Mawakili wa utetezi wasiomsaidia mshtakiwa-5

Muktasari:

Katika toleo lililopita tuliendelea kusoma kisa cha kweli kinachomhusu mtoto Mmarekani mweusi, George Stinney (14) aliyenyongwa nchini, Juni 16, 1944, baada ya kutuhumiwa kuwaua wasichana wawili wa kizungu.

Katika toleo lililopita tuliendelea kusoma kisa cha kweli kinachomhusu mtoto Mmarekani mweusi, George Stinney (14) aliyenyongwa nchini, Juni 16, 1944, baada ya kutuhumiwa kuwaua wasichana wawili wa kizungu.

Lakini baada ya kuuawa ilikuja kujulikana kuwa muuaji hakuwa yeye na kwamba ushahidi ulitumika kumhukumu ulikuwa tu wa mazingira. Nini kilitokea? Fuatana nasi kwenye mfululizo wa makala hizi.

Asubuhi ya Aprili 21, Mahakama Kuu ya Kaunti ya Clarendon ilikaa kikao maalumu kilichoongozwa na Jaji Philip Henry Stoll (70) ambaye alitajwa kuwa kuwa na uzoefu mkubwa na kesi zinazohusisha adhabu ya kifo.

Katika hali ambayo si ya kawaida, kesi ya George Stinney ilisikilizwa alasiri moja tu na kumalizika na hukumu kutolewa siku hiyohiyo.

George alipelekwa mahakamani na kuketishwa kizimbani. Kwa mwezi mmoja tangu akamatwe, mtoto huyo alikuwa peke yake na hakuwa na mawasiliano wazazi wala watu wengine wa familia yake. Mtu pekee aliyewasiliana naye ni mahabusu mwenzake, ambaye kama yeye, pia alikuwa Mmarekani mweusi.

Umati mkubwa wa watu waliokuwa na shauku ya kusikiliza kesi hiyo ulihudhuria mahakamani siku hiyo. Kwa mujibu wa simulizi za kihistoria, waliohudhuria walikuwa i zaidi ya watu 1,500.

“Walijaza kila kiti, wengine wakasimama kwenye milango, na wengine kwenye ghorofa na hata wengine kwenye viwanja vya mahakama,” kinaeleza kitabu kiitwacho ‘Criminology: Connecting Theory, Research and Practice’.

Kwa sababu ya fununu za vurugu zilizokuwa zimeenea siku chache kabla ya kesi, ulinzi uliimarishwa kuliko wakati mwingine wowote kabla ya hapo.

Mwendesha mashtaka aliingiza taarifa mbili zilizosomwa mahakamani. Ya kwanza ilisema wasichana wawili waliouawa—Betty June Binnicker (11) na Mary Emma Thames (7)—walikuwa wamemwendea George Stinney na kumuuliza ni wapi wangeweza kupata maua. Aliwaambia wakatafute mbali zaidi msituni. Lakini baadaye George alimshambulia Mary akaanguka kwenye shimo, Betty alipokuja kumsaidia, ndipo naye akashambuliwa.”

Taarifa ya pili ilikuwa ni madai ya George kukiri kwa Konstebo Sidney Pratt na Naibu Mkuu wa Polisi Huger Newman, kwamba aliwafuata wasichana hao msituni kwa nia ya kuwabaka. Mary alipiga kelele alipoona George Stinney anataka kumbaka Betty, ndipo George akampiga “hadi kupoteza fahamu.”

Kisha akamkimbiza yule Betty lakini akatumbukia kwenye shimo. Inasema George aliuondoa mwili wa Betty kutoka humo shimoni ili kumbaka, lakini alishindwa katika jaribio hili. Muda mfupi baadaye, alijaribu tena kumbaka, akashindwa kwa mara nyingine.

Baada ya kuingiza ungamo hili kwenye rekodi, upande wa mashtaka ulikuwa tayari kuwasilisha kesi yake. Wakili Franklin McLeod aliwaita mashahidi wake kuunda mlolongo wa kimantiki wa matukio: kuanzia kwanini wasichana hao wawili waliondoka nyumbani kwao, hadi kugunduliwa kwa miili yao asubuhi iliyofuata, kisha kukamatwa kwa Stinney na baadaye kuungama kwake, na mwishowe uchunguzi ambao mwili wa Betty ulifanyiwa.

Chini ya sheria ya Marekani, upande wa mashtaka katika kesi ya jinai lazima uthibitishe hatia bila shaka yoyote; utetezi, kwa upande mwingine, hauna mzigo wa kuthibitisha kutokuwa na hatia.

Utetezi unahitajika tu kupanda mbegu za shaka katika akili za majaji. Ushahidi uliotolewa uliwapa upande wa utetezi fursa ya kuweka mbegu hizo za shaka. Je, miili kuwa shimoni na baiskeli kukutwa imeharibiwa kunahusishwaje na George Stinney? Je, kwa umri wake mdogo kiasi kile, na asiye na nguvu kama mtu mzima, alikuwa na nguvu za kuny’ofoa gurudumu la mbele kutoka kwenye fremu ya baiskeli?

Nafasi ya kuibua shaka hii ilipita bila neno lolote kutoka kwa upande wa utetezi. Waliodaiwa kuwa mawakili wa Stinney hawakujitokeza kuuliza swali lolote wakati wote wa kesi wala katika majumuisho yao kabla ya kesi kufikia uamuzi.

Jaji Stoll alizuia maelezo mengine kutolewa akidai kuwa ushuhuda “huenda ungekuwa mbaya zaidi.” Alitaja maelezo yaliyokaribia kutolewa kuwa “ya kusikitisha.”

Ushahidi wa Pratt na Newman ulifuata, ambao ni madai kuwa mshtakiwa aliungama mbele yao kuwa ni kweli aliwaua wasichana hao, na kwamba walipompeleka eneo la tukio mshtakiwa aliwaonyesha kipande cha chuma ambacho alisema alikitumia kuwaua wasichana hao. Pia alikiri kwamba alimbaka Betty.

“Nilimuuliza maswali ya kutosha kujua kwamba yeye ndiye muuaji,” Pratt aliiambia mahakama na kuongeza, “Stinney alimuua msichana mdogo (Mary Emma) na kumbaka yule mkubwa zaidi (Betty June). Kisha akamuua msichana mkubwa na kubaka maiti yake. Dakika 20 baadaye alirudi na kujaribu kumbaka tena lakini mwili wake (Betty) ulikuwa wa baridi sana. Haya yote alikiri mwenyewe.”

Lakini maelezo haya ya kubakwa kwa wasichana hao yanatofautiana na taarifa ya madaktari walioifanyia uchunguzi miili ya wasichana wale ambayo ilidokeza kuwa hawakubakwa. Katika taarifa yao madaktari hao walisema wasichana hao “...Sehemu za siri zilikuwa shwari.”

Mawakili wa utetezi wa Stinney hawakuuhoji ushahidi uliokinzana wa Pratt na Newman wa kwamba Stinney “alikiri kubaka” pamoja na kwamba kulikuwa na ripoti ya daktari iliyoonyesha kuwa hawakubakwa. Hii ilitosha kujenga shaka akilini mwa jaji na wazee wa mahakama. Lakini haikuwa hivyo.

‘Watetezi’ wa Stinney wangeweza kuuliza kama wanasheria walipata nguo na viatu vilivyo na damu nyumbani kwa kina George Stinney. Wangeweza kupinga mlolongo wa matukio katika taarifa hizo mbili ambazo zilionekana kutofautiana na kupingana. Kwa mfano, Stinney alikutana vipi na hao wasichana na wapi?

Taarifa ya mchunguzi wa maiti, Newman ilisema George alimweleza kuwa alikutana na wasichana hao wawili walipokuwa wakichuma maua karibu na kiwanda cha mbao. Lakini baadaye Newman huyohuyo katika ushahidi wake akasema Stinney alidai kuwa aliwafuata kwa takriban nusu maili kabla ya kukutana nao ana kwa ana msituni.

Wangeweza kusema kwamba maungamo mawili ya Newman na Pratt yaliyohusishwa na George Stinney yalikuwa yanapingana kabisa. Katika hali yake ya kwanza, Stinney alidaiwa kusema wasichana hao wawili walimshambulia alipokuwa akitaka kumsaidia Mary baada ya kuanguka kwenye shimo.

Hata hivyo, kama aliungama, alimuungamia nani? Kwanini maofisa hao wawili waliikataa kauli yake ya kwanza wakidai ni ya uongo lakini wakaikubali ile ya pili wakadai ni ya kweli kwamba aliwafuata wasichana hao ili “kuwabaka,” mara mbili akijaribu kumbaka Betty na kuwaua wote wawili katika mchakato huo?

Wangeweza kuuliza kuhusu mlolongo wa matukio katika eneo la uhalifu. Ikiwa George aliwaambia Newman na Pratt kwamba aliwaua, kumbaka mmoja wao, akaacha miili, akarudi dakika 20 baadaye kujaribu kuwabaka tena hata baada ya wao kufa, na kisha akaweka baiskeli juu yao, ilikuwaje miili hiyo ikakutwa shimoni?

Au alikuwa amekiri kwamba aliitupa miili ya wasichana hao kwenye shimo lililojaa maji, baadaye akawatoa halafu akaweka baiskeli juu yao?

Lakini ripoti ya daktari aliyechunguza miili ile silaha iliyotumika ni bomba “nene kama kidole gumba.”

Nini ambacho upande wa utetezi ungeweza kufanya?

Tukutane toleo lijalo.