Mbaroni kwa kuuza watoto kwa Sh20,000

Mbaroni kwa kuuza watoto kwa Sh20,000

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watu watatu (majina yamehifadhiwa) kwa tuhuma za kuwatorosha na kuwauza watoto 13 wenye umri wa miaka 10 ili wakatumikishwe kazi majumbani na kuchunga mifugo wilayani Mbarali mkoani hapa.

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watu watatu (majina yamehifadhiwa) kwa tuhuma za kuwatorosha na kuwauza watoto 13 wenye umri wa miaka 10 ili wakatumikishwe kazi majumbani na kuchunga mifugo wilayani Mbarali mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Urlich Matei ameliambia Mwananchi jana Jumanne Septemba 7, 2021 kuwa waliwakamata watuhumiwa hao baada ya kupokea taarifa za raia wema na walipohojiwa walikiri kujihisisha na biashara ya kusafirisha binadamu kwa ujira wa Sh 20,000 kwa kila mmoja wanapowafikisha wanakotakiwa.

"Tumebaini kuwa licha ya watuhumiwa hao kuwatorosha watoto wengine lakini kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakikubaliana nao pasipo kujua ni kinyume cha sheria na kunyima uhuru wao wa kupata elimu na makuzi katika familia "amesema

"Tunaendelea na uchunguzi ikiwa ni pamoja na watoto hao kurejeshwa kwenye familia zao na kitendo cha kusafirisha binadamu ni kinyume cha sheria za nchi hivyo watuhumiwa watafikishwa mahakamaniĀ  wakati wowote mara baada ya uchunguzi kukamilika"amesema.

Amesema Jeshi la Polisi halitovumilia uvunjwaji wa sheria kwakuwa watoto hao bado ni wadogo na kitendo cha kutumikishwa kaziĀ  majumbani na kufuga mifugo hakivumiliki.

Amesema imeamua kutoa elimu bure hivyo mzazi yoyote atakayeendekeza tamaa lazima ya kumzuia mtoto wake asisome ni lazima atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Matei ametoa onyo kwa watu wote wanaojihusha na matukio ya kusafirisha binadamu hususan kwa watoto kuacha kufanya hivyo kwakuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwakuwa kitendo hicho kinakatisha ndoto za watoto kupata elimu na kujikuta wakifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza na Mwananchi kuhusiana na tukio hilo, Mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali Sauti ya Mama Afrika linalotoa elimu mashuleni ya ukatili wa kijinsia ,Thabitha Bughali alikemea kitendo hicho na kuomba jeshi la polisi kulivalia njuga kwakuwa limewaathiri kisaikolojia watoto hao.

"Jamani kweli Serikali imetoa elimu bure kwa watoto mzazi unakubali kulaghaiwa kwa fedha na mtoto anakosa elimu?, tunaomba jambo hili likomeshwe ili watoto wapate haki ya kupata elimu bora na si bora elimu. "amesema.

Amesema kuwa kwa miaka ya hivi karibuni wanakutana na kesi nyingi za watoto kutoroshwa na kunyanyaswa kwenye maeneo wanayokwenda kutumikishwa kazi majumbani na wengine kuolewa wakiwa na umri mdogo hivyo Jeshi la polisi liwabane watuhumiwa hao wataje wazazi wa watoto walijihusisha na biashara hiyo.