Mayai ya kuku wa kisasa yadaiwa kuwa hatari

Muktasari:

Akizungumza leo wakati alipozindua bodi  mpya ya ushauri ya wizara kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), Mwalimu amesema amehakikishiwa na wataalamu hao kuwa dawa zinazotumika kwenye mayai na kuku hao zinabaki ambapo si salama kwa afya ya binadamu.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mayai ya kuku wa kisasa yanayotengenezwa nchini  yamedaiwa kuwa na mabaki ya dawa ambazo ni hatari kwa  afya ya binadamu.
Akizungumza leo wakati alipozindua bodi  mpya ya ushauri ya wizara kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA), Mwalimu amesema amehakikishiwa na wataalamu hao kuwa dawa zinazotumika kwenye mayai na kuku hao zinabaki ambapo si salama kwa afya ya binadamu.
Mwalimu amesema kutokana na dawa hizo kubaki kwenye mayai na kuku hao ameitaka TFDA kufanya utafiti  ili kujua  kiwango kipi cha dawa zilizopo ili  Serikali iweze kuchukua hatua za  haraka.
“Hivyo tuwaachie TFDA waendelee na utafiti wao na wanapobaini ni kiasi gani cha dawa zilizomo kwenye mayai na kuku hao watuambie haraka dawa zipi hazitakiwi na zipi zinatakiwa ili kulinda soko la ndani,”amesema.
Pia amewatahadhalisha wataalamu wa TFDA wasihofie kutoa majibu haraka kwa kufikiri kuwa watakwamisha soko la ndani hivyo wanatakiwa wawe wa kweli ili tatizo lililopo liweze kupunguzwa.