Mazungumzo, ahadi tata za Russia, Magharibi

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona kwamba kupanuka kwa Nato (Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi) kuelekea Mashariki ndiko kunakotajwa kama mojawapo ya sababu kuu za ugomvi kati ya nchi hiyo na nchi za Magharibi.

Katika toleo lililopita tuliona kwamba kupanuka kwa Nato (Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi) kuelekea Mashariki ndiko kunakotajwa kama mojawapo ya sababu kuu za ugomvi kati ya nchi hiyo na nchi za Magharibi.

Vilevile ni mojawapo ya sababu za nchi hiyo chini ya Rais Vladmir Putin, kuivamia Ukraine.

Swali lililobaki kiporo katika toleo lililopita ni je, Putin anaiona Nato kama “mpinzani wake mkuu”? Na kama ndivyo kwa nini?

Isitoshe, mwishoni mwa Vita Baridi Nato ilirekebisha dhamira yake ya kuifanya “Ulaya nzima kuwa huru na kwa amani” na kuanzisha ushirikiano na Russia.

Pia imetafuta kufanya kazi na Russia katika vikao kadhaa, lakini jitihada nyingi hazijafaulu.

Ukitazama kutokea nyuma ya pazia, ni wazi kwamba Marekani na washirika wake katika miaka ya 1990 hawakuweza kutengeneza njia ya kujiweka katika hali ya usalama, ambayo Russia nayo ingejisikia salama pia.

Kile kilichoitwa “Ulaya nzima kuwa huru na kwa amani” kilikamilika bila kuihusisha nchi kubwa zaidi ya Ulaya, ambayo ni Russia.

Lakini je, Russia ilitaka kujumuishwa katika mpango huu? Je, nchi za Magharibi zilipaswa kuvunja Nato mwaka 1991 na kufanya kazi na Russia kuweka muundo mpya wa usalama ambao sheria za Moscow zingeruhusu watawala wa Russia kuwa sauti sawa katika kuamua mambo?

Ikiwa Nato sasa ingefifia na kuondoshwa kabisa, kama vile ilivyowahi kupendekezwa na Donald Trump, Rais wa zamani wa Marekani na Putin, je, hiyo ingeleta enzi mpya ya kuboreshwa kwa uhusiano kati ya Russia na nchi za Magharibi?

Ni ahadi gani alizopewa—au ambazo hakupewa Rais wa iliyokuwa Urusi kabla ya kusambaratika, Mikhail Gorbachev na baadaye Rais wa Russia, Boris Yeltsin kuhusu Nato? Na Russia chini ya Putin ina mtazamo gani kuhusu kuimarika kwa Nato?

Utata mwingi kuhusu ahadi aliyopewa Gorbachev unatokana na mazungumzo kadhaa ambayo kiongozi huyo wa Soviet aliyafanya Februari 1990, miezi mitatu baada ya kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, wakati Marekani ilikuwa ikijadili jinsi mazungumzo juu ya muungano wa Ujerumani yatapangwa na kabla ya Ujerumani Mashariki haijafanya uchaguzi huru wa kwanza Machi 18, 1990.

Katika hatua hii Gorbachev alitumaini kwamba Mkataba wa Warsaw (Makubaliano ya Muungano ya Kijeshi ya Umoja wa Kisovieti na nchi saba za Ulaya) ungeweza kudumu na kwamba Ujerumani iliyoungana inaweza kuwa ya kambi zote mbili za kijeshi (Nato na Warsaw) au bila kuwa na kambi yoyote.

Januari 1990, Hans-Dietrich Genscher, waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Magharibi katika hotuba yake alitangaza kwamba Ujerumani iliyoungana (Ujerumani Mashariki na Magharibi) itakuwa mwanachama wa Nato, lakini “hakutakuwa na upanuzi wa eneo la Nato kuelekea mashariki.”

Ijumaa ya Februari 9, mwaka huohuo, Gorbachev alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, James Baker, ambaye alimhakikishia kwamba Marekani na washirika wake watahakikisha “hakuna upanuzi wa mamlaka ya Nato kwa vikosi na hata kwa nchi moja kuelekea mashariki,” akimaanisha hakuna wanajeshi wa Nato wasio Wajerumani ambao wangepelekwa kwenye eneo la iliyokuwa Ujerumani Mashariki.

Lakini ingawa washiriki walikuwa wanazungumza tu kuhusu wanajeshi wa Nato kutowekwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani, yaani Ujerumani Mashariki (GDR), ni kweli kwamba dhana ya “mamlaka” ya Nato kutoenea hadi sehemu ya eneo la nchi mwanachama, haikuwa na maana.

Wakati wa mazungumzo ya Gorbachev na Kansela Helmut Kohl siku iliyofuata, Kohl alifafanua kile ambacho Baker alikisema, akimhakikishia kiongozi wa Urusi kwamba sehemu ya mashariki ya Ujerumani iliyoungana inaweza kuwa na “hadhi maalumu” katika Nato.

Kwa mujibu wa Kramer, rekodi kutokana na mazungumzo haya zinaonyesha kuwa hakuna wakati mada ya upanuzi wa Nato zaidi ya Ujerumani iliwahi kujadiliwa.

Gorbachev hakuwahi kupata hakikisho lolote kuhusu suala hili, wala hakuomba.

Hatimaye alikubali Julai katika mkutano na Kohl kwamba Ujerumani iliyoungana inaweza kubaki katika Nato. Lakini upanuzi wa Nato haukuwa katika akili ya mtu yeyote wakati huo.

Katika kitabu cha maisha yake alichokipa jina la ‘On My Country and the World’, Gorbachev anasema katika mazungumzo yake na Baker alisema kwamba upanuzi wowote wa Nato hautakubalika.

Aliyekuwa balozi wa Marekani nchini Urusi (1987 hadi 1991), Jack Matlock, pia alitoa ushuhuda wake kwamba Gorbachev alipokea “ahadi ya wazi kwamba ikiwa Ujerumani mbili zitaungana na kubaki katika Nato, mipaka ya umoja huo haitasonga kuelekea mashariki.”

Hayo pia yameandikwa katika waraka unaoitwa ‘Sera ya Marekani Kuelekea Upanuzi wa Nato’.

Kwa kuwa mazungumzo haya yalihusisha ahadi za mdomo, si za maandishi, haiwezekani kuthibitisha au kukanusha yale ambayo washiriki walidhani wamesikia.

Gorbachev huenda aliamini baadaye kuwa alisikia kutoka kwa Baker, Bush, Kohl na Genscher kwamba hakutakuwa na upanuzi wa Nato, lakini hakuna hata mmoja wa mshiriki katika mazungumzo hayo kutoka nchi za Magharibi ambaye alikuwa akifikiria juu ya kuipanua Nato wakati wa mazungumzo makali juu ya umoja wa Ujerumani.

Kwa hakika, mwaka 2014 Gorbachev alitoa mahojiano aliyofanya akisema, “mada ya ‘upanuzi wa NATO’ haikujadiliwa kabisa, na haikuletwa katika miaka hiyo. Nayasema haya kwa uthabiti kamili ... Suala jingine tuliloleta lilijadiliwa: Kuhakikisha kwamba ... nguvu za ziada kutoka kwa muungano hazitapelekwa kwenye eneo la GDR ya wakati huo baada ya kuungana tena kwa Wajerumani.”

Gobachev aliyasema hayo alipohojiwa na Maxim Korshunov wa kituo cha runinga TV-Novosti katika kipindi kinachoitwa ‘Russia Beyond’ kilichorushwa Oktoba 16, 2014, yaliyoitwa “Mikhail Gorbachev: I Am Against All Walls.”

Hata hivyo, hadithi kuhusu kile kinachodaiwa kuwa kiliahidiwa zinaendelea, na madai kuhusu kuvunjwa kwa ahadi yamekuwa ya kina zaidi na ya kupita kiasi, kwani uhusiano kati ya Russia na nchi za Magharibi umezidi kuzorota.

Je, upanuzi wa Nato ulikuwa “kosa baya zaidi la sera ya Marekani katika enzi ya baada ya Vita Baridi kama George Kennan alivyodai?

Kupata jibu la swali hili, tukutane toleo lijalo.