Mbaroni kwa kumuua mpenzi wake kisa wivu wa mapenzi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo.
Muktasari:
- Tukio hilo la mauaji limetokea Mei 21, 2025 saa 1 asubuhi ambapo mtuhumiwa anadaiwa alimchoma mpenzi wake kwa kutumia kisu, hali ilisababisha kutokwa na damu nyingi na kisha kufikwa na umauti papo hapo.
Musoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Machegere Wambura (52), mkazi wa Kijiji cha Robanda kilichopo Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake kutokana na ugomvi uliotokana na wivu wa mapenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Ijumaa Mei 23, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amemtaja marehemu kuwa ni Jane Nyamosenga (45), mkazi wa Kijiji cha Robanda.
Amesema tukio hilo la mauaji limetokea Mei 21, 2025 saa 1 asubuhi ambapo mtuhumiwa inadaiwa alimchoma mpenzi wake kwa kutumia kisu, hali ilisababisha kutokwa na damu nyingi na kisha kufikwa na umauti papo hapo.
Kamanda Lutumo amesema Wambura anadaiwa kusababisha kifo hicho baada ya kukataliwa na mpenzi wake baada ya kumtuhumu kujihusisha na vitendo vya wizi pamoja na ujangili ndani ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
“Hawa watu walianza uhusiano wakiwa watu wazima na wakati wakiendelea na uhusiano wao, mwanamke aligundua mwanaume ni mwizi na jangili, hivyo aliamua kuachana naye, uamuzi ambao pia uliungwa mkono na watoto wa mwanamke lakini mwanaume hakukubaliana na uamuzi huo,” amesema.
Amesema siku ya tukio, mwanamke huyo akiwa ameamka nyumbani kwake kwenye mji wake aliojengewa na watoto wake kijijini hapo akiendelea na shughuli zake za asubuhi, ghafla alivamiwa na Wambura na kuanza kumshabulia kwa kuchomwa na kisu sehemu mbalimbali mwilini mwake, hivyo kutokwa na damu nyingi.
Amesema mtuhumiwa huyo aliwahi kufika katika eneo la tukio mapema na kujificha kwenye miti iliyopo nyumbani kwa mwanamke huyo na baada ya kumuona ametoka nje, alitumia nafasi hiyo kutimiza lengo lake ambalo pia lilifanikiwa kutokana na watu wengi muda huo kuwa kwenye shughuli zao za shamba.
Kamanda Lutumo ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Mara kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafuate njia sahihi za kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.