoa, hata kama ni kwa kuteswa, zingekubalika katika mahakama hizo za kijeshi.

Bush alidai kwamba mahakama za kijeshi zingewatendea wafungwa kwa haki, lakini madai hayo yalikosa nguvu. Bunge la Marekani halikutangaza vita, kwa hiyo Serikali ya Bush haikuwa na mamlaka ya “Rais wa vita” ambaye angeweza kuamua mambo tofauti.

Kufikia Januari 2002 wafungwa wa kwanza walifikishwa gereza la Camp X-Ray, huko Guantanamo Bay, Cuba.

Baada ya kumaliza operesheni ya kuwaondoa Taliban kwenye utawala nchini Afghanistan, uliingia kwenye hatua ya tatu na ya mwisho kwa kuivamia Iraq.

Lakini kwanini Iraq? Tukutane toleo lijalo.

Advertisement