Mbaroni kwa kulewesha abiria kwenye basi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Polisi mkoani Mara inamshikilia Marco Saidi (68) mkazi wa kijiji cha Rugasha Bukoba Vijijini kwa tuhuma za kuwalewesha abiria kwenye mabasi yafanyayo safari zake kati ya Mwanza – Musoma na kuwaibia

Musoma. Polisi mkoani Mara inamshikilia mkazi wa kijiji cha Rugasha Bukoba Vijijini, Marco Saidi (68) kwa tuhuma za kuwalewesha abiria kwenye mabasi yanayofanya safari zake kati ya Mwanza-Musoma na kuwaibia

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa leo Desemba 7, 2021

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibushubwamu amesema kuwa mtuhumiwa huyo amekamatwa katika kituo cha mabasi wilayani Bunda mkoani Mara baada ya kumywesha abiria mmoja.

Kamanda Tibishubwamu amesema kuwa mtu huyo anadaiwa kuwalisha na kuwanywesha abiria dawa za kienyeji zinazojulikana kwa jina la khabharagata kutoka nchini Congo kwa lengo la kuwalewesha abiria na kuwaibia mali zao.

Amesema mtu huyo akishirikiana na watu wengine watano (bado hawajakamtwa) wamekuwa wakiwanywesha abiria dawa hizo kwa kuziweka kwenye maji au soda na kupaka kwenye biskuti au pipi kisha kuwapa abiria ambao baada ya kunywa ujikuta wamelewa na kupoteza fahamu.

"Walikuwa wanaweka kwenye kinywaji au anapaka kwenye shati lake eneo la mkononi kisha anasubiri abiria akishakaa yeye anapitisha mkono kama anafungua au kufunga  dirisha wakati huo mkono wake anauelekeza kwenye pua ya abiria hivyo abiria anajikuta amevuta hewa baada ya hapo mtu analewa na kupoteza fahamu au anakupa pipi ama biskuti ukila unalewa kisha anaiba na kushuka kabla hajagundulika" amesema

Kamanda huyo amesema kuwa matukio ya watu kuleweshwa wakiwa kwenye mabasi yalianza kutokea mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu huku watu kadhaa wakijikuta wameibiwa na kwamba baadhi yao walilazimika kukimbizwa hospitalini baada ya kukutwa wakiwa kwenye hali mbaya.

Amesema kuwa katika maelezo ya awali mtuhumiwa huyo amekiri kufanya vitendo hivyo katika mikoa kadhaa ikiwemo Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma na Dar es slaama huku akisema kuwa kwa sasa makazi yake alihamishia jijini Nairobi huku akija nchini kwaajili ya kufanya uhalifu huo.

Mmoja wa watu waliokutana na kadhia hiyo, Maulidi Omary licha ya kumtambua mtuhumiwa huyo lakini amesema kuwa alijikuta akiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara mjini Musoma akiwa amelazwa baada ya kupoteza fahamu kwa muda wa siku tatu.

"Nilikuwa natokea Mwanza kuja Musoma lakini mwisho wa siku nikajikuta nipo hospitalini na kwenye tukio nilipoteza vitu vyangu zikiwemo simu zangu mbili, fedha taslimu pamoja na vitambulisho vyangu" amesema Omary.

Mwisho