Mawaziri wawili Malawi wafariki dunia kwa corona

New Content Item (1)
Mawaziri wawili Malawi wafariki dunia kwa corona

Muktasari:

Ugonjwa wa virusi vya corona umechukua maisha ya mawaziri wawili wa Serikali ya Malawi, wakati dunia ikianza kutoa chanjo za kujikinga dhidi ya janga hilo.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa virusi vya corona umechukua maisha ya mawaziri wawili wa Serikali ya Malawi, wakati dunia ikianza kutoa chanjo za kujikinga dhidi ya janga hilo.

Waziri wa Serikali za Mitaa, Lingson Belekanyama, na wa Usafirishaji na Ujenzi, Sidik Mia, walifariki dunia jana kwa ugonjwa huo uliopewa jina la Covid-19, imeandika tovuti ya southerntimesafrica.com.

New Content Item (1)
Mawaziri wawili Malawi wafariki dunia kwa corona

Tovuti hiyo imemkariri msemaji wa Serikali ya Malawi, Gospel Kazako na Waziri wa Afya, Khumbize Kandodo Chiponda wakithibitisha vifo hivyo kwa nyakati tofauti.

“Malawi imempoteza mzalendo halisi, mfanyakazi hodari,” alisema Kazako akimzungumzia Berekanyama akikaririwa na news18.com, na baadaye kuangua kilio redioni wakati akitangaza taarifa ya kifo hicho.

Vifo vya viongozi hao vimetokea wakati Malawi ikirekodi maambukizi mapya 452 na kufanya idadi ya walioambukizwa kufikia 2,744, huku waliofariki kutokana na ugonjwa wa virusi hivyo vipya katika jamii ya corona, wakiwa watu 230 hadi juzi. Mgonjwa wa kwanza alitangazwa Aprili 2, 2020.

Wiki iliyopita, kamati maalumu ya rais ya Covid-19 ilisema Belekanyama alikutwa na maambukizi ya virusi hivyo na kuamua kujitenga.

Belekanyama alikuwa mjumbe wa kamati hiyo ya rais, southerntimesafrica.com imeandika.

Kwa upande mwingine, Mia alitangaza katika ukurasa wake wa Facebook kuwa amepata maambukizi ya corona.

Mawaziri hao walikuwa wanachama waandamizi wa chama tawala cha MCP, chama kikubwa katika muungano uliomuondoa kiongozi wa zamani wa Malawi, Peter Mutharika katika raundi ya pili ya uchaguzi wa Juni mwaka jana, na kumpa ushindi Rais Lazarus Chakwera.

Mia pia anasemakana angekuwa mrithi wa Chakwera.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya redio Jumapili, Rais Lazarus Chakwera alilishauri Taifa kutoingiza siasa katika janga hilo badala yake wananchi wafanye kazi kukabili tishio dhidi ya wote linalotokana na virusi vipya vya corona.

Jeshi la Polisi la Malawi limesambaza maofisa wake nchi nzima kuhakikisha wananchi wanafuata masharti yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuzuia mikusanyiko, uvaaji wa lazima wa barakoa na kutokaribiana.

Mwaka jana, mbunge wa Malawi ambaye aliripoti kupata maambukizi ya corona, Cornelius Mwalwanda, alifariki dunia kwa ugonjwa huo.

Mwalwanda, ambaye alikuwa mwanachama wa Chama tawala cha MCP aliandika katika mitandao ya kijamii kuwa amepata maambukizi ya Covid-19, katika kipindi ambacho wabunge wengine watatu waliambukizwa na kumlazimisha spika kuwataka wabunge wote 193 kwenda kupima.

Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Malawi, Francis Perekamoyo, na katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Ernest Kantchentche, pia walifariki dunia kwa ugonjwa huo, serikali ilitangaza.

Desemba 21, mawaziri wote 21 wa Malawi walihudhuria kikao ofisini kwa rais na siku iliyofuata, Waziri wa Kazi, Ken Kandodo aliripotiwa kupata maambukizi na baadaye akapona. Waziri mwingine, Rashid Gaffar, amejiweka karantini nyumbani kwake.

Kulikuwa na mikusanyiko kadhaa, sala na mazishi katika kipindi cha Krismasi ambayo Chakwera na viongozi wengine walihudhuria, na yote ilirushwa moja kwa moja na televisheni ya Serikali.